Dar es Salaam. Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (Nida) iko mbioni kuanza kutoa aina mpya ya Vitambulisho vya Taifa ambavyo vimeboreshwa na kuongezewa huduma nane ndani yake.
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi wa Uzalishaji wa Vitambulisho wa Nida, Edson Guyai katika mahojiano maalumu na Mwananchi yaliyofanyika Jumatatu, Februari 23, 2026.
Wanufaika wa vitambulisho hivi vipya watakuwa ni wale wanaojiandikisha kwa mara ya kwanza kuanzia siku vitakapozinduliwa rasmi, lakini havitaondoa uhalali wa vitambulisho vilivyotolewa miaka ya nyuma.
Guyai amesema vitambulisho vilivyoboresha vitakwenda kukomesha kabisa uzalishaji wa vitambulisho bandia mitaani, kwa kuwa vipya vitabeba alama za wazi ambazo ni vigumu mtu kughushi.
“Tumeweka alama za usalama ambazo ni ngumu mtu kughushi, kupitia alama hizi tunaamini kitendo cha wamiliki wa steshenari na watu wengine kutengeneza mfano wa vitambulisho vyetu, utakuwa umefikia kikomo,” amesema.
Amesema lengo la kufanya maboresho hayo ni kuwezesha mwananchi kupata huduma mbalimbali kupitia kitambulisho cha Taifa, badala ya kuwa na ulazima wa kumiliki vitambulisho vya aina tofauti.
“Mtu atakuwa na uwezo wa kupata huduma zaidi ya nane. Hii itaondoa ulazima wa kuwa na vitambulisho vingi ili kupata huduma hizo,” amesema Guyai.
Moja ya vitu muhimu vilivyoongezwa katika kitambulisho hicho ni namba maalumu ambazo zitakuwa mbadala wa pasi ya kusafiria (Machine Readable Zone), ambazo zitamwezesha mtu kwenda katika baadhi ya nchi ambazo pasi ya Tanzania inakubalika.
“Mtu akiwa na kitambulisho hiki hatakuwa na ulazima wa kwenda kuchukua hati ya dharura kwa ajili ya kwenda Kenya au Uganda. Hii pia itarahisisha ufanyaji wa biashara za kuvuka mipaka,” amesema.
Eneo lingine muhimu ni taarifa za afya za muhusika ambazo zitakuwa zikitumika nyakati mbalimbali ikiwemo zile za dharura kwani kitambulisho chake kitakapoingizwa katika mfumo kitaweza kuzitoa.
“Ikitokea mtu amedondoka, mkiingiza namba yake ya utambulisho mnaweza kupata taarifa anasumbuliwa na nini, huduma ya kwanza afanyiwe nini, kama ana mzio (allergy) unahusu kitu gani, dawa gani asipewe na mengineyo,” amesema.
Hata hivyo, vitambulisho vilivyokuwa vikitolewa awali na Nida vitaendelea kuwa halali, ingawa wenye navyo watakaohitaji kupata vipya vyenye maboresho hayo, watalazimika kulipia Sh20, 000.
“Utambulisho wako ni namba tu, kwa hiyo ukihisi unataka kuwa na kile kipya unalipa Sh20, 000 unapewa kipya kwa sababu tumeshakupa mara ya kwanza bure, lakini ukiwa na kitambulisho cha zamani hautaweza kupata vitu vipya vilivyoongezwa,” amesema.
Mabadiliko hayo yanafanyika wakati kunza watu waliokamatwa na Nida na kufikishwa katika mikono ya sheria kwa kosa la kutengenezea watu vitambulisho bandia kinyume na utaratibu.
Uchapishaji wa vitambulisho feki vya Taifa ni kosa la jinai na ni kinyume cha Sheria ya Usajili na Utambuzi Sura ya 36 ya mwaka 2012, Kanuni ya Usajili na Utambuzi wa Watu za mwaka 2014 na Sheria ya Kanuni ya Adhabu Sura Na. 16 Rejeo la mwaka 2022.
Kosa la kutumia kitambulisho ambacho kimechapishwa mtaani halimhusu mchapishaji tu, bali hadi mmiliki wa kitambulisho akikutwa nacho atakuwa na kosa la kujibu.
“Mwananchi kuwa na nyaraka ya Serikali uliyoghushi ni kosa kwa mujibu wa sheria, adhabu zake zinaweza kuwa kifungo na faini na vimetajwa kwa kiwango tofauti,” amesema.
Katika hatua nyingine, Nida imewataka wananchi kuepuka kutapeliwa na watu wanaojifanya maofisa wa mamlaka hiyo wanaowatuma ujumbe mfupi wa maandishi ukiwatishia kuwa namba zao kufungwa.
