MWANAFUNZI wa mwaka wa tatu katika Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (Muhas), Jocelyne Joshua, amesema wao kama kikundi cha Tanzania Biomedical Engineering Students Association (TABESA) wamebuni teknolojia maalum itakayowawezesha watu wenye changamoto ya usikivu kujumuika kikamilifu katika jamii na kueleweka kwa urahisi.
Jocelyne ambaye anasomea ya Shahada ya Uhandisi Tiba amesema awali waliamini kuwa watu wenye changamoto ya usikivu ni lazima wawe na msaidizi wa pembeni kwa ajili ya kutafsiri lugha za alama, lakini uhalisia ni kwamba wasaidizi hao ni wachache sana hali inayowafanya wahusika kukutana na watu wengi wasioweza kuwasiliana nao kwa lugha ya alama.
Amesema bunifu hiyo imekuja na application yenye uwezo wa kubadili alama za vidole na kuzipeleka moja kwa moja katika maneno na sauti ili kusaidia katika mawasiliano.
“Kwa mfano, walimu wanaofundisha watoto wenye changamoto hizi inapaswa wawe wanazijua lugha za alama au wawe na mtu wa pembeni atakayewasaidia kuwaelewesha wanafunzi darasani na kuwasaidia kuelewa masomo,” amesema.
Alisema kwa kutumia teknolojia hiyo, inaweza kuunganishwa darasani ambapo mwalimu akifundisha, mwanafunzi ataweza kuona kwenye screen kile ambacho mwalimu anazungumza hata kama mwalimu hajui lugha ya alama.
Kwa sasa wana bidhaa tatu; ya kwanza ni application inayoitwa Sauti App, ya pili ni tovuti inayoitwa Sauti Web, na pia wanatarajia kuja na kifaa maalum kwa ajili ya wale wanaopata changamoto ya kumudu au kupata simu janja ili kiwasaidie katika mawasiliano wanapokuwa wanatembea.
Amesema tayari wameshafanya usajili BRELA na sehemu nyingine husika ili kadri wanavyoendelea kuboresha bidhaa zao iwe rahisi kuzipeleka sokoni kwa kuwa tayari zimetambulika.
TABESA ni kikundi cha wanafunzi wa mwaka wa tatu wa Biomedical Engineering chenye wanafunzi wa fani mbalimbali, akiwemo mmoja ambaye hasikii wala haongei lakini bado anachangia mawazo yake kikamilifu katika utekelezaji wa mradi huo.