Wakati Soko la Sabasaba likiendelea kuwa kitovu kikuu cha biashara katikati ya Jiji la Dodoma, changamoto ya miundombinu ya vyoo imeanza kuonekana si tu kama suala la afya ya jamii, bali pia kama kikwazo cha moja kwa moja kwa ukuaji wa biashara.
Uchunguzi uliofanywa na Mwananchi umebaini kuwa baadhi ya wafanyabiashara hulazimika kutumia makopo na chupa kujistiri kwa haja ndogo ili kukwepa gharama ya Sh300 kwa kila matumizi ya choo gharama ambayo kwa kipato cha chini cha Sh2,000 kwa siku, inakuwa mzigo mkubwa wa uendeshaji.
Soko la sabasaba lipo katikati ya Jiji na kwa siku linahudumia watu zaidi ya 7200 wakiwemo wafanyabiashara wa moja kwa moja ambapo idadi yao inakadiriwa kufikia hadi watu 5500.
Katika idadi hiyo, vyoo vinavyotumika humo ndani vipo vinne ambavyo vimejengwa ndani ya yaliyokuwa majengo ya biashara hivyo hutumiwa zaidi na wenyeji kwani hakuna kilichojengwa eneo la wazi kuonyesha kwamba huduma zinapatikana hapo na gharama za kutumia huduma hiyo ni Sh300 kwa mara moja.
Wakizungumza na Mwananchi leo Februari 13, 2026, baadhi ya wanawake wanaofanya biashara sokoni hapo wanasema tatizo hilo limesababisha athari za kimazingira, kwani wafanyabiashara wasiokuwa na fedha hulazimika kujisaidia kwenye vichochoro na maeneo yasiyo rasmi.
Salma Jafar, anayefanya kazi ya kusambaza chakula kwa wafanyabiashara anasema ina mgharimu kati ya Sh600 hadi 900 kwa siku ili aweze kupata huduma kwa haja ndogo kila siku kitu ambacho anaona kazi anayofanya inaishia kulipia gharama za choo.
Salma anabainisha kuwa, malipo kwa kazi anayofanya ni Sh2000 kwa kutwa hivyo fedha nyingi anaziacha kwa watoa huduma za vyoo kwani hurudi nyumbani kwake na kiasi kisichozidi Sh1100 kwa siku.
“Ukitoa Sh900 ya choo, unabaki na Sh1100 ambayo bado inatakiwa igawanywe kwa nauli na mahitaji mengine sasa bila kutumia ujanja mwingine unajikuta hakuna kinachobaki kwa ajili ya familia,” anasema Salma.
Kwa mujibu wa Salma, wanaopata shida zaidi ni wafanyabiashara na watoa huduma wanawake ambao kutokana na maumbile yao ina walimu mara nyingi kukimbilia vyooni tofauti na wanaume.
“Tunaomba Serikali na uongozi wa Jiji la Dodoma kuchukua hatua za haraka za kutujengea vyoo vya gharama nafuu, lakini ikibidi tulipie malipo ya mfumo wa kadi za uanachama huenda kwa mwezi inaweza kuwa chini kidogo kuliko tunavyolipia sasa,” anasema Salma.
Joyce Mahube yeye anasema mbali na kipato cha Sh2000 kwa siku, lakini sehemu kubwa ya wanawake wanafanya biashara za mbogamboga ambazo zinapangwa chini tena kwenye jua jambo linalowafanya hata kushindwa kuwa na vichochoro vya kujibanza.
Joyce anaeleza namna wanavyokwepa kunywa maji ama kutumia vitu vya majimaji wakihofia kwenda chooni mara kwa mara ambako kunaweza kuwagharimu fedha nyingi.
“Unakuta mtu mzima analazimika kujisitiri kwa kutumia kopo, si kwa kupenda bali kwa kukosa fedha, lakini hapo uwe na kipenyo cha kujificha, kweli hii ni aibu na ni hatari kiafya,” anasema Joyce.
