Tanzania yaanika ilichokipata mkutano COP30, Brazil

Dar es Salaam. Tanzania imesema kupitia Mkutano wa 30 wa Nchi Wanachama wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi (COP30) uliofanyika Belem Brazil Novemba mwaka 2025, imekubaliana na nchi washiriki juu ya vigezo na viashiria vya namna ya kupima athari za mabadiliko ya tabianchi kwenye sekta mbalimbali na  kuona yanavyoweza kufuatiliwa.

Pia, fedha za mfuko wa kushughulikia mabadiliko ya tabianchi ambao kwa ujumla umepewa dola 250 milioni (zaidi ya Sh648 bilioni) ambapo kila nchi itapata dola milioni 20 (Sh52 bilioni) kwa mradi mmoja, huku Tanzania ikisema imeshaanza kujiandaa.

Hayo yamebainishwa na Mkurugenzi Msaidizi Kitengo cha Mabadiliko ya Tabianchi na Tathmini ya Mazingira, Ofisi ya Makamu wa Rais, Dk Kaninzio Manyika wakati akizungumza kwenye kongamano la kujadili matokeo ya mkutano wa COP30 ulioandaliwa na taasisi ya CAN Tanzania jijini Dar es Salaam.

Dk Manyika amesema vilevile kwenye mkutano huo, Tanzania imefanikiwa kuzibebesha nchi za Afrika ajenda ya nishati safi ya kupikia iliyoasisiwa na Rais Samia Suluhu Hassan ambayo utekelezaji wake unaanzia ngazi ya chini.

“Vijana wa vyuo vikuu wanatakiwa kuja na bunifu na teknolojia za kusaidia kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi kuanzia ngazi ya familia hadi Taifa, kwa kuwa ni ajenda iliyokubalika na kupitishwa,” amesema.

Dk Manyika amesema nchi zilizoendelea zinazopaswa kutoa fedha kwa sasa zimekubali kuongeza mara tatu ya fedha hizo za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, huku nchi zinazoathiriwa zikitaka zisiishie tu kwenye ahadi.

Ikumbukwe Tanzania ilienda COP30 ikiwa kama Mwenyekiti wa Kundi la Majadiliano la Afrika kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi (AGN), ambapo ilihimiza masuala yote yanayohusu bara hilo kupewa kipaumbele pamoja na hoja ya upatikanaji wa umeme wa bei nafuu kwa watu wote.

Mkurugenzi wa taasisi ya CAN Tanzania, Dk Sixbert Mwanga amesema zaidi ya asilimia 70 ya ajenda zilizobebwa na Tanzania kwenye mkutano wa COP30 zilifanyiwa kazi kama ahadi ya mara tatu ya fedha kutoka nchi zilizoendelea.

“Hapa tunapaswa kuhakikisha teknolojia na fedha zinawafikia watu wa mwisho, pia tuhakikishe tunahuisha mipango yetu ya kila sekta ili tuweze kustahimili mabadiliko haya,” ameshauri.

Mkurugenzi Taasisi ya Women in Climate Tanzania, Sylviabay Kijangwa amesema bado kunahitajika utekelezaji wa sera na mikakati inayojadiliwa kwenye mikutano juu ya kukabiliana na athari za mabadiliko hayo kwa kundi la wanawake.

“Wanawake wanapewa nafasi ya kuhudhuria mikutano hiyo lakini utekelezaji huku chini bado. Tunataka utekelezaji zaidi ya matamko,” amesema.

Naye, Balozi wa Ireland nchini Tanzania, Nicola Brennan amesema mabadiliko ya tabianchi bado yanaziathiri jamii, hivyo vijana hawawezi kukaa kimya au kukata tamaa kiasi cha kushindwa kuchukua hatua.

“Vijana wanatakiwa kuendelea kuwa na ujasiri na kutochoka katika mapambano ya haki ya tabianchi. Ireland haitazami tu bali imejitolea kusimama bega kwa bega na vijana wa Kitanzania, kusaidia uongozi wao, kuimarisha ushirikiano, na kuwekeza katika suluhisho zitakazoleta matokeo ya kweli pale yanapohitajika zaidi,”amesema.