Dar es Salaam. Wakati sekta ya uvuvi ikiendelea kubeba matumaini ya ajira, lishe na mapato ya fedha za kigeni, Serikali imefungua ukurasa mpya kwa kuanza mchakato wa kuandaa ramani ya muda mrefu ya uwekezaji na mageuzi ya mifumo ya vyakula vya majini nchini.
Hatua hiyo inatajwa kuwa mabadiliko ya kimkakati yatakayohamisha msukumo kutoka utekelezaji wa miradi ya muda mfupi kwenda mfumo jumuishi, endelevu na unaovutia uwekezaji wenye matokeo yanayopimika.
Mchakato huo umeanza kupitia Warsha ya Kitaifa ya GEDSI kuhusu Uundaji wa Nadharia ya Mabadiliko kwa Mageuzi ya Mifumo ya Vyakula vya Majini Tanzania, iliyowakutanisha watafiti, watunga sera na washirika wa maendeleo jijini Dar es Salaam.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa warsha hiyo, Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi (TAFIRI), Dk Ismail Kimirei, aliyemwakilisha Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Agnes Meena, amesema uchumi wa buluu ni miongoni mwa maeneo yenye fursa kubwa kwa ukuaji wa Taifa.
“Kwa kuungwa mkono na rasilimali kubwa za bahari, ukanda wa pwani na maji ya ndani, sekta ya uvuvi na ufugaji wa samaki ina mchango mkubwa katika usalama wa chakula, lishe, ajira na mapato ya fedha za kigeni,” amesema Dk Kimirei.
Ameeleza kuwa uvuvi wa kiwango kidogo unaendelea kuwanufaisha mamilioni ya Watanzania moja kwa moja na kwa njia isiyo ya moja kwa moja, huku ufugaji wa samaki ukiibuka kama eneo muhimu la ajira kwa vijana na kuongeza upatikanaji wa samaki katika soko la ndani.
Kwa mujibu wa Dk Kimirei, sekta pana inayojumuisha kilimo, mifugo na misitu inachangia takribani asilimia 26.4 ya Pato la Taifa na karibu asilimia 30 ya mapato ya mauzo ya nje, huku ikiwezesha maisha ya takribani asilimia 65 ya Watanzania.
Ndani ya mfumo huo, vyakula vya majini ni nguzo muhimu ya uchumi wa vijijini na maeneo ya pwani.
Hata hivyo, amesema sekta hiyo bado inakabiliwa na changamoto kadhaa za kimuundo, zikiwamo uvuvi kupita kiasi katika baadhi ya maeneo, uzalishaji mdogo, upatikanaji mdogo wa mitaji na teknolojia za kisasa, pamoja na kuingia kwa shida katika masoko yenye thamani kubwa.
Ameongeza kuwa mabadiliko ya tabianchi yanaongeza shinikizo kwa mifumo ya ikolojia na jamii za wavuvi, jambo linalohitaji mikakati thabiti na jumuishi.
Akizungumzia usawa, Dk Kimirei amesema baadhi ya vikwazo vinahusiana moja kwa moja na upatikanaji wa fursa kwa makundi maalumu.
“Wanawake wamejikita zaidi katika shughuli za baada ya mavuno na biashara ndogondogo zenye faida ndogo ndani ya mnyororo wa thamani. Vijana wanakumbana na changamoto za mitaji, ujuzi na umiliki wa rasilimali, huku watu wenye ulemavu na jamii za pembezoni wakibaki nje ya michakato rasmi ya maamuzi na uwekezaji,” amesema.
Warsha hiyo imeweka ajenda ya usawa wa kijinsia, ujumuishaji wa watu wenye ulemavu na makundi maalumu (GEDSI) kuwa kiini cha mageuzi ya sekta, badala ya kuyaona masuala hayo kama nyongeza ya pembeni.
Kwa upande wake, Mkuu wa Ndaki ya Kilimo na Sayansi ya Chakula ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Mkabwa Manoko, amesema Nadharia ya Mabadiliko itakayoundwa itaweka wazi matokeo yanayotarajiwa katika maeneo ya ushiriki, mamlaka ya maamuzi, upatikanaji wa rasilimali na mgawanyo sawa wa faida.
“Lengo ni kuhakikisha ongezeko la uzalishaji linatafsiriwa kuwa ukuaji jumuishi unaowagusa wote,” amesema.
Amebainisha kuwa kupitia mradi wa Asia–Africa Blue Tech Superhighway, unaofadhiliwa na Mfuko wa Blue Planet wa Uingereza na kutekelezwa na WorldFish kwa kushirikiana na wadau wengine, mambo kadhaa yamefanyika.
Ameyataja mambo hayo ni pamoja na majaribio ya mifumo ya kisasa ya takwimu za uvuvi, zana za maamuzi zinazotumia taarifa za tabianchi na teknolojia janja za uvuvi.
Mwakilishi wa Maendeleo ya Kimataifa kutoka Uingereza, Glory Mramba, amesema nchi hiyo itaendelea kuunga mkono juhudi za Tanzania katika kuboresha mifumo ya vyakula vya majini, akisisitiza umuhimu wa kuwa na Nadharia ya Mabadiliko inayomilikiwa kitaifa ili kuoanisha sera, ushirikiano na mitaji.
Amesema ni muhimu kubainisha wazi majukumu ya Serikali, watafiti, jamii, sekta binafsi na asasi za kiraia ili kuhakikisha uwajibikaji na matokeo yanayopimika.