Bwege Ajiuzulu ACT Wazalendo, Aeleza Kujiunga na CHADEMA – Global Publishers


Aliyekuwa Mbunge wa Kilwa Kusini, Selemani Said Ally Bungara, maarufu kama ‘Bwege’

Mwanasiasa machachari na aliyekuwa Mbunge wa Kilwa Kusini, Selemani Said Ally Bungara, maarufu kama ‘Bwege’ ametangaza rasmi kujivua uanachama wa chama cha ACT Wazalendo kuanzia Februari 18, 2026.

Taarifa yake, iliyotolewa kwa umma, imesema kuwa uamuzi huo umetokana na hiyari yake mwenyewe na tafakari ya muda mrefu juu ya mwelekeo wa kisiasa wa chama hicho.

Bwege, anayejulikana kwa msimamo wake thabiti na lugha za mvuto majukwaani, alisema kuwa mwelekeo wa ACT Wazalendo umekuwa tofauti na matarajio yake, jambo lililompelekea kutafuta jukwaa jingine.

“ACT Wazalendo si rafiki sahihi kwangu, nilivyofikiria ni tofauti na nilivyohisi. Kuanzia sasa mimi si mwanachama wa ACT Wazalendo tena kuanzia tarehe 18/2/2026. Mengine nitaongea baadaye,” ameandika Bwege.

Bwege amebainisha kuwa anachotaka sasa ni kushirikiana na CHADEMA katika siasa za kudai demokrasia na maendeleo ya taifa.

“Ninategemea kushirikiana na kulitumia jukwaa la CHADEMA katika siasa za kudai demokrasia na maendeleo la taifa langu nilipendalo-Tanzania.”

Hii ni hatua kubwa kisiasa, kwani Bwege ni mmoja wa wabunge wenye mvuto mkubwa na aliyejulikana kwa msimamo wake wa kishujaa katika Bunge na vyombo vya habari.

Kujiuzulu kwa Bwege kunaleta mabadiliko makubwa kwenye taswira ya siasa za upinzani nchini Tanzania. Changamoto kubwa kwa ACT Wazalendo ni kuhakiki iwapo watapoteza umaarufu na msaada wa wafuasi wa Bwege katika maeneo wanayoshirikiana.

Kwa upande mwingine, CHADEMA inaweza kupata nguvu mpya kisiasa, hasa katika miji na vijiji vya Kusini mwa Tanzania, kutokana na uhamisho huu wa kiasili.