Mbeya. Hebu fikiria utapata maumivu kiasi gani pale ulipoagana vizuri na mtoto wako mdogo akaenda shule, lakini hakurudi. Baadaye unapokea simu kutoka kwa mtu anayehitaji Sh10 milioni ili amwachie huru.
Lakini utapata maumivu ya kiakili na kisaikolojia kiasi gani unapogundua kuwa mtekaji huyo amemuua mwanao kwa kuchelewa kutuma fedha hizo, kisha akautupa mwili wake katika eneo la Igawilo, Mlimanyoka, katika Jiji la Mbeya.
Hiki ndicho alichokifanya Mussa Mbelechamo baada ya kumteka mtoto wa Bakari Siame aitwaye Junior wa Jijini Mbeya. Tukio lililotokea Aprili 9, 2019 na simu alizopiga kuomba pesa ndizo zilizomkamatisha.
Katika kuhangaika kuokoa maisha ya mwanae, siku iliyofuata baba mzazi alimtumia mtekaji Sh32,000 na akazitoa, kisha akamtumia tena Sh100,000, lakini safari hii muamala huo ulikuwa umezuiwa ili mtekaji asiweze kuzitoa.
Julai 6, 2023, Jaji Victoria Nongwa wa Mahakama Kuu, Kanda ya Mbeya, alimtia hatiani na kumhukumu kunyongwa hadi kufa. Akakata rufaa, lakini Mahakama ya Rufani katika uamuzi wake wa jana, Februari 17, 2026, ilibariki adhabu hiyo.
Jopo la majaji watatu wa Mahakama ya Rufani walioketi Jijini Mbeya, Rehema Kerefu, Lucia Kairo na Dk Deo Nangela, walisema wameridhika na uchambuzi wa jaji aliyemhukumu kwamba hakuna mtu mwingine aliyemuua Junior isipokuwa yeye.
Simulizi ya utekaji huo inaanzia Aprili 9, 2019, ambapo Junior (8), ambaye ni mtoto wa Siame, alitekwa nyara na Mbelechamo wakati anarudi nyumbani kwa wazazi wake akitokea shule.
Baadaye mtekaji huyo, aliyejitambulisha kwa majina yake, alimpigia simu baba mzazi wa Junior akimtaka ampe Sh10 milioni ili amwachie mwanae, na alikwenda kutoa taarifa Polisi Ilombe na kukabidhi namba ya simu iliyompigia.
Siku iliyofuata (Aprili 10, 2019), baba mzazi wa Junior alimtumia mtekaji Sh32,000, na Aprili 12, akamtumia tena Sh100,000, lakini muamala huo ulikuwa umezuiwa na kampuni ya Vodacom ili usiweze kutolewa.
Pamoja na jitihada zote hizo za baba, Junior hakurejeshwa. Kufuatia hayo, Polisi Kituo cha Kati Mbeya wakaanzisha uchunguzi wa tukio hilo.
Walichoeleza mashahidi wengine
Aprili 10, 2019, shahidi namba 5, Koplo Johnson mwenye namba G.9929, aliyekuwa kachero kutoka Kituo Kikuu cha Polisi Mbeya, alikabidhiwa namba ya Vodacom iliyowasiliana na baba yake Junior kuomba fedha, kwa ufuatiliaji.
Shahidi huyo aliwasiliana na Vodacom ili kupata mawasiliano ya mwisho ya namba hiyo, na ilibainika kuwa mbali na kuwasiliana na baba wa Junior, mtekaji aliwasiliana na watu wengine wawili, Stanley Samwel na Emmanuel Mbilinge.
Samwel alikuwa fundi friji na alikuwa akifahamiana na baba yake Junior, na alieleza mahakama kuwa mtekaji huyo alimpigia simu na kujifanya ana kazi ya matengenezo anayotaka kumpa, na kumwelekeza nyumba ya baba wa Junior.
Baada ya kufika kwa baba wa Junior, na wakati huo akiwa “live” kwenye mawasiliano ya simu na mtekaji, mtekaji alimwelekeza ampe simu baba wa Junior, ndipo alimweleza baba wa mtoto huyo kuwa anahitaji Sh10 milioni ili amwachie.
Hapo baba wa Junior akamtaarifu mkewe kuwa mtoto wao ametekwa na mtekaji alikuwa anahitaji kiasi hicho cha fedha, ili amwachie mtoto wao.
Ilibainika kuwa Mbelechamo (mtekaji) alipata namba ya fundi huyo wa friji kupitia matangazo yake aliyoyaweka mitaani chini ya neno “Fundi friji”.
Ufuatiliaji wa namba ya pili (ya Mbilinge), ambayo mtekaji aliwasiliana nayo, ulianza kwa kumtafuta yuko wapi, na mawasiliano yalionesha yuko Tunduma, Mbeya.
Alipofuatwa na kuoneshwa namba iliyompigia kama anamfahamu, Mbilinge aliwajulisha polisi kuwa namba hiyo ni ya Musa Mbelechamo, na Mbilinge alisaidia kupatikana kwa namba nyingine aliyokuwa akiitumia Mbelechamo.
Namba zote mbili, ile iliyotumika kumpigia baba yake Junior na namba mpya iliyotolewa na Mbilinge, zilikuwa zikitumika katika kifaa kimoja (single device). Zilipochunguzwa, zilionesha zote zipo Iringa na zimesajiliwa kwa jina Musa.
