Mahakama Kuu Yafungua Kikao cha Mwaka, Jaji Kiongozi Asisitiza Uwajibikaji

Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Dkt. Mustepher Mohamed Siyani.

Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Dkt. Mustepher Mohamed Siyani, amewasisitiza Majaji, Mahakimu na Wakurugenzi wa Mahakama ya Tanzania kuhakikisha wanatekeleza mikakati inayowekwa na vikao mbalimbali pamoja na kuwasilisha utekelezaji wake kwa wakati.

Dkt. Siyani ametoa rai hiyo leo tarehe 25 Februari, 2026 kabla ya kumkaribisha Jaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, George Masaju, kufungua kikao cha mwaka cha Majaji Wafawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania kwa mwaka 2026, kinachofanyika katika ukumbi wa Mahakama, Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma.

Jaji Kiongozi amesema kuwa lengo na shabaha ya vikao hivyo ambavyo hufanyika walau mara moja kila mwaka ni kupata fursa ya kujipima na kujitathmini juu ya utendaji kazi wa Mahakama, sambamba na utekelezaji wa Dira na Dhima ya Mahakama.

“Kwa hiyo, lengo la vikao hivi ni kujitathmini wapi tumefanya vizuri lakini pia maeneo gani hatukufanya vizuri, matokeo ya tathmini hii ni kuboresha mchakato mzima wa utoaji haki nchini, jukumu ambalo Mahakama imekasimiwa na umma kupitia Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,” amesema Dkt. Siyani.

Ameeleza kuwa siyo vema hata kidogo kwa Viongozi kusubiri maelekezo ili kutekeleza mikakati inayowekwa. Amemtambua kwa namna ya pekee Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Manyara, Alvin Mgeta, ambaye amekua akitekeleza mikakati ya vikao mbalimbali bila kusubiri barua au maelekezo kutoka Mahakama Kuu.

“Ninalolisema kwa Waheshimiwa Majaji nalisema pia kwa Wakurugenzi wengine ambao kwa nafasi zao wanahudhuria vikao hivi na hivyo wana wajibu wa kutekeleza mikakati na yale ambayo yanaelekezwa, siyo vema hata kidogo kwa Viongozi kusubiri maelekezo ili kutekeleza mikakati inayowekwa,’amesisitiza Jaji Kiongozi.

Akitoa taswira ya utendaji kazi wa Mahakama Kuu na Mahakama zilizopo chini yake, Dkt. Siyani amesema kuwa Mahakama ya Tanzania ilivuka mwaka 2024 kukiwa na mashauri yaliyobaki 38,121.