Akizungumzia changamoto hiyo, Mwenyekiti wa Soko la Sabasaba, Adam Kombo, amesema uongozi wa soko umeanza kutafuta suluhisho la kudumu kwa kuandaa mpango wa ujenzi wa vyoo vitakavyotoza Sh200 kwa matumizi.
Kombo anasema wako kwenye mazungumzo na wamiliki wa vyoo ili kupunguza gharama, lakini changamoto iliyopo ni wao kudai gharama kubwa za uendeshaji ikiwemo maji na vifaa vya usafi
Mwenyekiti huyo anasema Jumla ya wafanyabiashara ndani ya Soko hilo wanafika 14,000 waliopo ndani ya eneo la ekari 12.5 lakini watu wanaopata huduma kila siku sokoni hapo wanafikia 100,000 huku akikiri matundu ya vyoo yaliyopo hayatoshi.
Mmoja wa wamiliki wa vyoo hivyo ambao waligeuza sehemu ya maduka yao kuwa vyoo Awadh Ismail anasema bei wanayotoza ni ya kawaida kwani wanafanya hivyo kwa kuangalia gharama za maisha ikiwemo kupanda kwa gharama za maji, sabuni na vifaa vya ujenzi.
Awadh anasema hali hiyo imewapelekea kudhibiti idadi ya watumiaji na wanaotumia wanafanya hivyo kwa masharti yaliyopo licha ya athari zake kiafya na kimazingira.
Mmiliki mwingine George Mazengo anasema kuwa wananufaika na hali hiyo hasa baada ya kukosekana kwa mfumo mbadala wa ushindani hali inayowapa uhuru wa kupanga bei bila shinikizo la uongozi wa soko.
“Hakuna vyoo vya umma ambavyo vinasimamiwa na Halmashauri au uongozi wa soko, sisi wamiliki binafsi tunauza bei hiyo kwa kuangalia namna tunavyoweza kuboresha huduma zetu maana kwenye wingi wa watu lazima usafi kwanza,” anasema Mazengo.
Kwa mujibu wa Mazengo, wastani wa pato kwa siku katika huduma hiyo wanapata Sh280,000 hadi Sh310,000 kipindi cha kiangazi lakini bei hiyo hupungua kipindi cha nyakati za mvua kwani iko tabia ya baadhi ya watu kutumia maji yanayotembea kumwaga mikojo ama kujisaidia maeneo ya maficho hasa kwa wanaume.
Naye Mkuu wa Idara ya Usafi wa Mazingira na Udhibiti wa Taka Ngumu katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Dickson Kimaro, amesema ni muhimu kwa wafanyabiashara kuhakikisha wanatumia vyoo kwa usahihi na kudumisha usafi katika maeneo wanayofanyia kazi zao.
Kimaro anasisitiza kuwa Halmashauri ya Jiji la Dodoma imejipanga kwa kushirikiana na uongozi wa soko kuchukua hatua zitakazosaidia kupunguza gharama za huduma za vyoo ili kuwawezesha wafanyabiashara kuendelea na shughuli zao kwa ufanisi.
“Ni jukumu letu kuhakikisha huduma za vyoo zinakuwa nafuu na zenye ubora ili kulinda afya za wananchi na kuzuia uchafuzi wa mazingira, soko hili linabeba watu wengi kwa hiyo tumeelekeza macho huku,” amesema Kimaro.
Anasema juhudi za mazungumzo kati ya Serikali ya Jiji, uongozi wa soko na wamiliki wa vyoo, na mipango ya kupunguza gharama na kuimarisha elimu ya usafi, zinaashiria mwelekeo wa kupata suluhisho la kudumu ndani ya soko la sabasaba.
Iwapo mikakati hiyo itatekelezwa kwa vitendo, wafanyabiashara wataondokana na mzigo wa gharama kubwa za vyoo, mazingira ya soko yatabaki safi, na afya ya wananchi italindwa hatua itakayoweka msingi wa biashara salama na yenye tija jijini Dodoma.