KIUNGO mshambuliaji wa TRA United, Ramadhan Salum Chobwedo, ingawa kwa sasa amefunga bao moja dhidi ya Tanzania Prisons, anasema malengo yake makuu ni kuhakikisha mchango wake unasaidia timu kushinda.
Chobwedo alisajiliwa na TRA dirisha dogo la msimu uliopita akitokea KenGold, ambapo alicheza nusu msimu kabla ya timu hiyo kushuka daraja. Anasema kwamba malengo ya timu yanapita mbele ya yale binafsi, hivyo anapopata nafasi ya kucheza anahakikisha mchango wake ni muhimu.
“Ligi ni ngumu na ina ushindani mkali, hivyo jambo la msingi ni tunapambania pointi tatu kila tunapocheza mechi. Ndiyo maana nasema malengo ya timu ni muhimu kuliko ya mchezaji binafsi. Pia kuna ushindani wa namba ambao unanipa chachu ya kujituma kwa bidii mazoezini,” amesema Chobwedo.
Aliongeza: “Timu inapokuwa na ushindani wa namba, kila mchezaji atajituma ili kumshawishi kocha kumpanga. Hilo kwangu nalifurahia, linanisaidia nisijisahau na kujua bado nina safari ndefu.”
Katika nafasi yake, wachezaji wanaoshindana naye namba ni Denis Nkane aliyejiunga nao dirisha dogo msimu huu akitokea Yanga, Enock Jiah aliyecheza nje kwa muda baada ya kuachana na Fanja FC ya Oman, Muhsin Malima kutoka Azam, na Shaban Chilunda aliyekuwa TRA tangu msimu uliopita.
“Ni wachezaji wazuri wenye ushindani na wazoefu. Nafurahi kucheza nao pamoja kwa sababu tunajenga na kupambania malengo ya timu moja, kila mmoja wetu kocha anatupa nafasi ya kucheza mechi,” amesema Chobwedo.