SERIKALI kupitia Baraza la Michezo la Taifa (BMT), imeidhinisha marekebisho ya katiba ya Klabu ya Simba baada ya kukamilika kwa mchakato wa kisheria uliokuwa chini ya Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Michezo.
Ikumbukwe Februari 16, mwaka huu, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Paul Makonda alimuagiza Msajili wa Vyama vya Michezo kuhakikisha kuwa mchakato wa katiba ya Simba unakamilika kabla ya mwezi huu kwisha.
Akizungumza leo, Februari 18, 2026, Msajili wa Vyama vya Michezo nchini, Abel Mathias Ngilungwa amesema marekebisho hayo yamefanyika kwa kuzingatia sheria na kanuni zote zinazosimamia vyama vya michezo.
“Napenda kuufahamisha umma kuwa mchakato wa uchambuzi, tathmini na uidhinishaji wa marekebisho ya Katiba ya Klabu ya Simba umekamilika kwa mujibu wa Sheria ya Baraza la Michezo la Taifa Sura ya 49 na Kanuni zake,” amesema Ngilungwa
Ameongeza kuwa katiba hiyo iliyorekebishwa iliwasilishwa kwa mujibu wa Kanuni ya 11 ya Kanuni za Msajili wa Vyama vya Michezo T.S Na. 441 ya mwaka 1999 kwa ajili ya kupitiwa na kuidhinishwa.
Vilevile ameeleza kuwa msajili alitekeleza wajibu wake kwa mujibu wa Kanuni ya 11(3)(a) ya Kanuni za Msajili wa Vyama vya Michezo T.S Na. 441 ya mwaka 1999, inayomtaka kuhakikisha marekebisho yoyote ya Katiba hayaathiri usalama, hayavurugi amani miongoni mwa wanachama au jamii kwa ujumla, wala kuathiri maendeleo ya chama.
“Serikali imejiridhisha kuwa marekebisho haya hayaathiri usalama, hayachochei migogoro miongoni mwa wanachama na hayapingani na sheria za nchi, hivyo yameidhinishwa rasmi,” amesema.
Vilevile, katika maboresho hayo, Katiba imezingatia masharti ya Kifungu cha 18A(1) cha Sheria ya Baraza la Michezo la Taifa, Tangazo la Serikali Na. 422/2017, kinachohusu masuala ya umiliki na usimamizi wa vyombo vya michezo vinavyohusisha uwekezaji.
Miongoni mwa maboresho yaliyoidhinishwa ni kuweka wazi nafasi ya Simba Sports Club Company Limited kama chombo kitakachosimamia masuala ya kibiashara na kiutendaji, huku umiliki wa hisa ukiendelea kuwa chini ya Baraza la Wadhamini kwa niaba ya wanachama.
“Lengo siyo kunufaisha watu wachache, bali kuweka uwiano wa haki kati ya wanachama na wawekezaji, sambamba na kulinda misingi ya usajili na umiliki,” ameeleza msajili huyo
Ameendelea kwa kusema Serikali ilibainisha kuwa muundo mpya wa Baraza la Wadhamini utakuwa na wajumbe wasiopungua watano na wasiozidi saba, watakaosimamia mali za klabu kwa niaba ya wanachama, huku Mkutano Mkuu ukiendelea kuwa chombo chenye mamlaka ya mwisho.
Ofisi ya msajili ilizingatia ushauri wa Mwanasheria Mkuu wa Serikali uliotolewa Mei 12, 2025, uliopendekeza kuwepo kwa kampuni moja mahsusi ya kusimamia uendeshaji wa klabu kwa uwazi zaidi.
“Marekebisho haya hayaathiri usalama wala kuvuruga amani ya wanachama. Badala yake, yanalenga kuimarisha utawala bora na kuweka mazingira rafiki ya uwekezaji,” amesisitiza msajili huyo.
Ngilangwa amesisitiza kuwa marekebisho hayo hayahatarishi usalama, hayachochei migogoro miongoni mwa wanachama wala kuathiri maendeleo ya klabu. Badala yake, yanalenga kuweka mazingira rafiki ya uwekezaji na kuondoa mkanganyiko wa kisheria uliokuwepo awali.
Katika hitimisho lake amewataka wanachama na wadau wa Simba kuheshimu maamuzi hayo ya kisheria na kushirikiana katika utekelezaji wake, likisisitiza kuwa lengo kuu ni kuilinda klabu, kuimarisha utawala bora na kusukuma mbele mafanikio ndani na nje ya uwanja.