Dar es Salaam. Mahakama Kuu, Masjala Ndogo Dar es Salaam, imelazimika kuahirisha mapema kesi ya uhaini inayomkabili Mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu, kutokana na mmoja wa mashahidi kufiwa na baba mkwe wake.
Lissu anakabiliwa na shtaka moja la uhaini kinyume na kifungu cha 39(2) (d) cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu, linalotokana na maneno aliyoyatamka kuhusu kusudio la kuzuia kufanyika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.
Anadaiwa Aprili 3, 2025, jijini Dar es Salaam, akiwa raia wa Tanzania, kwa nia ya uchochezi alishawishi umma kuzuia kufanyia kwa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025, huku akitamka na kuandika maneno ya kumshinikiza kiongozi Mkuu wa Serikali ya Tanzania kuwa:
“Wakisema msimamo huu unaashiria uasi, ni kweli…, kwa sababu tunasema tutazuia uchaguzi, tutahamasisha uasi, hivyo ndivyo namna ya kupata mabadiliko…, kwa hiyo tunaenda kikinukisha…, sana sana huu uchaguzi tutaenda kuuvuruga kwelikweli…, tunaenda kukinukisha vibaya sana…”
Kesi hiyo inasikilizwa Mahakama Kuu Masjala Ndogo Dar es Salaam na jopo la majaji watatu linaloongozwa na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Iringa, Dunstan Ndunguru, akishirikiana na majaji James Karayemaha na Ferdinand Kiwonde.
Leo Jumatano, Februari 18, 2026, kabla ya kesi hiyo kuanza kusikilizwa, Wakili wa Serikali Mkuu, Renatus Mkude, ameieleza mahakama hiyo, shauri hilo limeitwa kwa ajili ya kuendelea na usikilizwaji, lakini mmoja wa mashahidi wa kesi hiyo amepata msiba, lakini wana shahidi mwingine ambaye atatoa ushahidi.
“Mheshimiwa Jaji, kabla ya kuendelea kuna jambo tunataka kuieleza mahakama hii, leo alfajiri tumepokea simu kutoka kwa mmoja wa mashahidi wetu, ametuambia amefiwa na baba mkwe wake, hivyo kutokana na mazingira yalivyo na kwa kuwa msiba huo upo hapa hapa Dar es Salaam, tunaomba apewe nafasi ya kwenda kushiriki msiba huo,” amedai Mkude.
Lissu alipopewa nafasi ya kuzungumza kuhusiana na shahidi huyo kupewa ruhusa ya kushiriki msiba, amesema hana pingamizi la shahidi huyo kupewa ruhusa ya kuhudhuria msiba.
“Waheshimiwa majaji, niko tayari kuendelea na usikilizwaji na sina pingamizi la shahidi kupewa ruhusu ya kwenda kuhudhuria msiba, ila maelekezo ya mahakama hii yalikuwa upande wake wa mashtaka uwe na mashahidi wasiopungua watatu,” amedai Lissu.
Hata hivyo, wakili Mkude amedai hawakuandaa mashahidi wengi kwa kuwa shahidi huyo aliyefiwa ana ushahidi mrefu.
Baada ya ufafanuzi huo, Lissu amekubaliana na maelezo ya upande wa Jamhuri na kisha shahidi wa 11 ambaye ni wa kificho alitoa ushahidi wake kuanzia saa 3:47 asubuhi hadi saa 6 na dakika 5 mchana.
Kesi hiyo itaendelea kesho Alhamisi Februari 19,2025