Vizingiti vinavyofanya safari ya Katiba mpya kuwa ndefu

Dar es Salaam. Safari ya Tanzania kuandika Katiba mpya imeendelea kuwa ndefu kukiwa na ahadi ya kisiasa zinazojirudia bila hatua ya utekelezaji.

Katika safari hiyo ya kisiasa nchini, mahitaji ya Katiba mpya yameendelea kubainishwa kwa zaidi ya miongo mitatu; Tume mbalimbali zilizotumia rasilimali za umma, zimeundwa mara kadhaa kwa lengo la kushauri mageuzi ya kisiasa na kikatiba bila mafanikio.

Hatua hizo zimeanza tangu utawala wa awamu ya pili chini ya Rais Ali Hassan Mwinyi (1985-1995), Benjamin Mkapa (1995-2005), Jakaya Kikwete (2005-2015), John Magufuli (2015-2021) na Samia Suluhu Hassan 2021-hadi sasa), lakini Katiba mpya haijapatikana.

Katika vipindi hivyo, dhamira za maneno zilielezwa, lakini vizingiti viliendelea kuibuka hasa katika muda wa utekelezaji wa ahadi na hivyo kufanya safari hiyo kuwa ya miiba isiyofika mwisho.

Ukiacha harakati na ahadi za miaka ya 1990, tangu mwaka 2014, rasimu iliyotokana na Tume ya Mabadiliko ya Katiba iliyoongozwa na Jaji Joseph Warioba ilipokwama mwaka 2014, zimekuwepo kauli nyingi tofauti zinazozidi kurefusha safari hiyo.

Awamu ya tano chini ya Rais John Magufuli, iliyoingia madarakani Novemba 5, 2015 ilichukua msimamo wa wazi kwamba kipaumbele chake si Katiba mpya, kauli iliyorefusha zaidi safari ya mchakatp huo.

Mabadiliko ya uongozi yaliyomwingiza Rais Samia Suluhu Hassan mwaka 2021 baada ya kifo cha Magufuli, yaliashiria kufungua ukurasa mpya wa maridhiano ya kisiasa, kufufua michakato ya kitaifa iliyokwama kama mchakato wa Katiba mpya na kupanua wigo wa kidemokrasia, ikiwemo kuruhusu mikutano ya vyama vya siasa iliyokuwa imezuiwa.

“Tutaendelea kujenga maridhiano ya kisiasa ili kuweka mazingira mazuri ya Katiba mpya,” alisema Rais Samia na baadaye mwaka 2022 alitangaza mpango wa kuanza kutoa elimu kwa umma kuhusu Katiba mpya na kuandaa mazingira ya kuhuisha mchakato huo.

Hatua hizo zilitia moyo, hata kwenye bajeti ya mwaka 2023/2024, SerikalI ilitenga Sh9 bilioni kwa ajili ya mchakato wa Katiba mpya, ingawa hadi kufikia mwisho wa mwaka huo, hakukuwa na tangazo rasmi kuhusu utekelezaji.

Akizungumza wakati wa hotuba yake ya kuvunja Bunge jijini Dodoma Juni 2025, Rais Samia alitangaza mchakato wa kuandika Katiba mpya ungeanza mwaka 2026.

Aidha, ilani ya uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi (CCM) ya 2025 iliweka misingi ya mchakato huo na katika mikutano ya kampeni wakati wake kama mgombea urais, Rais Samia aliahidi kuhuisha mchakato ndani ya siku 100 za utawala wake.

Mbali na msimamo binafsi wa Rais Samia, CCM imewahi kutoa msimamo wake mara kadhaa kupitia vikao vyake ikionesha nia kusimamia mchakato huo.

Katika kampeni za Uchaguzi Mkuu wa 2025, hoja ya Katiba mpya ilirejea kwa nguvu kwa wagombea wa urais wa vyama vyote, huku Rais Samia akiahidi kuanzisha mchakato huo ndani ya siku 100 za mwanzo.

Hata hivyo, siku 100 zimetimia huku Serikali ikiingiza jipta la kusubirisha mchakato huo hadi yafanyike ‘maridhiano ya kisiasa’ kufuatia machafuko ya kisiasa yaliyoibuka wakati na baada ya uchaguzi.

