Wawakilishi waitaka SMZ kusimamia miradi ya kimkakati kikamilifu

Unguja. Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi wameitaka Serikali kuweka mkazo na kusimamia kikamilifu miradi ya kimkakati badala ya kueleza mipango yake kwenye makaratasi pekee ili kupata matokeo chanya.

Wameeleza hayo leo Februari 18, 2026 wakati wakichangia Mpango wa Taifa na mwelekeo wa bajeti mwaka 2026/27 katika mkutano wa 11 wa Baraza la Wawakilishi, Chukwani Unguja Zanzibar.

Mwakilishi wa Mfenesini, Machano Othman Said (CCM) amesema licha ya mipango mizuri katika bajeti hiyo lakini iwapo hakutakuwa na usimamizi mizuri katika miradi hiyo itakuwa kazi kubwa kufikia malengo hayo.

Machano ametolea mfano wa kuimarisha bandari ambayo amesema bado kuna changamoto kubwa, hivyo inatakiwa kuhakikisha zinaimarishwa ili kuondoa matatizo ya usafirishaji mizigo kutoka nje ya nchi.

“Huu mpango ni mzuri lakini Serikali ihakikishe inasimamia miradi hii ya kimkakati, hizi barabara ziendelee kusimamiwa kujengwa vinginevyo tunaweza kukwama,” amesema.

 “Katika mpango huu Serikali lazima kuwepo msukumo mkubwa wa upatikanaji wa umeme kwa sasa Zanzibar hatuna uhakika wa umeme unakatika ovyo, maeneo mengine haupo, kwa hiyo bila ya kuwa na umeme wa uhakika hatuwezi kufanikiwa katika mpango huu na shughuli zingine zinaweza kushindwa kuendelea,” amesema Machano.

Mwakilishi nafasi za uteuzi wa Rais, Toufiq Salim Turky akizungumza wakati wa mjadala wa mpango wa taifa na mwelekeo wa bajeti mwaka 2026/27 katika mkutano wa 11 wa Baraza la Wawakilishi Chukwani Unguja Zanzibar



Katika mchango wake mwakilishi wa Mwanakwerekwe, Mohamed Manzi Haji (CCM) amesema Serikali iendelee kuweka mkazo zaidi katika sekta ya kilimo uvuvi na uchumi wa buluu, kwani vina mchango mkubwa katika uchumi wa nchi.

“Katika upande wa kilimo lazima tuzingatie miundombinu ya umwagiliaji tutaongeza thamani ya mazao jambo ambalo litaongeza ajira na uzalishaji wa kisekta,” amesema.

Amesema katika mwelekeo huo inaonekana katika mwaka unaokwenda kuisha imefanya vizuri katika makusanyo na kuweka bajeti kubwa katika maendeleo.

Pia, amesema wanatakiwa kuweka mifumo mizuri kuwatambua wageni wanaoingia na kutoka Zanzibar ili wapate taarifa sahihi za wageni maana kwa sasa inaonekana hawana taarifa hizo.

“Ipo haja kuendelea kutangaza zaidi utalii nje ili kufanya vizuri zaidi katika sekta hiyo,” amesema.

Naye mwakilishi viti vya wanawake, Dk Nasra Nassor Omar (ACT Wazalendo) amesema licha ya kuelezwa kwamba deni la Taifa ni himilivu lakini ipo haja kuangalia ikiwa mwananchi wa kawaida anawezaje kuhimili.

“Tunasema deni la Taifa ni himilivu lakini tujiulize kwama mwananchi wa kawaida linamsaidiaje, maana bado anaona gharama za vitu vipo juu na huku anawekewa mzigo mkubwa wa kulipa deni hilo,” amesema Dk Nasra.

Ameshauri pia kuangalia upya mfuko wa huduma za afya licha ya kulenga watu wote lakini  hauna wanachama kwani waliopo mpaka sasa ni asilimia 50 pekee.

Mwakilishi wa Magomeni, Mahfoudh Abdalla Mohamed (CCM) amesema mpango huo ni mzuri lakini inatakiwa uwe shirikishi kila anayestahili kwani haiwezi kufikia malengo yake bila kushirikiana.

Pia, amesema mipango hiyo iendane na ulinzi na kusimamia utawala bora ikiwa ni pamoja na kuhakikisha masilahi ya watumishi yanazingatiwa ili kutoa motisha ya kazi.

Mahfoudh amesema inaonesha uchumi umekuwa lakini bado umeme unaendelea kuwa changamoto, hivyo kuna hatari ya kurejesha nyuma kasi ya ukuaji wake.

“Hapa tutawalalamikia watendaji wa Zeco (Shirika la Umeme) lakini shida hii ya umeme sio ya kwao, kama Taifa tunatakiwa kuwa na mikakati maalumu kuondoa changamoto hii maana inakwaza uwekezaji katika visiwa vyetu,” amesema.

Naye, Toufiq Salim Turky (mteule wa Rais), amesema kwa sasa angalau fedha zinazokusanywa kwa wananchi zinafanya miradi mikubwa ya maendeleo na inaonekana wazi, tofauti na ilivyokuwa zamani fedha zinakusanywa lakini hazionekani kinachofanyika.