Shahidi aieleza Mahakama chanzo jengo la CCM kuchomwa moto

Dar es Salaam. Mkaguzi wa Polisi mwenye namba PF 20122, Jafari Nguli (49) ameieleza Mahakama jinsi alivyobaini chanzo cha moto uliyounguza na kuteketeza jengo la Chama cha Mapinduzi (CCM) Kivule, lililopo Kata ya Majohe, Wilaya ya Ilala.

Nguli ambaye alikuwa mpelelezi mkuu katika kesi hiyo, amedai upelelezi wake ulibaini chanzo cha kuchoma jengo hilo kilitokana na vurugu zilizofanywa na watuhumiwa ambao walikiri kosa lao polisi.

Pia ripoti ya wataalamu kutoka Kikosi cha Zima Moto na Uokoaji, ilieleza washtakiwa hao walichoma moto jengo hilo kwa makusudi kwa kutumia mafuta ya petroli na wala sio ajali ya moto ya kawaida, kama ilivyoelezwa.

Mkaguzi huyo wa Polisi, ambaye ni shahidi wa nne wa upande wa Jamhuri katika kesi  ya kuchoma moto jengo la CCM Kivule, inayowakabili washtakiwa watatu, ametoa ushahidi wake leo Jumatano Februari 25, 2026 katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, ametoa ushahidi wake wakati kesi hiyo ilipoitwa kwa ajili ya usikilizwaji.

Washtakiwa katika kesi hiyo ya jinai namba 28997 ya mwaka 2025 ni Mohamed Madea (28) maarufu Teacher, Fredy Chacha (21) maarufu Chank na Peter Chobe (49).

Washtakiwa wanadaiwa kosa moja la kuchoma jengo la CCM, kinyume na kifungu 319(a) cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu, Sura 16 iliyofanyiwa marejeo mwaka 2023.

Katika shtaka lao, kwa pamoja anadaiwa Oktoba 30, 2025 muda wa usiku, katika eneo la Bwera lililopo eneo la Kivule, Kata ya Majohe, kwa makusudi walichoma moto jengo la CCM Kivule, lililopo Kata ya Majohe.

Akiongozwa kutoa ushahidi wake na wakili wa Serikali Monica Matwe, shahidi huyo alidai Oktoba 30, 2025 saa mbili asubuhi akiwa kituo cha Polisi Stakishari na aliitwa na mkuu wake wa kazi, SP Abugast Kililumo ambaye ni Mkuu wa Upelelezi wa Wilaya ya Kipolisi Ukonga na kupewa jalada lenye kumbukumbu namba STS/ IR/ 7518/2025 kwa ajili ya kulifanyia uchunguzi.

“Baada ya kupewa jalada hilo nilifanyie uchunguzi, nililisoma na kubaini lilikuwa na watuhumiwa watatu ambao ni Peter Masote, Mohamed Steven na Frank Samson,” amedai Nguli ambaye alikuwa Mpelelezi Mkuu wa kesi hiyo.

Amedai alibaini watuhumiwa wao walikuwa wamehojiwa na kuchukuliwa maelezo muda mfupi baada ya kufika kituo cha Polisi, Stakishari.

“Baada ya kugundua wamehojiwa, nilibaini kuwa washtakiwa wamekiri maelezo yao ya onyo ya kutenda kosa la kuchoma moto ofisi ya CCM Kivule, iliyopo eneo la Bwera,”  amedai Nguli ambaye ana uzoefu wa miaka 18 katika Jeshi hilo,  huku katika kitengo cha upelelezi ana uzoefu miaka tisa.

Amedai yeye mbali ya kuwa mpelelezi katika kesi hiyo, pia alikuwa mtunza jalada la kesi hiyo na ndio mpelelezi mkuu wa kesi hiyo.

“Nilivyopewa jalada na kiongozi wangu pale kituoni, nilitoka na kwenda  mahabusu na kisha kuwaita majina washtakiwa hao kwa ajili ya kuthibitisha” amedai Nguli ambaye ni msaidizi wa mkuu wa upelelezi Kituo cha Polisi Stakishari.

Amedai mshtakiwa Peter alichukuliwa maelezo na Sajenti Said, huku Sajenti Noel akichukua maelezo ya onyo ya mshtakiwa Mohamed.

Hata hivyo, shahidi huyo alitambua maelezo ya onyo ya washtakiwa wawili ambao ni Peter na Mohamed, ambayo yalishapokelewa na mahakama na kuwa kielelezo cha kwanza cha upande wa Jamhuri.

Baada ya kuyatambua maelezo hayo, shahidi huyo aliyasoma maelezo hayo mahakamani ambapo Mohamed ni mwalimu anayefundisha wanafunzi wa chekechea, aliyejiajiri mwenyewe na alipata mafunzo ya ualimu wa chekechea mwaka 2018.

Katika maelezo ya Mohamed, amedai Oktoba 30, 2025 alikuwa kijiwe cha bodaboda eneo la Majohe Bwera.

