…….
Na Carlos Claudio, Dodoma.
Serikali imetenga Shilingi bilioni 5 kufadhili wanafunzi 20 wa Shahada ya Uzamili katika fani za Sayansi Takwimu (Data Science), Akili Unde (Artificial Intelligence) na Sayansi Shirikishi kupitia mpango wa Samia Scholarship Extended (SSE DS/AI+), ikiwa ni sehemu ya mkakati wa taifa kuimarisha rasilimali watu katika teknolojia za kisasa.
Wanafunzi 10 tayari wameanza masomo yao katika Taasisi ya Afrika ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela (NM-AIST), huku wengine 10 wakitarajiwa kuanza katika Indian Institute of Technology Zanzibar.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda, alisema mpango huo maalum wa ufadhili wa uzamili umeanzishwa kwa kuzingatia mahitaji makubwa ya taifa katika maeneo ya teknolojia, ubunifu na uchambuzi wa takwimu.
“Vyuo tunavyopeleka wanafunzi wa Samia Scholarship AI/DS+ vinatoa fursa ya mafunzo kwa vitendo katika makampuni makubwa ya teknolojia na vinaendelea kudahili wanafunzi wetu,” alisema Prof. Mkenda.
Alibainisha kuwa wanafunzi waliopata ufadhili wanatoka katika shule za Serikali na zisizo za Serikali, akieleza kuwa kwa ngazi ya Uzamili udahili unafanyika kupitia mfumo wa maombi, tofauti na ngazi ya Shahada ya Kwanza ambako wanafunzi huchaguliwa kulingana na ufaulu wao wa juu kitaaluma.
Prof. Mkenda alitumia fursa hiyo kuwataka wadau mbalimbali kuunga mkono juhudi za Serikali kwa kuchangia mfuko wa Samia Scholarship, akisisitiza dhamira ya Serikali ya kuongeza uwekezaji katika masomo ya STEM (Sayansi, Teknolojia, Uhandisi na Hisabati).
Alieleza kuwa juhudi hizo zinaenda sambamba na ujenzi wa shule maalum za wasichana za sayansi katika kila mkoa, utoaji wa mikopo yenye upendeleo kwa wanafunzi wa sayansi kupitia Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu, pamoja na ufadhili kwa wahitimu bora wa Kidato cha Sita.
Aidha, aliwataka wanafunzi waliopata ufadhili wa Shahada ya Kwanza kuangalia majina yao kupitia tovuti ya Wizara ya Elimu, Tume ya Sayansi na Teknolojia Tanzania (COSTECH) na NM-AIST.
Serikali pia imesisitiza kuwa inaendelea kunyoosha na kuimarisha taratibu za kuchagua wanufaika wa ufadhili wa masomo ya juu, ikibainisha kuwa kigezo kikuu ni ubora wa kitaaluma, si hali ya kifedha ya mzazi wala aina ya shule aliyosoma mwanafunzi.
Kwa upande wake, Makamu Mkuu wa NM-AIST, Prof. Maulilio Kipanyula, alisema mpango wa SSE DS/AI+ ni uwekezaji wa kimkakati unaolenga kujenga wataalamu wa ndani wenye ushindani wa kimataifa, huku ukitoa fursa ya kubadilishana uzoefu na wanafunzi kutoka mataifa mbalimbali.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa COSTECH, Prof. Amos Nungu, aliishukuru Serikali kwa kuipa tume hiyo jukumu la kuratibu mpango huo, akisema mwitikio wa wanafunzi umekuwa mkubwa.
“Tukiwa waratibu, tunaamini mwitikio utaongezeka zaidi katika awamu zijazo. Tunajivunia fursa hii na tunaona picha kubwa ya maeneo ya kimkakati ya kuwekeza ili kupata wataalamu wa aina inayohitajika nchini,” alisema Prof. Nungu.




