Wizara ya Afya Yatoa Tahadhari Ongezeko la Influenza, UVIKO-19, Dengue na Kipindupindu – Video

WIZARA ya Afya imetoa taarifa kwa umma kuhusu mwenendo wa magonjwa ya mlipuko nchini, ikiwemo mafua makali ya Influenza, UVIKO-19, Homa ya Dengue na Kipindupindu, huku ikitoa tahadhari na wito kwa wananchi kuendelea kuchukua hatua za kujikinga.

Katika taarifa hiyo iliyotolewa jijini Dodoma, Wizara imeeleza kuwa katika kipindi cha karibuni kumekuwapo na ongezeko la wagonjwa wa mafua makali ya Influenza na UVIKO-19.

 

Magonjwa hayo huenezwa kwa njia ya hewa kupitia matone madogo yanayotoka kwa mgonjwa anapokohoa, kupiga chafya au kuzungumza, pamoja na kugusa mazingira yaliyochafuliwa.

Dalili za mafua makali ya Influenza na UVIKO-19 ni pamoja na homa kali, kikohozi, maumivu ya kichwa na mwili, mafua, kuwashwa koo na uchovu. Takwimu za ufuatiliaji zinaonesha kuwa kila mwaka kuanzia mwezi Novemba hadi Aprili, kunakuwa na ongezeko la magonjwa hayo hapa nchini na duniani.

Wizara imewahimiza wananchi kuchukua tahadhari ikiwemo kufunika pua na mdomo wanapokohoa au kupiga chafya, kunawa mikono kwa maji tiririka na sabuni au kutumia vitakasa mikono, kuepuka misongamano isiyo ya lazima, kuvaa barakoa wanapokuwa na dalili au wanapokuwa karibu na mwenye dalili, kuzingatia usafi binafsi na wa mazingira, pamoja na kuwahi katika vituo vya kutolea huduma za afya kupata matibabu stahiki.

Aidha, wananchi wametakiwa kuepuka kujitibu au kutumia antibiotiki bila ushauri wa wataalam wa afya.

 

Kuhusu Homa ya Dengue, Wizara imeeleza kuwa ugonjwa huo huongezeka wakati wa msimu wa mvua kutokana na mazalia ya mbu aina ya Aedes, ambao huuma zaidi nyakati za asubuhi, mchana na jioni.

Dalili zake ni homa kali, maumivu ya kichwa na viungo, maumivu nyuma ya macho na uchovu, na mara nyingi hufanana na dalili za malaria.

Wananchi wametakiwa kutokomeza mazalia ya mbu kwa kuondoa maji yaliyotuama kwenye makopo, matairi ya magari, vyombo na kufukia madimbwi, kujikinga na mbu kwa kuvaa nguo ndefu, kutumia dawa za kufukuza mbu na kuweka nyavu kwenye madirisha, pamoja na kuwahi kituo cha afya wanapopata dalili.