Wakati Tanzania ikitangaza rasmi kuanza kuzisajili na kuzitambua kampuni changa za Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama) maarufu kama startups, hatua hiyo imetajwa kuwa miongoni mwa mikakati muhimu ya kuchochea ukuaji wa uchumi wa kidijitali.
Wadau wa sekta hiyo wanasema ni hatua ya msingi inayofungua ukurasa mpya wa kuimarisha mfumo wa ubunifu nchini, huku wakielekeza maeneo muhimu yanayopaswa kupewa kipaumbele ili manufaa yake yaonekane kwa haraka na kwa upana.
Hivi karibuni, Serikali kupitia Tume ya Tehama (ICTC) ilitangaza kuanza rasmi usajili na utambuzi maalumu (labelling) kwa kampuni changa za Tehama.
Hatua hiyo inaashiria mabadiliko ya kimkakati kutoka mfumo wa usajili wa kawaida wa kampuni hadi utambuzi rasmi unaolenga pia kutoa msaada wa kitaalamu kulingana na mahitaji na hatua ya ukuaji wa kila kampuni.
Mkurugenzi Mkuu wa ICTC, Dk Nkundwe Mwasaga, amesema mfumo huo mpya unaojulikana kama ICT Startup Labelling unalenga kujenga mazingira yatakayorahisisha safari ya kampuni changa kutoka hatua ya wazo hadi kuwa biashara kamili yenye ushindani wa kitaifa na kimataifa.
Kwa mujibu wake, si suala la kutambua majina pekee, bali ni kuweka mfumo wa kitaasisi utakaowezesha ubunifu kukua kwa kasi na kwa tija.
Akizungumza na mwandishi wa makala haya, Mkurugenzi wa Sahara Ventures, Jumanne Mtambalike, anasema kuanza kwa utambuzi huo si ishara ya kuchelewa, bali ni dalili kwamba Tanzania sasa inaingia katika hatua ya kuimarisha na kurasimisha kikamilifu mfumo wa uchumi wa kidijitali.
“Kiukweli, nchi nyingi zilizofanikiwa kwenye ubunifu, ikiwemo Kenya, zilianza kwa kujenga mifumo ya utambuzi na viwango kabla ya kuvutia mtaji mkubwa wa kimataifa,” anasema Mtambalike, ambaye ni miongoni mwa wabunifu wanaotajwa kuwa mfano nchini.
Anaongeza kuwa Tanzania tayari ina idadi inayoongezeka ya startups, vipaji vingi vya vijana na taasisi kama COSTECH, BuniHub na DTBI. Kilichokuwa kinakosekana ni mfumo rasmi wa kutofautisha na kuthibitisha startups zenye ubora na uwezo wa kukua.
“Hatua hii inafunga pengo la kimuundo na kuweka msingi wa ukuaji unaopimika na unaoaminika kimataifa,” anasisitiza.
Hata hivyo, Mtambalike anaonya kuwa athari chanya za kiuchumi zitategemea namna utekelezaji utakavyokwenda sambamba na hatua za ziada za kisera na kifedha. Kwa mtazamo wake, utambuzi utaongeza uaminifu kwa wawekezaji, kurahisisha upatikanaji wa mitaji na kusaidia Serikali kulenga motisha na programu zake kwa startups halisi badala ya kampuni za kawaida zisizo na ubunifu wa kiteknolojia.
“Kwa uzoefu wa kimataifa, mifumo ya aina hii huongeza ajira kwa vijana wenye ujuzi, huchochea ubunifu katika sekta kama fintech, agritech na healthtech, na huimarisha nafasi ya nchi kuvutia uwekezaji wa teknolojia kutoka nje. Kwa Tanzania inayolenga uchumi wa viwanda sambamba na uchumi wa kidijitali, huu ni mkondo sahihi wa sera,” anasema.
Anaongeza kuwa ili kufunga pengo na nchi kama Kenya na kuongeza thamani ya uwekezaji katika kampuni hizi, hatua inayofuata inapaswa kuwa kuunganisha mfumo wa labelling na fursa halisi za soko na mtaji.
Serikali na wadau wanapaswa kuweka mifumo ya ubia wa uwekezaji (co-investment) kati ya sekta ya umma na binafsi, kufungua sehemu ya zabuni za umma kwa startups zilizoidhinishwa, na kuimarisha daraja kati ya tafiti za vyuo vikuu na mahitaji ya soko.
Sambamba na hilo, anasisitiza umuhimu wa kujenga data room ya kitaifa ya startups itakayorahisisha upatikanaji wa taarifa kwa wawekezaji, pamoja na kuandaa mazingira rafiki ya exits ili kuvutia mitaji ya kimataifa ya ubia (venture capital).
“Tukifanya hivi kwa kasi na uratibu mzuri, Tanzania ina nafasi si tu ya kufunga pengo, bali hata kujitofautisha kikanda ndani ya miaka michache ijayo,” anasema.
Ikumbukwe kuwa kupitia mageuzi hayo, ICTC imelenga kuongeza ufanisi na kasi ya kusaidia bunifu na kampuni changa kutoka kuwa mawazo au miradi ya majaribio hadi kuwa bidhaa au huduma za kibiashara zenye ushindani. Maboresho hayo yanatoka katika mfumo wa kusajili tu hadi kutoa alama maalumu ya utambuzi inayothibitisha hadhi na daraja la ukuaji wa kampuni husika.
Mchumi kutoka Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Dk Mwinuka Lutengano, anasema kumekuwa na wimbi la biashara ndogo na za kati zilizoanzishwa na vijana, hususan katika eneo la Tehama. Hata hivyo, si zote zimerasimishwa au kusajiliwa ipasavyo.
