Tanzania ijiweke mguu sawa kwa India

Uhusiano wa Tanzania na India, umejengwa kutoka mbali. Kabla ya uhuru, kisha Tanganyika ilipopata uhuru, India chini ya Waziri Mkuu wa kwanza, Jawaharlal Nehru, ilifungua ubalozi wake Dar es Salaam, Novemba 1962.

Uhusiano ukatanuka baada ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.

Misimamo ya Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere na Nehru, iliendana katika maeneo mengi, hasa kutenganisha dini na siasa, kupiga vita ubaguzi wa aina yeyote na kupambana na ukoloni.

Mwaka 1971, Mwalimu Nyerere alifanya ziara ya kwanza India. Mwaka 1972, Rais wa India Varahagiri “V.V” Giri, alizuru Tanzania. Mwalimu Nyerere alifanya ziara saba akiwa Rais (mwaka 1971, 1976, 1981, 1982, 1983, 1984 na 1985). Na kila Rais wa Tanzania, alitembelea India, kasoro Rais wa Tano, Dk John Magufuli.

Rais wa Pili, Ali Mwinyi alitembelea India mara mbili (mwaka 1989 na 1993). Rais wa Tatu, Benjamin Mkapa, mara moja, mwaka 2002. Kikwete mara mbili (mwaka 2008 na 2015.

Viongozi wakuu wa India, wamekuwa wakitembelea Tanzania. Baada ya Rais V.V Giri mwaka 1972, Makamu wa Rais wa India G.S. Pathak, alizuru Tanzania mwaka 1974 na aliyemfuatia, D.B. Jatti mwaka 1975.

Waziri Mkuu wa vipindi viwili India, Indira Gandhi, alitembea Tanzania mara mbili, mwaka 1976 na 1980. Waziri Mkuu wa Sita wa India, Rajiv Gandhi (mwaka 1986). Waziri Mkuu wa 12, Inder Gujral (1997). Waziri Mkuu wa 13, Manmohan Singh (Mwaka 2011) na Waziri Mkuu wa 14, ambaye ndiye aliye ofisini hivi sasa, Narendra Modi, mwaka 2016.

Mwaka 1989, Tanzania ilimpokea Rais wa Nane wa India, Ramaswamy Venkataraman na mwaka 2004, Rais wa 11 wa nchi hiyo, Abdul Kalam.

Mwaka 1974, Serikali ya India ilimtunuku Mwalimu Nyerere, Tuzo ya Jawaharlal Nehru ya Uelewa wa Kimataifa. Kisha, mwaka 1995, India walimpa Mwalimu Nyerere, Tuzo ya Amani ya Gandhi kwa kufanikisha uhuru wa Tanganyika bila kumwaga damu.

Inathibitishwa bila kuacha shaka kuwa uhusiano wa Tanzania na India una mizizi ya muda mrefu. India ina miaka 78 tangu ilipopata uhuru wake kutoka UK, kadhalika Tanzania miaka 64. Asili ya uhusiano uliojengwa na Mwalimu Nyerere pamoja na Nehru ni tofauti kabisa na mazingira ya sasa.

Miaka ya 1960 hadi 1980, India na Tanzania, zilijenga uhusiano wa kufaana na kuliwazana dhidi ubeberu wa Magharibi. Muongo wa tatu wa Karne ya 21, India ni taifa tajiri na linatarajiwa kuwa kwenye kilele cha dunia miongo mitatu ijayo.

Price Waterhouse Coopers (PwC) ni taasisi ya kimataifa ya mahesabu. Makao yake makuu ni UK. Imo kwenye zile taasisi nne kubwa za utaalamu wa hesabu duniani. Nyingine ni Deloitte, Ernst & Young (EY) na KPMG.

Kwa mujibu wa PwC, matazamio ya kimahesabu ya pato la taifa (GDP), ifikapo mwaka 2050, nchi za Magharibi zitapigwa mweleka. China itashika nafasi ya kwanza, India itakuwa ya pili kwa uchumi mkubwa duniani.

Ripoti ya Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) mwaka 2023, inaonesha kuwa Marekani inaongoza kwa GDP dola 25.035 trilioni (Sh62,500 trilioni), China ikifuatia kwa dola 18.321 trilioni (Sh45,802 trilioni), Japan ipo namba tatu kwa dola 4.301 trilioni (Sh10,752 trilioni).

Katika 10 bora ya IMF, Ujerumani inashika nafasi ya nne, India tano, UK namba sita, Ufaransa saba, nane ipo Canada, Urusi inasimama tisa, halafu Italia inafunga 10 bora.

Pamoja na Marekani kuwa kinara na uchumi wake kuwa imara kwa kubebwa na kampuni za teknolojia, IMF inatambua kuwa uchumi wa ushirikiano wa sekta binafsi na umma (PPP), China imeshapiga hatua kubwa na India inafuatia kwa karibu.

PwC, imeweka matazamio kuwa mwaka 2050, China itakuwa kinara, India itakuwa ya pili, Marekani watashika nafasi ya tatu, Indonesia watakuwa namba nne, Brazil watafunga orodha ya tano bora. Sita watakuwa Urusi, saba Mexico, nane Japan, tisa Ujerumani na UK watasalia namba 10.

Nyakati zijazo zinazungumza neema nyingi kwa India. Hivyo, Tanzania inahitaji kuendelea kuimarisha uhusiano wake na nchi hiyo, ili iendelee kuijumuisha Tanzania kwenye kitabu chake kizuri.

Tanzania inahitaji kuimarisha uhusiano wake na China, India, Indonesia, Brazil na Mexico, bila kulegeza kwa Marekani, Urusi, Japan, Ujerumani na UK. Hayo ni matakwa ya kujenga na kuimarisha uhusiano wenye manufaa, kulingana na uelekeo wa uchumi duniani.

Ripoti ya Benki ya Dunia, imeitaja India kuwa mnunuzi mkubwa wa malighafi, ikishika nafasi ya sita ulimwenguni. India ni taifa jabali duniani ambalo linaelekea kupata ushindi mkubwa dhidi ya umaskini. Ripoti ya Tume ya Mipango India, inaonesha kuwa kasi ya kubadili maisha ya wananchi kutoka umaskini hadi daraja la kati ni kubwa. Na inahitajika miongo michache, hakutakuwa na Mhindi fukara.

India, nchi yenye idadi kubwa zaidi ya watu ulimwenguni. Ikifikisha watu bilioni 1.4 na kuipiku China, Aprili 2023, imekuwa na wastani wa kuwavusha watu milioni 130 kila miaka 10, kutoka umaskini hadi daraja la kati. Wastani wa kuishi wa wananchi wa India ni miaka 70.

Tanzania inahitaji maarifa ya mageuzi ya kimaisha ya wananchi. Watanzania wapo milioni 62 tu. Inawezekana kabisa kuushinda umaskini na Tanzania isiwe na raia fukara ndani ya miongo michache kama itasoma mbinu ambazo India watazitumia.

India ni taifa linalotamba kwa ufahari mkubwa kwamba linaongoza kwa demokrasia duniani na limeweza kujenga uchumi mkubwa wakati likijenga na kuimarisha misingi ya kidemokrasia.

Tazama taifa ambalo linapiga hatua kubwa kiuchumi na kuelekea kileleni, likizipiku nchi ambazo zamani ilizinyenyekea, bila kuminya uhuru wa maoni wala kuchomoza makucha ya udikteta, lipo lilipo.

Tanzania lazima ijiweke mguu sawa India, ukizingatia ni nchi jirani, zikitenganishwa na Bahari ya Hindi.