Vyakula vya kuepuka wakati wa kufungua

Mwanza. Kufungua swaumu ni hatua muhimu baada ya saa nyingi za kujinyima chakula na kinywaji.

Ni wakati ambao mwili unahitaji kurejeshewa nguvu, maji na virutubisho vilivyopungua kwa muda wa mchana.

Hata hivyo, wataalamu wa lishe wanaonya kuwa si kila chakula kinafaa kuliwa mara tu baada ya kufuturu, kwani baadhi vinaweza kusababisha uchovu, kujaa kwa tumbo au hata kudhoofisha afya.

Baada ya muda mrefu bila kula, mfumo wa mmeng’enyo huwa katika hali ya utulivu na hufanya kazi polepole. Kuingiza vyakula vizito ghafla kunaweza kuushtua mwili na kuleta usumbufu.

Miongoni mwa vyakula vinavyoshauriwa kuepukwa wakati wa kufungua ni vile vyenye mafuta mengi. Vyakula vya kukaanga kama sambusa, bhajia, vitumbua na chipsi, kwani  huongeza mzigo kwa tumbo na kusababisha kichefuchefu, uchovu na tumbo kujaa haraka.

Mbali na hilo, mafuta mengi huongeza  hatari ya magonjwa ya moyo na mishipa.

Utafiti uliochapishwa katika jarida la American Journal of Clinical Nutrition mwaka 2018, ulioshirikisha washiriki 120 wenye umri kati ya miaka 18 hadi 45, ulionyesha kuwa kula vyakula vyenye mafuta mengi mara moja baada ya kufunga kuliongeza kiwango cha ‘triglycerides’ kwa asilimia 25 na kupunguza kasi ya mmeng’enyo kwa asilimia 30, hali iliyosababisha washiriki wengi kuripoti uchovu na tumbo kujaa.

Vinywaji na vyakula vyenye sukari nyingi pia ni hatari kwa mfungaji. Soda, juisi zenye sukari iliyoongezwa, keki na donati huongeza sukari mwilini kwa kasi kubwa.

Ongezeko hilo la ghafla la glukozi hutoa nishati ya muda mfupi, lakini baada ya saa chache sukari hushuka kwa kasi, na kusababisha uchovu na njaa ya haraka.

Kwa mujibu wa utafiti uliochapishwa mwaka 2020 katika jarida la Diabetes Care, kuingiza sukari nyingi mara moja kuliongeza kiwango cha glukozi kwa asilimia 30 hadi 40 ndani ya dakika 30, kisha kushuka kwa takribani asilimia 20 baada ya saa mbili hadi tatu. Wataalamu wanasema mabadiliko hayo ya ghafla yanaweza kuathiri utulivu wa mwili na kuongeza hamu ya kula kupita kiasi.

Chumvi nyingi nayo ni tatizo jingine linaloweza kujitokeza wakati wa futuru. Vyakula vyenye chumvi kupita kiasi huongeza shinikizo la damu na kupunguza usawa wa maji mwilini, jambo linaloweza kusababisha kiu kali hata baada ya kunywa maji. Wataalamu wa afya wanashauri matumizi ya chumvi yasizidi gramu tano kwa siku.

Utafiti uliofanywa Japan mwaka 2017 kwa washiriki 150 ulibaini kuwa matumizi ya zaidi ya gramu sita za chumvi kwa siku yaliongeza shinikizo la damu kwa wastani wa milimita 8 za zebaki (8 mmHg) na kuathiri uwiano wa maji mwilini.

Aidha, vyakula vinavyosababisha gesi kama maharagwe mengi, kabichi au vyakula vyenye nyuzi nyingi kupita kiasi vinapoliwa mara moja baada ya kufunga vinaweza kusababisha tumbo kujaa, gesi na usumbufu.

Utafiti wa mwaka 2019 uliochapishwa katika jarida la Nutrition Reviews ulionyesha kuwa washiriki waliokula vyakula vyenye nyuzi nyingi kwa wingi mara moja waliripoti ongezeko la gesi kwa asilimia 45.

Kwa mujibu wa mtaalamu wa lishe, Asina Abas, njia bora ya kufuturu ni kuanza na maji na matunda mepesi kama papai au tikiti maji ili kurudisha maji na sukari asilia mwilini.

Katika mwongozo wake wa “Eating Healthy During Ramadhan,” Asina anashauri kula kidogo na taratibu, kujumuisha mboga na matunda yenye nyuzinyuzi, vitamini na madini, na kupunguza vyakula vizito vyenye mafuta, sukari na chumvi nyingi.

“Punguza vyakula vizito na vyenye mafuta; vyenye kalori nyingi na vinavyoweza kusababisha kuongezeka kwa uzito,” anasisitiza.

Kwa ujumla, wataalamu wanakubaliana kuwa futari bora ni ile inayorejesha nguvu bila kuushtua mwili. Kuchagua vyakula sahihi si tu kunasaidia mfungaji kujisikia vizuri usiku mzima, bali pia hulinda afya kwa muda mrefu.