Kwa mujibu wake, utambuzi maalumu una maana kubwa katika kuzifanya biashara hizo kuwa rasmi, kuzisaidia kimfumo na hatimaye kufanya mchango wake katika pato la taifa uwe bayana. “Biashara hizi changa zinahitaji kuatamiwa na kujengewa uwezo ili ziwe na tija. Utambuzi ni daraja muhimu la kuwezesha hayo yote na kuleta matokeo tarajiwa,” anasema.
Anasisitiza kuwa mchakato wa utambuzi unapaswa kwenda sambamba na ukusanyaji wa taarifa muhimu kama ukubwa wa kampuni, sekta wanazowekeza, mahitaji yao ya mitaji, miundombinu, mafunzo na teknolojia. Hii itasaidia kupanga sera na rasilimali kwa usahihi zaidi.
Kwa upande wake, mchumi Oscar Mkude anasema utambuzi ni hatua muhimu, lakini msaada wa kweli kwa startups ndio kipimo cha mafanikio.
“Tujiulize, ni kwa kiasi gani startups hizi zimesaidiwa kufikia hapo zilipo? Ni vikwazo gani vya kimfumo na kisera vinazikwamisha? Kwa nini nyingi hazifiki hatua ya ukuaji mkubwa (scalable stage) kama ilivyokuwa kwa Uber, Facebook au Nala?” anahoji.
Anafananishia utambuzi na sherehe ya mahafali ya mtoto. “Muhimu si mahafali, bali ni kuhakikisha mtoto anafikia hapo: kulipa ada, kumsimamia na kumpa msaada wote anaohitaji. Huo ndio msaada unaotoa matokeo. Haina maana kushangilia startup mbili na kusahau zipo 100 zinazotaabika kwa mifumo yetu,” anasema.
Noel Henjewele, Mkuu wa Kitengo cha AI na Cloud kutoka Dynatech Solutions Limited, anasema mwekezaji anayeanza anahitaji mtaji wa kutosha na mazingira yasiyomkatisha tamaa. Anashauri kuwepo kwa unafuu wa baadhi ya kodi ndogondogo zinazoweza kuzuia ukuaji wa awali wa kampuni hizo.
Naye mchumi anayejikita katika uchumi wa kidijitali, Francis Nyonzo, anasema uwezo wa miundombinu ya kidijitali bado ni changamoto ikilinganishwa na nchi jirani. Anasisitiza umuhimu wa kuimarisha miundombinu, mifumo ya kulea startups, na kuhakikisha sheria za kifedha na gharama za uendeshaji hazizuii ubunifu.
“Tuweke fedha za kutosha kuwajengea vijana uwezo, hata kuwapeleka kujifunza katika masoko makubwa kama Marekani. Pia tuwatumie Watanzania waliofanikiwa kama Benjamin Fernandes ili kujifunza kutoka kwao,” anashauri.
Kwa mtazamo wa kitaaluma, Mtafiti wa uchumi wa kidijitali kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Mussa Mkwizu, amesema hatua hiyo inaashiria ukomavu wa kisera.
“Kwa miaka mingi Tanzania imewekeza kwenye miundombinu kama Mkongo wa Taifa na huduma za kidijitali. Sasa tunaona uratibu wa ubunifu kuwa taasisi rasmi. Hivyo ndivyo unavyojenga uchumi endelevu wa kidijitali,” anasema.
Hivi sasa, Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano umesambaa kwa maelfu ya kilomita ukiunganisha mikoa yote na nchi jirani, huku matumizi ya simu yakifikia zaidi ya asilimia 90 ya Watanzania. Mazingira haya yanatoa fursa kubwa kwa startups kupanua huduma zao.
Kwa upande wa wabunifu, mfumo wa utambuzi unatarajiwa kupunguza vikwazo vya muda mrefu, hususan katika upatikanaji wa mitaji. Judith Rwegasira, mwanzilishi mwenza wa agritech startup mkoani Morogoro, anasema wawekezaji mara nyingi huuliza kuhusu uhalali na hadhi ya kisheria ya kampuni.
“Ikiwa Tume itatuthibitishia daraja letu la ukuaji, inapunguza usumbufu wa uchunguzi wa awali na kuongeza imani kwa wawekezaji,” anasema.
Kwa mujibu wa takwimu za ICTC, hadi Desemba 2025, zaidi ya vituo 95 vya ubunifu vilikuwa vimeanzishwa nchini, huku asilimia 76 vikijikita katika suluhisho za Tehama. Aidha, zaidi ya startups 600 zilikuwa zimesajiliwa, ambapo 161 zilikuwa zimekidhi vigezo vya kuingia katika programu za kulelewa na kuendelezwa.
Dk Mwasaga anasema usajili ni bure na unasaidia Tume kuelewa mahitaji ya wabunifu. Hata hivyo, ilionekana wazi haja ya kuwa na mfumo unaoendana na matarajio ya maendeleo ya taifa.
“Utambuzi huu utajenga imani kwa wawekezaji, wadhibiti na washirika wa maendeleo. Pia utarahisisha majaribio ya bidhaa sokoni na kuingia mikataba ya kibiashara,” anasema.
Hatua hiyo imejikita katika Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050, ambako mabadiliko ya kidijitali yametajwa kuwa miongoni mwa nguzo kuu za ukuaji, huku ujasiriamali wa vijana na ajira endelevu vikiwa kiini cha uchumi wa Tanzania wa baadaye.