Shilingi imesimama, Dodoma Jiji yakataa unyonge mbele ya Simba

MECHI ya Ligi Kuu Bara kati ya wenyeji, Dodoma Jiji dhidi ya Simba, imemalizika kwenye Uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma, huku ikishuhudiwa pambano hilo lililokuwa la kuvutia kutokana na ushindani tangu mwanzoni likiisha kwa suluhu (0-0).

Mechi hiyo iliyokuwa na kasi kubwa huku ikitawaliwa na ushindani wa hali ya juu, ilishuhudiwa Simba ikitengeneza nafasi nyingi za kufunga, japo uimara wa kujilinda wa kikosi cha Dodoma Jiji ‘Walima Zabibu’ uliinyima kuondoka na pointi tatu.

Simba iliingia ikiwa na kumbukumbu nzuri dhidi ya Dodoma Jiji, kwani mara ya mwisho kwa timu hizo kukutana katika Ligi Kuu, kikosi hicho kilishinda mabao 6-0, katika mechi iliyopigwa kwenye Uwanja wa KMC Complex, Mwenge, Machi 14, 2025.

Sare ya leo inakuwa ya kwanza kwa Dodoma Jiji dhidi ya Simba, kwani kikosi hicho tangu kipande daraja kutoka Ligi ya Championship hadi Ligi Kuu msimu wa 2019-2020, kilikuwa hakijashinda wala kutoka sare, zaidi ya kuambulia vichapo tu.

Tangu Dodoma Jiji ianze kucheza Ligi Kuu msimu wa 2020-2021, mechi ya leo ni ya 11, ambapo kati ya hizo imepoteza 10 na kutoka sare moja, huku kikosi hicho cha ‘Walima Zabibu’, kikifunga mabao mawili tu na kuruhusu nyavu zake kutikiswa mara 22.

Matokeo haya, yanaifanya Dodoma Jiji kuendelea kubakia nafasi ya sita kwa pointi 21, baada ya kucheza mechi 16, ambapo kati ya hizo imeshinda tano, sare sita na kupoteza tano, ikifunga mabao 14 na kuruhusu nyavu zake kutikiswa mara 15.

Kwa upande wa Simba inaendelea kubakia nafasi ya tatu kwa pointi 23, baada ya kushinda mechi zake saba, sare mbili na kupoteza moja kati ya 10, iliyocheza, huku ikifunga mabao 18 na kuruhusu nyavu zake kutikiswa mara nne.

Baada ya mechi hii, kwa sasa kikosi hicho cha Simba kinajiandaa kupambana na watani wao wa jadi Yanga, katika mechi inayotarajiwa kuwa kali na ya kusisimua inayosubiriwa kwa hamu, itakayopigwa Jumapili ya Machi 1, kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar.

Mechi hiyo ya ‘Kariakoo Derby’, inazikutanisha timu hizo zikiwa na matokeo tofauti, ambapo licha ya Simba kutoka suluhu, wapinzani wao wa jadi Yanga ambao ndio vinara wa Ligi wana pointi 28, baada ya kuichapa JKT Tanzania mabao 5-0 katika mechi iliyochezwa leo saa 10:00 jioni