“Mtu unatumiwa ujumbe namba yako ya Nida itafungiwa, fanya hivi na hivi kuepuka kufungiwa. Usifuate maelekezo hayo, Nida haiwasiliani na mtu kwa namba ya kawaida, ina namba maalumu ya mawasiliano, wananchi wawe makini kuepuka haya,” amesema Mkurugenzi Mkuu wa Nida, James Kaji.
Amesema wananchi hawatakiwi kutumia fedha mitaani kupata vitambulisho, badala yake wanatakiwa kwenda katika ofisi za wilaya kufanyiwa usajili na baada ya muda watatumiwa ujumbe kwenda kuchukua vitambulisho vyao vikitengenezwa.
Vilevile, Kaji ameonya wanaosusia vitambulisho vyao baada ya kutengenezwa: “Kuna madhara ya kutovichukua, hivi vitambulisho vinafungwa, kwa sababu hakijachukuliwa huenda hakihitajiki tena, huenda mtu ameshakufa. Huyu (kama yupo) atakosa huduma za msingi kwa sababu hajachukua kitambulisho chake,” amesema.
Kubaini vitambulisho feki
Akielezea namna unavyoweza kubaini vitambulisho vilivyoghushiwa, Guyai amesema zipo njia tofauti ikiwemo matumizi ya namba maalumu ambazyo mtu au taasisi huweza kuitumia atakapowezeshwa na Nida.
Pia matumizi ya UV light torch nayo yatamwezesha mtu kutambua alama za siri zilizowekwa na Nida kwenye kitambulisho husika.
“Sasa kwa mwananchi wa kawaida ni ngumu kuona hivi vitu (kwenye kitambulisho cha zamani), ndiyo maana tumekuja na kitambulisho hiki kipya ambacho hata kwa muonekano tu mtu ataweza kubaini kilichoghushiwa. Hakuna mtu wa kawaida anayeweza kughushi aina hii mpya ya kitambulisho,” amesema Guyai.
Mmoja wa wafanyabiashara aliyezungumza na Mwananchi, Sabato Msangi amesema hatua ya kitambulisho cha Taifa kuwa na uwezo wa kutambulika kama pasi ya kusafiria, itaweka urahisi kwao kama wafanyabiashara kufikia masoko ya Afrika ya Mashariki kwa haraka.
“Itaweka vitu kuwa rahisi, itaondoa mlolongo na muda ambao tulikuwa tukiutumia kutafuta hati za dharura. Mpango huu kama ulichelewa lakini ujio wake unatuweka sehemu nzuri ambayo itatusaidia kuondoa uchapishaji holela wa vitambulisho mitaani,” amesema.
Akizungumzia kwa nini uchapishaji wa vitambulisho kiholela uliendelea kufanyika mitaani kinyume na taratibu, Wakili Domonic Ndunguru amesema ni kunatokana na uchache wa ofisi rasmi nchini zinazotoa vitambulisho.
Uchache wa ofisi hizo umefanya wananchi kutumia muda mwingi kuvitafuta.
“Mtu anatumia gharama kubwa kufuata huduma, mtu anakaa Goba, Mbezi, Tegeta anakwenda kufuata kitambulisho Kawe, bado atatumia siku nzima au siku mbili hadi tatu kupata huduma hiyo, usumbufu unakuwa mkubwa,” amesema Ndunguru.
Amesema jambo hilo limefanya baadhi ya watu wanapopata vitambulisho halisi kwenda kwenye steshenari kutoa vitambulisho bandia ili wawe wanatembea navyo na vile halisi kuviacha nyumbani kwa sababu wanajua kitakapopotea kukipata ni mtihani mwingine.
“Utaratibu wa ufanyakazi wa Nida haujashuka hadi katika maeneo ya watu, hivyo ni bora huduma ziendane na mahitaji ya watu. Kwa nini wasitoe vitambulisho kama ilivyokuwa kwa vitambulisho vya kupigia kura, walishuka hadi chini hadi serikali za mitaa, kwa nini mtu akijiandikisha asiondoke na kitambulisho chake palepale,” amesema Ndunguru.
Amesema pia ni vyema Nida iangalie upya suala la uwekeji wa ofisi katika maeneo mbalimbali nchini badala ya kuwa na ofisi moja kwa wilaya, ili kuhakikisha huduma kwa wananchi zinafika kirahisi.
“Hii itawaepusha watu kukwepa kufuata huduma hizo na kutafuta namna rahisi ya kupata kitambulisho,” amesema Ndunguru.