Kiungo wa zamani Simba awataja wawili Yanga

UKISIKIA ngoma droo ndio hii. Wakati Simba na Yanga zote zikiwa na kilio kimoja cha kutolewa katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu, lakini Waarabu wa JS Kyblie wameondoka na majina ya washambuliaji wa Jangwani.

Akizungumza na Mwanaspoti, kiungo wa zamani wa Simba, Babacar Sarr anayecheza JS Kabylie, amesema kuna wachezaji wawili ambao walifanikiwa kuvuruga hesabu zao kwenye mchezo wa mwisho.

Sarr amesema kuwa licha ya Yanga kutofuzu, lakini amemuona Laurindo Dilson ‘Depu’ ni mshambuliaji hatari ambaye kama Simba isipojipanga Machi Mosi mwaka huu, atawaliza.

Sarr amesema mshambuliaji huyo analijua goli na si rahisi sana kumkabili endapo mabeki hawatokuwa na hesabu nzuri za kumzuia.

“Yule mchezaji namba 40 (Depu) ni mpya lakini ni hatari sana, anajua kufunga, lile goli la pili alilotufunga hawezi kufunga kila mchezaji, ni hesabu kubwa sana, si sisi tu hata wachezaji wa timu yake niliona wameshtuka.

“Yule mpaka tunaondoka pale uwanjani kila mchezaji anamzungumzia juu ya kile ambacho amekionyesha, kweli kabisa hakuna timu haitamani kuwa na mtu hatari vile hasa eneo la muhimu kama mbele,” amesema Sarr.

Kiungo huyo ambaye aliwahi kuichezea Simba miezi sita msimu uliopita akitua dirisha dogo, amesema kwenye mchezo wa Dabi ya Kariakoo, Wekundu wana kazi ya kufanya kumzuia mshambuliaji huyo.

“Timu yangu ya zamani (Simba) wanatakiwa kujipanga sana kumzuia, vinginevyo kama mabeki hawatampa ulinzi mkubwa ataweza kuwasababishia matatizo.

“Lakini kama wataweza kumzuia vyema anaweza asiwe na madhara makubwa ijapokuwa haitakuwa kazi rahisi kabisa,” amesema.

Sarr amesema hatua ya Depu kucheza na Prince Dube ndiyo mambo yanaweza kuwa magumu zaidi kutokana na kasi za washambuliaji hao.

“Ukiangalia kwenye mechi yetu walianza pamoja Dube na huyu mshambuliaji mpya (Depu), mabeki wetu walipata tabu sana, unajua Dube ana kasi sana na anaweza kushambulia kutokea upande wowote.

“Namna Dube anavyozunguka anatengeneza presha kwa mabeki kuanza kumfikiria yeye na kumuacha Depu, mkifanya kosa hilo ndiyo unajikuta unapoteza,” amesema.

Rekodi za mastaa hao kwenye michuano ya Ligi Kuu Bara zinaonyesha kwamba Dube amefunga mabao matatu, huku Depu akiwa nayo matatu.

Amesema safu ya kiungo ya Yanga ina ubora mkubwa, lakini baada ya kuumia Pacome Zouzoua iliwapunguzia presha. “Yanga wana viungo wazuri sana pia. Kitu kibaya zaidi wana kasi sana, ukiangalia mchezo wetu tulipata bahati baada ya kuumia Pacome, lakini kama angeendelea ingekuwa si rahisi.”

Yanga itakuwa mwenyeji wa Simba kwenye mchezo wa duru la kwanza katika Ligi Kuu Bara msimu huu, utakaopigwa Jumapili ya Machi Mosi 2026 kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar ambao itakuwa Kariakoo Dabi ya kwanza kwenye ligi kupigwa kisiwani humo.