Kusubiri maridhiano kumekuwa msingi wa kusogezwa mbele utekelezaji wa mchakato wa Katiba mpya na bila shaka itakuwa ndiyo sababu ya kurefusha zaidi upatikanaji wake, licha ya msisitizo wa baadhi ya vyama vya siasa kuwa mchakato huo haupaswi kufungwa na masharti ya kisiasa yanayoweza kuchelewesha haki ya wananchi.

Hata hivyo, Rais Samia ameendelea kusisitiza mchakato huo unahitaji utulivu na makubaliano, akionya haupaswi kuhodhiwa na wanasiasa wala kuleta mgawanyiko, akitaka usubiri maridhiano ya kisiasa.

Msimamo wa wadau, Serikali

Wakati mchakato wa Katiba mpya ukikwama, katika mhojiano na vyombo vya habari kwa nyakati tofauti, aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko, Jaji Joseph Warioba, amekuwa akizungumzia kukwama kwa mchakato huo, akisema changamoto zake si ukosefu wa maoni ya wananchi, bali kukosekana nia thabiti ya kisiasa katika kuumalizia.

Mara kadhaa ameeleza rasimu iliyowasilishwa kwenye Bunge Maalumu la Katiba mwaka 2013 ndiyo msingi mzuri.

Kwa mtazamo wake, mchakato wa kupata Katiba mpya unaweza kukamilika ndani ya muda mfupi endapo kutakuwa na nia ya kweli ya kisiasa kwa kutumia rasimu hiyo.

Vyama vya upinzani na vikundi vya wanaharakati kwa upande wake, vimeendelea kuibeba ajenda ya mabadiliko ya Katiba kwa uzito wake, vikionyesha umuhimu na udharura wa mchakato huo kwenye kampeni, mikutano na hata mahakamani.

Mchakato huo wa zaidi ya miongo mitatu, umeshuhudia kuundwa kwa Tume na vikosi kazi vya kitaifa vilivyotumia rasilimali za umma, bila kuzaa matunda.

Mwaka 1991, Rais Ali Hassan Mwinyi aliunda Tume ya Jaji Francis Nyalali kuchunguza mustakabali wa mfumo wa chama kimoja, iliyozunguka nchi nzima kukusanya maoni, ikigharimu fedha za umma. Licha ya Tume hiyo kuibua umuhimu wa Katiba mpya, suala hilo halikutekelezwa.

Baadaye mwaka 1998, Rais Benjamin Mkapa aliunda Tume ya Jaji Robert Kisanga ya Kuratibu Maoni ya Wananchi “White Paper” juu ya maeneo mbalimbali ya kisiasa na kiuchumi ambayo pamoja na mambo mengine, ilipendekeza maeneo yanayohusu mabadiliko ya Katiba, lakini hayakufanyiwa kazi.

Bunge Maalumu la Katiba lililokaa baada ya Tume ya Jaji Joseph Warioba kukusanya maoni nchi nzima na kuandika rasimu ya katiba mpya mwaka 2013,  mchakato uliotafuna takribani Sh40 bilioni bila kuhitimisha suala hilo.

Hivi karibuni, mwaka 2022, Rais Samia aliunda Kikosi Kazi cha Mageuzi ya Kisiasa nchini ambacho kilikutana na wadau nchi nzima kikitumia fedha za umma, hata hivyo mapendekezo yake, mengi yakihusu Katiba mpya, hayajazaa matunda.

Kwa sasa, macho na masikio ni kwa Tume ya Jaji Chande Othman, inayochunguza matukio ya wakati na baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka jana, ndiyo inayosubiriwa kuwa huenda ripoti yake itawezesha kutoa mwanga wa maridhiano na hatimaye kutoa njia ‘fupi’ itakayowezesha kupatikana Katiba mpya.

Suluhu ya suala hilo inapendekezwa na Sabatho Nyamsenda, mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), kuwa mwafaka wa kitaifa ni njia pekee inayoweza kuukwamua mchakato huo.

“Katiba ni zao la mwafaka wa kitaifa kwa wananchi na watawala, kwa namna ilivyo kwa nchi yetu tangu uhuru mpaka sasa mchakato umekuwa ukihodhiwa na wanasiasa, hasa chama kinachotawala. Mfano hata rasimu ya 2014 iliweka kando maoni ya wananchi, kwani haifanani maeneo mengi na rasimu ya Warioba,” amesema.

