::::::::
Waziri wa Fedha, Balozi Dk. Khamis Mussa Omar, amekabidhi rasmi magari mapya 72, pamoja na mawili kati ya 10 ya ofisi zinazotembea (“Mobile Tax Office Vehicles”), kwa mamlaka ya TRA. Magari haya yamenunuliwa kwa gharama ya jumla ya shilingi bilioni 24.8 na lengo kuu ni kuongeza ufanisi wa huduma za ukusanyaji wa kodi na kusaidia wafanyabiashara nchini.
Akizungumza wakati wa hafla ya ukabidhiano, Waziri Dk. Omar alisema kuwa magari haya ni mali ya Watanzania wote na yataongeza tija ya TRA bila shughuli za mbwembwe. “Magari haya ni ya kioperesheni, kwa ajili ya kufanya kazi za TRA. Yalenga kuimarisha makusanyo na kutoa huduma bora kwa wananchi,” alisema.
Kamishina Mkuu wa TRA, Tanzania Yusuph Mwenda, alibainisha kuwa baadhi ya magari yatabaki Dar es Salaam, huku mengine yakisambazwa mikoa yote nchini. Aliongeza kuwa magari haya pia yatasaidia kutoa elimu kwa wafanyabiashara, kusaidia usajili wa wateja wapya, na kuimarisha ushirikiano na sekta binafsi.
TRA inatarajia magari haya yataendeleza utulivu wa ukusanyaji wa kodi, kuongeza ufanisi wa utendaji wa mamlaka, na kufanikisha malengo ya Rais ya kuimarisha mapato ya taifa.
= = = = = = =



