Global Publishers
February 24, 2026
0 Comments
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba amewaonya watumishi wa Halmashauri mbalimbali ambao wamekuwa wakichukua vizimba katika masoko mbalimbali na kuvikodisha kwa gharama ya juu kwa wafanyabiashara, akisema ikiwa atabaini kufanyika kwa tabia hiyo, mtumishi huyo atakuwa amejifukuzisha kazi serikalini.
Waziri Mkuu Mwigulu amebainisha hayo leo Jumanne Februari 24, 2026 Mkoani Arusha, wakati akizungumza na wananchi kwenye Mkutano wake wa hadhara mara baada ya kuweka jiwe la msingi kwenye soko la Kilombero Jijini Arusha, akisisitiza kupewa vizimba kwa wafanyabiashara husika.
“Vizimba hivi wapewe watu wanaofanya biashara na hii haiitaji mtu wa kati, ulanguzi, unyonyaji au wizi sasa Mkurugenzi wa Jiji hatutarajii kumkuta Mtumishi wa serikali akishikilia kibanda, ifanyike sensa kama kwenye soko la zamani walikuwa wanashika vibanda hapa hakuna kumiliki kama si mfanyabiashara.” Amesema Waziri Mkuu.

Aidha Mhe. Mwigulu amesema Rais Samia Suluhu Hassan ametoa kibali katika mwaka wa fedha ujao, kuongeza asilimia tano kwaajili ya kujenga miundombinu ya masoko, kwa kuzingatia upatikanaji wa wateja, akitaka masoko hayo kujengwa katika maeneo ya Kimkakati yatakayokuwa na wateja.
Mwigulu pia amesema hatarajii kuona wafanyabiashara wakifanya biashara katika masoko yasiyokuwa nadhifu, akiagiza Majiji na Manispaa zote nchini kuweka utaratibu wa kuhakikisha masoko yanakuwa nadhifu na yenye muonekano mzuri, akitaka masoko yafanane na nchi yenye uchumi wa kipato cha kati.
