Global Publishers
February 26, 2026
0 Comments
Msanii wa muziki wa Bongo Fleva, Fatma Omary maarufu kama Gachi, amejitokeza hadharani kumuomba radhi msanii mwenzake Yammi kufuatia tuhuma alizozitoa mitandaoni hivi karibuni akimtuhumu kumchukulia mwanaume wake.
Katika hatua iliyoonekana kuwa ya kutafuta suluhu na kurejesha heshima, Gachi aliambatana na wakili wake wakati wa kutoa tamko hilo, akisisitiza kuwa jumbe alizochapisha hazikuwa na maadili wala hazikuwakilisha utu wake wa kweli.
“Sikuwaza Kwa Kina”
Kwa mujibu wa maelezo yake, Gachi alikiri kuwa alichapisha jumbe hizo kwa hasira na bila kutafakari athari zake, akiongeza kuwa kitendo hicho kimeleta taharuki na kuharibu taswira yake pamoja na kumuumiza mhusika aliyemtaja.

Alisema kuwa anajutia kwa dhati kauli hizo na yuko tayari kuchukua hatua zozote za kurekebisha makosa aliyoyafanya.
Mbali na kumuomba radhi Yammi, Gachi pia aliwaomba Watanzania kumsamehe, akieleza kuwa amejifunza umuhimu wa kujizuia na kuthibitisha taarifa kabla ya kuzitoa hadharani.
“Naomba radhi kwa wote niliowakwaza. Yale niliyoyaandika hayakuwa na maadili na hayakunionesha mimi halisi,” alinukuliwa akisema.