Amedai wakati Mohamed akiwa katika kijiwe hicho wakijadiliana na wenzake kuhusiana na vurugu zilizotokea Oktoba 29, 202, mshtakiwa Peter alipeleka mafuta ya petroli na kuchoma jengo la CCM Majohe na Ofisi ya serikali za mitaa za Kata ya Majohe.

Pia mshtakiwa huyo alitumia matairi chakavu kuzuia gari kupita na wakiwa wanahakikisha jengo la CCM linateketea, ghafla ilifika gari la Polisi likiwa linarusha mabomu ya machozi na wao walikimbia na baadaye walilipiga mawe.

“Baada ya hapo, Mohamed na Peter walirudi majumbani kwao na ilipofika  saa mbili, walienda watu sita nyumbani kwa Mohamed na Peter na kujitambulisha kuwa wao ni askari Polisi na kisha kuwakamata kwa tuhuma  za kuchoma jengo la CCM na kuwapeleka kituo cha Polisi Stakishari” amedai shahidi huyo ambaye alipata mafunzo ya upelelezi katika chuo cha Taaluma ya  Polisi, Kidatu mkoani Morogoro mwaka 2013 na kumaliza 2024.

Amedai Oktoba 31, 2025 alienda eneo la tukio na kuona ofisi ya CCM ilivyoungua na kuteketea pamoja na vitu vilivyokuwemo ndani kisha kuchora ramani.

Amedai kuwa upelelezi ulibainisha kuwa moto huo ulisababishwa na kundi la vijana ambao walichoma jengo hilo kwa kutumia mafuta ya petroli kutokana na vurugu.

Ameendelea kudai kuwa washtakiwa hao walikutwa na simu za mkononi ambazo zilipelekwa Kitengo cha Uchunguzi wa Kisayansi kwa ajili ya uchunguzi.

Shahidi huyo ameeleza pia mbali na jengo hilo kuungua, baadhi ya vitu vilivyoteketea ndani ya ofisi hiyo ni viti 20 vya plastiki pamoja na meza 15 na vifaa vingine.

Amedai kabla ya kukamilisha upelelezi wake, alimhoji na kuchukua maelezo ya Mwenyekiti wa CCM Tawi la Kivule, Emmanuel Siaga, kuhusiana na tukio hilo.

Mshtakiwa baada ya kumaliza kutoa ushahidi, alihojiwa maswali ya dodoso na Wakili wa washtakiwa Maduhu na hii ni sehemu ya mahojiano hayo.

Wakili: Shahidi wewe ni mkazi wa Dar es Salaam?

Wakili: Upo hapa Dar es Salaam kwa muda gani?

Wakili: Wewe ndio Mpelelezi Mkuu wa kesi hii?

Wakili: Sasa mueleze hakimu kama washitakiwa walikiri maelezo ya onyo ya kuchoma ofisi ya CCM Majohe, Kata ya Bwera.

Wakili: Kati yako wewe na bosi wako ASP Kilulumo aliyewaandikia barua Jeshi la Zima Moto kuomba ripoti, alikuwa wapi?

Wakili: Ukiwa kama Mkuu wa jalada la upelelezi wa kesi hii, Mkoa wa Kiupelelezi Ukonga, mlifanikiwa kukamata watu wangapi?

Wakili: Ofisi iliyochomwa moto ni ipi?

Shahidi: Majohe, mtaa wa Bwera.

Wakili: Unafahamu kama washtakiwa Peter Masote na wenzake walifikishwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Novemba 7, 2025 wakikabiliwa na kesi ya uhaini?

Wakili: Unafahamu chochote kuhusiana na ofisi ya serikali ya mitaa kuharibiwa?

Shahahi: Sifahamu chochote.

Wakili: Unafahamu nishati iliyotumika kuchoma moto jengo hilo?

Shahidi: Ndio, ni petroli

Wakili: Kwenye maelezo yako umeeleza ni petroli?

Shahidi: Ndio, yapo kwenye maelezo na ni kwa mujibu wa ripoti ya Jeshi la Zimamoto na Uokoaji

Wakili: Je, barua ya Zimamoto mliopeleka kuomba ripoti umeileta hapa mahakamani?

Shahidi: Mimi sileti barua, barua ipo kwenye jalada la kesi ambalo tunapeleka ofisi ya Taifa ya Mashtaka.

Wakili: Nje ya maelezo ya onyo, kuna kitu kingine kinachothibitisha washtakiwa walitenda kosa hilo?

Shahidi: Ripoti ya uchunguzi wa Kisayansi.

Wakili: Swali la mwisho, sasa shahidi Mahakama ichukue kipi kati ya ofisi ya CCM kivule na Ofisi ya CCM Majohe Kata ya Bwera, ipi ndio imechomwa moto?

Shahidi: Ni ofisi ya CCM Majohe.

Hakimu Mushi ameahirishwa kesi hiyo hadi Machi 2, 2026 kwa ajili ya kuendelea na usikilizwaji na washtakiwa wamerudishwa rumande kutokana na kukabiliwa na kesi nyingine ya uhaini ambayo haina dhamana kisheria.