Za ndaaaani beki Simba mambo magumu

WAKATI uongozi wa Simba SC ukiendelea kuumiza kichwa juu ya majeraha yanayowaandama wachezaji, hasa safu ya ulinzi, mapya yameibuka ikielezwa kuwa Abdulrazack Hamza amemaliza msimu ndani ya Simba.

Hamza aliumia kwenye mchezo wa Ngao ya Jamii kati ya Simba na Young Africans SC (Yanga), uliomalizika kwa Simba kukubali kichapo cha bao 1-0, na baadaye kwenda kufanyiwa matibabu nchini Morocco katika Kliniki ya Zerktouni.

Mchezaji huyo alifanyiwa upasuaji Desemba Mosi, mwaka jana, kufuatia kupata majeraha katika mchezo wa Ngao ya Jamii uliofanyika Septemba 16 katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, jijini Dar es Salaam.

Chanzo cha kuaminika kutoka ndani ya Simba kililiambia Mwanaspoti kuwa beki huyo anaendelea vizuri, lakini wataendelea kumkosa hadi mwisho wa msimu wakifuata taratibu walizopatiwa na madaktari ili mchezaji huyo arudi akiwa imara na kuendelea kuitumikia Simba.

“Awali matarajio yalikuwa ni beki huyo kurejea uwanjani mapema, lakini mambo yamekuwa tofauti kwani imeelezwa alikuwa na jeraha kubwa linalohitaji mapumziko ya muda baada ya kufanyiwa upasuaji. Nafikiri hili si jambo zuri kwa mchezaji na kwa klabu kwa ujumla,” kilisema chanzo hicho.

Chanzo hicho kilisema sababu ya kumuweka nje kwa muda zaidi pia imechangiwa na kucheleweshwa kufanyiwa upasuaji baada ya kubaini ana shida ya goti, hivyo jeraha likawa linaendelea kukua.

Mtaalamu wa kuchua misul), Hamis Kimweri alipotafutwa amesema kazi yake ni kuwatibu na taarifa zake huzipeleka kwa daktari ambaye pia huijulisha idara ya habari ili iwafikishie wadau na mashabiki wa Simba.

“Siwezi kuzungumzia hili siyo kazi yangu. Mtu sahihi ni daktari ambaye mimi namripoti kwake, lakini pia Ahmed Ally ambaye ndiye mzungumzaji wa taarifa za wachezaji,” amesema.

Mwanaspoti lilimtafuta Daktari wa Simba, Edwin Kagabo, lakini hakupatikana na hata simu yake kila ilipopigwa iliita bila kupokewa.