Dada asimulia maisha ya utoto ya Kardinali Pengo

Dar es Salaam. Katika historia ya Kanisa Katoliki Tanzania, jina la Polycarp Kardinali Pengo limebeba uzito mkubwa wa kiroho; hata hivyo, nyuma ya mavazi yake ya ukardinali kuna simulizi ya familia iliyomlea na kumshuhudia akipanda ngazi za utumishi wake.

Hadi Kardinali Pengo anastaafu, amelitumikia kanisa kwa jumla ya miaka 54 akiwa padri. Miaka 42 ametumika katika nafasi ya uaskofu na wadhifa wa kardinali kwa miaka 27.

Kardinali Pengo alifariki dunia Februari 19, 2026, alipokuwa akipatiwa matibabu katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), iliyopo Jijini Dar es Salaam.

Kutoka ndani ya nyumba ya kifamilia hadi madhabahuni, hadithi ya Kardinali Pengo si ya uongozi wa kanisa pekee, bali pia ni ya malezi, maadili na urithi wa kiimani.

Akizungumzia safari ya kiroho ya Kardinali Pengo, dada yake, Helena Pengo amesema misimamo na ukimya wa kaka yao vilianza tangu utoto wake, akieleza namna (Kardinali Pengo) alivyoweka nadhiri ya kutaka kuwa askofu.

Akizungumza na Mwananchi nyumbani kwake Temeke, jijini Dar es Salaam leo Jumatano Februari 25, 2026, ambako familia inaendelea na maombolezo ya kifo cha ndugu yao, Helena amesema kaka yao alikuwa mtoto pekee ambaye wazazi wao hawakuwahi kumchapa katika makuzi yake.

“Alikuwa mtii na hakupenda uongo. Alikasirika sana alipogundua umemdanganya. Hayo ndiyo yalikuwa maisha yake. Ilikuwa vigumu kwa wazazi kumuadhibu kwa kosa lolote. Sisi wengine tuliadhibiwa, lakini si yeye,” amesema.

Dada wa marehemu, Helena Pengo akizungumza na mwandishi wa gazeti la Mwananchi, nyumbani kwa marehemu Chang’ombe, jijini Dar es Salam. Picha na Michael Matemanga



Akisimulia namna imani yake ilivyoanza kukua na kuweka nadhiri ya kutaka kuwa askofu, Helena amesema akiwa mtoto, Kardinali Pengo alimfuata mama yao na kumwambia anataka kuwa askofu.

“Ilikuwa baada ya kusikia tangazo kanisani kwamba, kuna sherehe ya Askofu Polycarp Nahimidiwe. Tangazo lile lilimvutia na kwa kuwa naye aliitwa Polycarp, akasema hata yeye anataka aje kuwa askofu,” amesema dada yake Kardinali Pengo.

Amesema katika azimio hilo, mama yao alimwambia hawezi kuwa askofu bila ya kuwa Padri, lakini kaka yao (Kardinali Pengo) alisisitiza kuwa atakuwa tu.

“Mama alitabasamu na kumwambia, sawa, ngoja tutaona. Alipohitimu darasa la nne, alijiunga na seminari na huko ndipo safari yake ya kiroho ilipoanzia,” amesema.

Amesema katika makuzi yao, Polycarp (Kardinali Pengo) alikuwa mtoto pekee kati ya tisa ambaye hakuwahi kuchapwa na wazazi wao.

“Alikuwa mtii, mkimya na hakupenda uongo. Akigundua umemdanganya alichukia sana. Hata yeye alikuwa mkweli na ikitokea tumefanya kosa, baba aliamini yeye hausiki na mara nyingi ndivyo ilivyokuwa,” amesema.

Amesema jambo ambalo ndugu yao alilithamini sana ni kujitoa kwa dada yao mkubwa, Mwamkodula Pengo, aliyepewa jukumu la kuwasomesha wadogo zake watano, akiwamo Kardinali Pengo.

Ndugu na jamaa wakiimba msibani.