Aprili 12, 2019, shahidi wa tano na maofisa wengine wa Polisi walisafiri hadi Iringa, wakafika siku iliyofuata na kutafuta mahali laini hizo zinasoma (active location), na ilionekana ni Ipogolo, Iringa, na polisi wakafanikiwa kumkamata.
Kulingana na ushahidi, alipoulizwa na polisi mahali alipo Junior, alikiri kwamba alimuua mtoto huyo na kuuacha mwili wake huko Mbeya. Hapo ndipo timu ya makachero ikarudi na mtekaji hadi Mbeya na kuwasili usiku wa manane.
Walipofika Mbeya, Mbelechamo aliwaongoza makachero hao katika eneo alilotupa mwili wa Junior. Walipofika eneo la Mlimanyoka, karibu na barabara, chini ya mti mkubwa katika shamba la mahindi, waliupata mwili wa Junior.
Mwili huo ulikutwa ukiwa umefungwa kwa kutumia fulana kuzunguka shingo, na ulikuwa umelala kifudifundi, na baba mzazi wa Junior aliutambua mwili huo kuwa ni wa mtoto wake aliyekuwa ametekwa.
Aprili 14, 2019, Mkuu wa Upelelezi Wilaya (OC-CID), Kamishina Msaidizi wa Polisi (ACP) Luambano, shahidi wa saba, aliandika maelezo ya onyo ya mtekaji huyo, ambapo alikiri kila kitu, na maelezo hayo yalipokelewa kortini bila kipingamizi.
Katika maelezo hayo, Mbelechamo alieleza mwanzo mwisho kuanzia wazo la kumteka Junior lilivyomjia, namna alivyotekeleza mpango wa kumteka na akaeleza namna mtoto huyo alivyokufa huko Igawilo, eneo la Mlima Nyoka.
Mbelechamo alipopata nafasi ya kujitetea, alikanusha mashtaka na kueleza kuwa yeye alikuwa muuza samaki anayesafirisha samaki kutoka Mwanza, akashikilia msimamo kuwa hana hatia, na kwamba maelezo aliyoyatoa yalitokana na kuteswa.
Baada ya Jaji kupitia ushahidi wa Jamhuri na utetezi wa mshtakiwa, aliona kuwa upande wa Jamhuri ulithibitisha shtaka bila kuacha mashaka, hivyo kumhukumu kunyongwa hadi kufa.
Hakuridhika na adhabu hiyo, akakata rufaa akiegemea sababu tatu kuu, kwanza, jaji aliyesikiliza shauri lake alishindwa kuchambua na kupima kikamilifu ushahidi, pili, shtaka halikuthibitishwa na tatu, utetezi wake haukuzingatiwa.
Hata hivyo, baada ya majaji kusikiliza mawasilisho ya mawakili wa pande zote, kuyachambua na kuyapima, walitupilia mbali rufaa hiyo na kusisitiza kuwa upande wa mashtaka ulithibitisha shtaka dhidi yake katika viwango vinavyokubalika.
Majaji hao walisema wameridhika kuwa jaji aliyesikiliza shauri hilo alipima ushahidi wa Jamhuri ulioletwa mbele yake kwa usahihi, na kwamba si sahihi kusema mahakama hiyo ilishindwa kutimiza wajibu wa kupima ushahidi huo.
Kulingana na majaji hao, hakuna ubishi kuwa upande wa Jamhuri ulithibitisha kuwa Junior ni marehemu na kifo chake si cha asili.
Kuhusu hoja kama ni mrufani ndiye aliyesababisha kifo hicho, majaji hao walisema kipengele hicho kilithibitishwa kwa ushahidi wa mazingira, na ushahidi wa aina hiyo unakubalika ikiwa unamnyooshea kidole mrufani na si mtu mwingine.
Ushahidi huo wa mazingira ambao haukukatika ni kwamba, kwanza, baba mzazi alipokea simu ikimtaka atoe pesa kwa mrufani ili amwachie mwanae, na hilo linathibitishwa na kwamba simu ya pili ilikuwa imesajiliwa kwa jina lake.
Pili, ni kupitia taarifa za laini alizokuwa akitumia ndizo zilizowezesha kukamatwa kwake akiwa eneo la Ipogolo, Iringa na tatu, baada ya kukamatwa, mrufani alikiri kuua na kuwaongoza polisi hadi alipoutupa mwili.
Mbali na mazingira hayo, hoja ya nne ni kuwa mrufani huyo aliandika maelezo ya maandishi ya kukiri kufanya mauaji hayo, ambayo yalipokelewa kama kielelezo P4, na hata kilipotaka kutolewa kortini kama kielelezo, hakukipinga.
Majaji hao walisema katika maelezo hayo, mrufani alieleza mwanzo mwisho namna alivyopata wazo la kumteka Junior na mazingira ya kifo chake, na huo ni ushahidi mzito kwani ulitolewa na mtu anayefahamu Junior alikufaje.
Kuhusu kama alifanya mauaji hayo kwa nia ovu, majaji walisema kupitia maelezo yake ya kukiri kosa inaonesha wazi kuwa aliamua kumteka Junior ili kujipatia fedha, na sababu za kifo zinaonesha alikuwa na nia ya kumuua.
Majaji hao wakahitimisha kwa kusema: “Baada ya kupitia ushahidi kwa ujumla wake, tumeridhika kuwa upande wa mashtaka ulithibitisha shtaka bila kuacha mashaka, hivyo tunaona ni mrufani pekee ndiye aliyemuua mtoto huyo.”
Ni kwa msingi huo, majaji walibariki adhabu ya kifo iliyotolewa awali.