WAZIRI WA FEDHA AZIKABIDHI TUZO ZA UBUNIFU ZA TRA

:::::::

Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imetoa Tuzo za ubunifu kwa washindi 9 waliotoa mawazo bora zaidi yatakayosaidia kuendelea kuboresha huduma za kodi na kuongeza wigo wa kodi. 

Akikabidhi tuzo hizo, vyeti pamoja na hundi kwa washindi hao Februari 25.2026, Waziri wa Fedha Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar ameipongeza TRA kwa kuja na Tuzo hizo ambazo zitaongeza ukaribu na ushirikishwaji wa wananchi katika masuala ya ukusanyaji wa kodi. 

Waziri wa fedha amesema jukumu la kukusanya kodi ni la kila mwananchi hivyo kwa walioshiriki kutoa mawazo ya ubunifu hata kama hawakushinda wameshiriki katika kuongeza wigo wa kodi kwa kuona umuhimu wa zoezi hilo. 

Akizungumza wakati wa utolewaji wa tuzo hizo Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya TRA Bw. Uledi Mussa Abasi amesema wameamua kutoa tuzo hizo ili kuongeza wigo wa kodi na kuiweka TRA karibu zaidi na wananchi.

Kamishna Mkuu wa TRA Bw. Yusuph Juma Mwenda akizungumza katika hafla hiyo amesema Tuzo hizo ni endelevu na kwa mwaka wa fedha 2025/2026 dirisha la kupokea mawazo bunifu litafunguliwa April 1.2026 na kufungwa Juni 30.2026 ambapo watatoa muongozo wa namna ya kupangilia mawazo hayo bunifu.

Amesema kupitia mawazo bunifu TRA itaboresha zaidi huduma zake na kuongeza wigo wa kodi utakaoongeza makusanyo ya kodi na hatimaye kupunguza viwango vya kodi. 

“Ni matarajio ya walipakodi kuwa wigo ukiongezeka viwango vya kodi vitapungua, sisi pia tunayo matarajio hayo ndiyo maana tunafanya juhudi za kuongeza wigo wa kodi” amesema Kamishna Mkuu Mwenda. 

Mshindi wa jumla katika tuzo hizo ni Gabriel Mashenene ambaye amepatiwa hundi ya Sh. Milioni 50, washindi watatu wamepatiwa Sh. Milioni 30 kila mmoja huku washindi 5 wakipatiwa Sh. Milioni 20 kwa kila mmoja.

Jumla ya mawazo bunifu 5,681 yaliwasilishwa na washiriki wa tuzo hizo ambayo yalichujwa na kubakia mawazo 106 badae mawazo 9 ambayo ndiyo washindi wake wamepatiwa tuzo za Ubunifu.