Wajasiriamali 3,000 Mtumba kunufaika | Mwananchi

Dar es Salaam. Zaidi ya wajasiriamali 3,000 wa Jimbo la Mtumba wanatarajiwa kunufaika na mpango wa mikopo wenye thamani ya Sh2 bilioni.

Mpango huo, unatekelezwa kwa ushirikiano kati ya Ofisi ya Mbunge wa Jimbo hilo, Anthony Mavunde na CRDB Bank Foundation, kupitia programu ya Imbeju.

Uzinduzi wa programu hiyo umefanyika jijini Dodoma leo Jumatano, Februari 18, 2026, ukilenga kuwawezesha wananchi kiuchumi na kukuza shughuli za uzalishaji katika jimbo hilo.

Mbunge wa Jimbo la Mtumba, Anthony Mavunde. 



Akizungumza katika uzinduzi huo, Mkurugenzi Mtendaji wa CRDB Bank Foundation, Tully Mwambapa, amesema taasisi hiyo imejipanga kuwafikia wajasiriamali wengi zaidi nchini kwa kuwapatia mitaji na mikopo nafuu itakayowawezesha kukuza biashara zao.

Ameeleza Jimbo la Mtumba limechaguliwa kuwa miongoni mwa majimbo ya mfano katika utekelezaji wa mpango huo na vikundi vya wajasiriamali zaidi ya 3,000 vitanufaika na mikopo hiyo yenye thamani ya takribani Sh2 bilioni.

Kwa upande wake, Mavunde ambaye pia ni Waziri wa Madini, amesema mpango huo ni sehemu ya kuunga mkono jitihada za Serikali za kuwawezesha wananchi kiuchumi kupitia mikakati mbalimbali ikiwemo utoaji wa Sh200 bilioni kuchochea biashara.


Amesisitiza uwekezaji katika mitaji ya wajasiriamali ni njia madhubuti ya kupunguza umaskini na kuongeza ajira katika jamii.

Amewahimiza wananchi wa Mtumba kuchangamkia fursa zinazojitokeza, akibainisha kuwa jimbo hilo linatarajiwa kunufaika na mradi mkubwa wa kilimo cha umwagiliaji utakaotekelezwa kwa kushirikiana na mashirika makubwa ya kilimo kutoka Bara la Afrika.

Amesema mradi huo utafungua milango ya ajira, kuongeza uzalishaji wa mazao na kuinua kipato cha wakazi wa eneo hilo.