“Baba yetu hakuwa amesoma sana, lakini alimpeleka dada yetu mkubwa shule hadi akawa mwalimu. Baada ya kuajiriwa, alisema hataolewa hadi atusomeshe sisi wadogo zake.

“Yeye Polycarp (Kardinali Pengo), mimi (Helena) na ndugu zetu wengine, Modesti na Gasper, aliwasomesha. Alibeba jukumu la baba. Jambo hilo kaka (Kardinali Pengo) aliliheshimu na kulithamini sana,” amesema Helena, ambaye ni mtoto wa nane kati ya tisa katika familia yao.

Kardinali Pengo alikuwa wa sita kuzaliwa, katika makuzi yake, anatajwa kuwa mtoto mtulivu na asiye na ugomvi, tofauti na ndugu yao wa saba aliyekuwa mjanja zaidi.

“Tukiwa kijijini, tulipokuwa tukienda shambani yeye (Kardinali Pengo) alikuwa akituelekeza. Katika utoto, wengi hupenda kudanganya, lakini hilo halikuwa kwake. Ikiwa ni nyeusi, angesema ni nyeusi; na ikiwa ni nyeupe, angesema ni nyeupe. Alikuwa mtu wa misimamo sana,” amesema.

Akizungumzia maisha yake ya kiroho, amesema malezi ya ukimya, usikivu na upendo aliokulia ndiyo aliyoyaishi katika safari yake ya imani. Amesema hakuruhusu familia kumshauri kuhusu masuala ya kanisa, akisisitiza kuwa masuala hayo yanawahusu washauri wa kanisa pekee.

“Hakupenda kabisa watu kuingilia masuala ya kanisa. Kuna nyakati hilo lilimletea changamoto, lakini huo ndiyo ulikuwa msimamo wake. Hata katika jamii, wapo ambao hawakupenda, lakini huo ndiyo ulikuwa ukweli wake,” amesema.

Amesema nje ya majukumu ya kiroho, Kardinali Pengo alipenda kupiga kinanda na kuimba akimtaja kuwa alikuwa mpigaji wa ala za muziki.

Mwananchi imefika eneo atakalozikwa Kardinali Pengo Februari 28, 2026 kama alivyotangaza Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Jude Thadaeus Ruwa’ichi.

Kardinali Pengo atazikwa Jumamosi, Februari 28, katika Kituo cha Hija kilichopo Pugu, eneo aliloliandaa mwenyewe miaka michache iliyopita na kuonesha nia ya kutaka kuzikwa huko.

Mwili wake utazikwa ndani ya kanisa linalotumika kwa misa za hija katika kituo hicho kilichofunguliwa Julai 7, 1995 na Kardinali Pengo anayetajwa kuwa muasisi wa eneo hilo.


Misa ya maziko yake itafanyika Jumamosi eneo hilo, kuanzia saa 4:00 asubuhi.

Kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa na Askofu Ruwa’Ichi, Ijumaa Februari 27, mwili wa marehemu utachukuliwa kutoka Lugalo na kuletwa katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Joseph (St Joseph Cathedral) kuanzia saa tatu asubuhi, waumini na wananchi watapata nafasi ya kutoa heshima za mwisho.

“Misa takatifu ya kumuombea itaanza saa saba mchana, baada ya misa hiyo waombolezaji wataendelea kutoa heshima hadi saa 10 jioni, itakapoadhimishwa misa nyingine. Baada ya hapo, mwili utabaki kanisani kwa ajili ya ibada ya mkesha kwa watakaopenda kukesha wakisali na kuimba,” amesema Ruwa’ichi.

Amesema Jumamosi ya Februari 28, saa 12 alfajiri, mwili utaondolewa Kanisa Kuu la St Joseph na kupelekwa Pugu, ambako misa ya mazishi itaanza saa nne asubuhi.

Askofu Mkuu Ruwa’ichi amesema amepokea msiba huo kwa imani, akimuomba Mungu amjalie marehemu pumziko la milele na kuwataka waumini na watu wote wenye mapenzi mema kujitokeza kwa wingi kushiriki ibada na maziko hayo.