Ameeleza kuwa Katiba ya sasa ya 1977 iliundwa wakati wa chama kimoja, wale inaowanufaisha wameendelea kuikumbatia na hivyo kuendeleza mkwamo kwa Taifa kupata Katiba wanayoitaka wananchi.

“Ili kutoka hapa tunapaswa kuiga kwa waliotutangulia kwa kuwa sisi siyo wa kwanza kutaka mabadiliko ya Katiba. Zipo namna mbili; tunapaswa kuanza mchakato mpya shirikishi zaidi au kuendelea tulipoishia kwa kukubaliana tuanzie hatua gani,” amefafanua mwanazuoni huyo.

Anasema maridhiano hayamalizi tofauti, bali maafikiano ndiyo njia ya kumaliza migogoro ya kitaifa.

Lawama kwa wanasiasa pia zinaibuliwa na Wakili Alloyce Komba, akisema Tume zimekuwa zinafanya kazi nzuri lakini wanasiasa, hasa wanaotawala, ndio wamekuwa wakiacha mapendekezo ya tume wanazoziteua.

Akitolea mfano mjadala wa muundo wa Muungano kuwa wataalamu wa Katiba wamekuwa wakiibua madai ya jamii ya kuwa na Serikali tatu, akibainisha kuwa hapo ndipo wanasiasa wamekuwa wakikwamisha Katiba.

“Tume zote zilizoundwa zimewekwa kisheria na zimefanya kazi nzuri nzuri sana, shida ni wanasiasa tu wanakosa utashi. Leo tunaongozwa na Rais aliyekuwa kiongozi mkubwa kwenye Bunge Maalumu la Katiba, lakini mchakato bado unasuasua. Hapa tatizo siyo Tume,” amesema.

Anasema Tume na vkosi kazi hivi hutumia pesa nyingi na kuwasilisha ripoti zao nzuri sana, hivyo wanasiasa na viongozi wanatakiwa kuweka utashi wa kisiasa kukwamua mchakato huo badala ya kuuhodhi na kuuteka wenyewe.

Mwenyekiti wa Baraza la Vyama vya Siasa nchini, Juma Khatibu amekana vyama vya siasa kuhusika moja kwa moja kupoka mchakato wa Katiba mpya.

Hata hivyo, anasema Tanzania ni nchi ya kidemokrasia, hivyo watu wanaounga mkono au kupinga ushiriki wa vyama vya siasa kwenye mchakato wa Katiba wanatumia haki yao.

“Sisi kwenye vyama vya siasa sioni kama kuna tatizo hilo, naheshimu maoni ya hao wanaosema hivyo lakini nampongeza Rais Samia kwani kwenye ilani yake ya CCM aliahidi kuanzisha mchakato wa Katiba mpya ndani ya siku 100. Kuhusu vyama vya siasa kuhodhi mchakato, hii si kweli kwani si wanasiasa pekee wanaoshiriki kwenye mchakato, bali makundi mbalimbali ya jamii,” amesema.

Amesema kwenye Bunge maalumu la Katiba la mwaka 2013 si wanasiasa pekee walioshiriki, Rais Kikwete aliteua wawakilishi kutoka makundi mbalimbali wakiwemo wavuvi, wataalamu na wanasiasa wachache, ingawa anakiri kuwa katika mchakato huo mvutano wa kisiasa uliibuka na baadhi ya vyama vilijitoa bungeni vikaunda Ukawa.

“Mimi ninaamini yasingetokea yale yaliyotokea Oktoba 29, 2025 mchakato huo ungekuwa umeshaanza. Shida ni vurugu hizo na nimpongeze Rais Samia kuunda Tume ambayo vyama vya siasa tumeshiriki vyema kutoa maoni yetu ambayo tunaamini yatasaidia kututoa kwenye mkwamo huo.

“Mimi nawasihi viongozi wangu wa vyama vya siasa ili tutoke hapa lazima waheshimu mamlaka ili utulivu uwepo viongozi wetu waweze kutekeleza mahitaji haya, wasipoheshimu mamlaka wanasababisha mambo yasifanyike na michakato ikwame, wajue kuwa mamlaka haielekezwi bali inashauriwa,” amesema.