Zimamoto Maswa yakabidhiwa gari lenye uwezo wa kuzima moto ghorofa ya 10

Maswa. Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Wilaya ya Maswa mkoani Simiyu, limepewa mtambo wa kuzima moto wenye uwezo wa kufika kwenye jengo lenye urefu wa ghorofa 10 ikiwa ni sehemu ya mkakati wa Serikali kukabidhi mitambo hiyo kwa ajili ya shughuli za jeshi hilo katika wilaya zote nchini.

Akikabidhi gari hilo leo Februari 18, 2026 mjini Maswa, Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Anamringi Macha amesema hizo ni juhudi za  Serikali katika kulipatia jeshi hilo vitendea kazi ili liweze kutekeleza majukumu ya kila siku.

Mkuu wa mkoa wa Simiyu,Anamringi Macha akizungumza wakati wa hafla ya kukabidhi gari la Zimamoto na Uokoaji katika Wilaya ya Maswa. Picha na Samwel Mwanga



Amesema kuwa mojawapo ya malalamiko ya wananchi kuhusu jeshi hilo ni uhaba wa vitendea kazi lakini Serikali imeliona hilo na ndiyo maana imekabidhi mtambo huo mpya.

“Huu ni mfano wa kuigwa, tangu Wilaya ya Maswa kuanzishwa ni miaka 100 ilikuwa haina gari au mtambo wa kuzima moto, Serikali inaendelea kushughulikia changamoto za Jeshi la Zimamoto na Uokoaji kwa kununua mtambo kama huu,” amesema.

Amesema ni vizuri Wakala wa Barabara Mijini na Vijijini (Tarura) wakahakikisha miundombinu ya barabara inakuwa vizuri ili gari hilo lifike mahali popote katika wilaya hiyo pindi litakapohitajika.

Kaimu Mkuu wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Simiyu, Faustine Mtitu amesema ni vizuri kwa Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira Mjini Maswa (Mauwasa) na Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (Ruwasa), kutenga vituo vya kujazia maji ili kuwezesha gari hilo linapoishiwa maji kuyapata umbali wa mita 100 mjini na umbali wa mita 200 vijijini.

Kaimu Mkuu wa jeshi la Zimamoto na Uokoaji mkoa wa Simiyu,Faustine Mtitu akizungumza wakati wa hafla ya kukabidhi gari la Zimamoto na Uokoaji wilaya ya Maswa. Picha na Samwel Mwanga



“Gari hili lenye thamani ya zaidi ya Sh2.3 bilioni ni vizuri wananchi wakalitumia kwa kutoa taarifa majanga yanapotokea nasi tutafika kwa wakati, huu ni mtambo ukiwa na vifaa vya kisasa vya kuthibiti moto na kuokoa maisha ya watu na mali zao,” amesema.

Mkuu wa Wilaya ya Maswa, Dk Vicent Anney amesema wilaya hiyo imekuwa ikikumbwa na majanga ya moto kwa muda mrefu na upatikanaji wa gari hilo ni hatua ya kihistoria.

Mkuu wa wilaya ya Maswa,Dk Vicent Naano akizungumza wakati wa hafla ya kukabidhiwa gari la Zimamoto katika wilaya hiyo. Picha na Samwel Mwanga



Anitha Mboje, mkazi wa Maswa mjini, amesema kuwa wilaya hiyo imepata mkombozi wa majanga ya moto kutokana na kuwepo kwa ajali za nyumba kuungua.