Na Pamela Mollel, Arusha
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mwigulu Nchemba, ameonyesha kuridhishwa na mwenendo wa utekelezaji wa miradi ya maendeleo inayoendelea katika Jiji la Arusha, akisema kasi iliyopo inaleta matumaini mapya kwa wananchi.
Katika ziara yake ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa stendi kuu ya mabasi katika eneo la Bondeni City,Waziri Mkuu alisisitiza umuhimu wa miundombinu bora itakayokidhi mahitaji ya ukuaji wa jiji hilo. Alielekeza pia ujenzi wa barabara za njia nne ili kupunguza msongamano wa magari, sambamba na kuhimiza matumizi ya mabasi ya mwendokasi yanayotumia nishati safi ikiwemo gesi na umeme.
Akizungumza na wananchi na viongozi wa eneo hilo, Dkt. Nchemba alisema utekelezaji wa miradi hiyo ni sehemu ya dhamira ya Serikali katika kuimarisha huduma za kijamii na kukuza uchumi wa taifa.
Aidha, aliwataka wakandarasi waliolipwa na Serikali kuhakikisha wanalipa wafanyakazi wao kwa wakati, akionya kuwa haki za wafanyakazi zinapaswa kulindwa. Kuhusu vizimba vya wafanyabiashara katika stendi hiyo, alisisitiza vitolewe kwa walengwa halisi wanaofanya biashara badala ya kuhodhiwa kwa lengo la kupangisha kwa bei ya juu.
Katika ziara hiyo, Waziri Mkuu alipokea na kutatua baadhi ya kero za wananchi, akiahidi kuendeleza utaratibu huo katika maeneo mengine nchini.
Kwa upande wake, Waziri wa Habari, Michezo, Sanaa na Utamaduni, Paul Makonda, alimpongeza Waziri Mkuu kwa msisitizo wake wa kusikiliza changamoto za wananchi na kuzitafutia suluhisho. Alieleza kuwa Arusha kuna jumla ya miradi 52 inayoendelea kutekelezwa kwa kuzingatia Ilani ya Chama Cha Mapinduzi.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Amos Makalla, aliwahimiza wakandarasi kuongeza bidii ili kuhakikisha miradi inakamilika kwa wakati. Aliahidi ushirikiano wa karibu kati ya ofisi yake na wadau mbalimbali ili kusimamia utekelezaji wa miradi hiyo.
Hata hivyo, alionya dhidi ya migogoro isiyo ya lazima kati ya wafanyabiashara na baadhi ya watumishi wasio waadilifu, akisisitiza umuhimu wa uwajibikaji na maadili katika utekelezaji wa majukumu ya umma.
.jpeg)

