Kamusi ya Kiswahili mtandaoni muhimu utoaji elimu ya fedha

Katika miaka ya karibuni, Tanzania imekuwa ikishuhudia ongezeko kubwa la juhudi za utoaji wa elimu ya fedha. Benki, taasisi za udhibiti, mashirika ya kiraia, wanataaluma, na wadau wengine wanaendesha programu mbalimbali za kuwajengea wananchi uelewa wa masuala ya mikopo, akiba, bima, uwekezaji, pamoja na matumizi ya huduma za kifedha za kidijitali.

Hata hivyo, changamoto kubwa inayojitokeza ni kwamba maarifa haya kwa kiasi kikubwa huandaliwa na kuwasilishwa kwa lugha ya Kiingereza. Hali hii huwafanya wadau wa elimu ya fedha kukabiliwa na ugumu wa kupata istilahi sahihi za Kiswahili ili kuwasilisha dhana hizo kwa wananchi wengi wanaotumia Kiswahili kama lugha kuu ya mawasiliano. Pale ambapo istilahi hazijasanifiwa, kila mtoa elimu anaweza kutumia tafsiri yake binafsi, hali inayoweza kuathiri uelewa na ufikishaji wa maarifa hayo.

Changamoto hapa si kwamba kamusi ya Kiswahili haipo, ila ni urahisi wa kuzipata, kasi ya kuzisasisha, na uwezo wake wa kukidhi mahitaji ya elimu ya fedha katika mazingira ya uchumi na sekta ya fedha yanayobadilika kwa haraka.

Mathalan, mwandishi anapotaka kujua neno interest rate atalitafsiri vipi kwa Kiswahili, au mtoa elimu ya fedha anapoandaa somo kuhusu saving schemes, je, kwa haraka ndani ya muda mfupi anawezaje kupata msamiati sahihi wa kutumia?. Hapa ndipo hoja yangu kuwa na kamusi ya Kiswahili iwekwe kwenye tovuti yake maalumu inaweza kufikiwa kimtandao.

Kwanza, uwepo wa kamusi hiyo utasaidia matumizi ya istilahi sahihi katika kufikisha elimu ya fedha kwa Kiswahili. Bila kamusi sanifu na inayopatikana kirahisi, neno moja la kifedha linaweza kupewa maana tofauti. Mwandishi wa gazeti anaweza kulitaja interest rate kama “riba”, mwalimu wa elimu ya fedha akasema ni “gharama ya mkopo”, mwingine akaitaja kama “faida”.

Hali hii inaweza kuwachanganya wale wanaojifunza dhana hizi kwa mara ya kwanza. Elimu ya fedha inapokosa lugha iliyo wazi na thabiti, badala ya kumsaidia mlaji, inaweza kumwacha akiwa na mkanganyiko.

Kamusi ya Kiswahili kimtandao ingeondoa hali hii. Ndani ya dakika chache, kupitia tovuti rasmi, mtumiaji angeweza kupata msamiati sahihi na maelezo yanayolingana na dhana ya kifedha anayotaka kufafanua.

Endapo wadau wote wa elimu ya fedha wangetumia rejea hiyohiyo, ingejenga ufikishaji wa elimu ya fedha wenye mfanano na uendelevu wa istilahi (standard vocabulary usage).

Pili, kamusi ya kimtandao ingerahisisha usanifishaji wa maneno mapya. Uchumi wa sasa huzalisha dhana mpya kila wakati: mikopo ya kidijitali, uwekezaji masoko ya fedha, mifumo mipya ya malipo, na mengineyo. Kamusi iliyochapwa huchukua muda mrefu kuingiza maneno mapya hadi itakapotolewa toleo jingine. Kamusi ya kimtandao, kwa upande mwingine, inaweza kusasishwa mara moja neno jipya linapoidhinishwa. Una “search” unapata neno la Kiswahili ndani ya sekunde.

Tatu, uwepo wa kamusi hiyo ungepunguza changamoto kwa watoa elimu ya fedha wenyewe. Waandishi wa makala, watayarishaji wa vipindi, walimu, na taasisi zinazotoa elimu ya fedha hulazimika mara kwa mara kubuni tafsiri zao binafsi. Hii hupoteza muda na husababisha elimu kutolewa bila mwelekeo mmoja.

Nne, hoja hii inaendana na muktadha wa zama za teknolojia na mawasiliano ya haraka. Leo, elimu ya fedha inasambazwa kupitia mitandao ya kijamii, tovuti, na simu za mkononi. Ni mantiki basi kwamba nyenzo ya lugha inayotumika pia iwe ya kidijitali. Kamusi ya Kiswahili kimtandao ingeendana na mazingira haya mapya na kasi ya mahitaji ya sasa.

Kwa ujumla, wazo la kamusi ya Kiswahili kimtandao halilengi kusaidia elimu ya fedha pekee, bali utoaji wa maarifa na habari kwa ujumla.

Hata hivyo, katika muktadha wa juhudi za sasa za kuongeza uelewa wa elimu ya fedha na kuwafikia wananchi wengi zaidi, upatikanaji wa misamiati sahihi, usanifishaji wa istilahi mpya, na urahisi wa rejea ni jambo la msingi.

Haya yote yatawezekana kwa ufanisi zaidi endapo kamusi ya Kiswahili itapatikana kwa njia nyepesi, iwepo tovuti maalumu ya kamusi ya Kiswahili cha Tanzania iliyounganishwa na akili unde kurahisisha upatikanaji wa istilahi sahihi katika utoaji wa elimu fedha.