Hii hapa ratiba ya mazishi ya Kardinali Pengo

Dar es Salaam. Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Dar es Salaam limetoa ratiba ya mazishi ya aliyekuwa Askofu Mkuu mstaafu wa Jimbo kuu Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo yakitarajiwa kufanyika  Jumamosi Februari 28, 2026, jijini Dar es Salaam.

Kardinali Pengo alifariki dunia Februari 19, 2026, katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete alikokuwa akipatiwa matibabu, kifo kilichopokelewa kwa masikitiko makubwa na waumini wa Kanisa Katoliki pamoja na Watanzania kwa ujumla, kutokana na mchango wake mkubwa wa kiroho na kijamii nchini.

Kwa mujibu wa taarifa ya Kanisa, Ijumaa Februari 27, 2026, mwili wa marehemu utawekwa katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Yosefu kuanzia saa 3:00 asubuhi kwa ajili ya waumini kutoa heshima za mwisho hadi saa 9:30 alasiri. Misa ya kumuaga itaanza saa 10:00 jioni katika kanisa hilo.

Siku inayofuata, Jumamosi Februari 28, 2026, shughuli za maziko zitaendelea katika Kituo cha Hija Pugu ambapo mwili utawasili saa 12:45 asubuhi, huku heshima za mwisho zikitolewa kuanzia saa 1:00 hadi saa 3:30 asubuhi kisha misa ya mazishi itakayoanza saa 4:00 asubuhi.

Aidha Jimbo kuu Dar es Salaam, limetoa maelekezo maalumu kwa mapadri na mashemasi kuwa mavazi ya misa yatakuwa ya rangi nyeupe.

 Mbali na hayo, utaratibu wa maegesho umetajwa kuwa ili kurahisisha ushiriki wa waumini, magari madogo yatapaki katika eneo la GSM nyuma ya Shule ya St. Joseph’s Millennium, wakati mabasi kutoka parokiani yatapaki katika viwanja vya Karimjee  mjini na Mnazi Mmoja.

Kwa mazishi yatakayofanyika Pugu, magari yatapaki katika viwanja vya Shule ya Sekondari Pugu, yakipitia geti la shule hiyo, huku mengine yakielekezwa Parokia ya Pugu kadri yatakavyoongozwa.

Imeelezwa pia kuwa magari binafsi hayataruhusiwa kuingia ndani ya Kituo cha Hija Pugu isipokuwa yale ya maaskofu na viongozi wa Serikali.

Kardinali Pengo anakumbukwa kwa uongozi wake wa muda mrefu katika Kanisa Katoliki Tanzania, akihudumu kama Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Dar es Salaam kwa miaka mingi kabla ya kustaafu.

Wengi waliojitokeza kusaini kitabu cha maombolezo wakiwemo viongozi wa Serikali wamemtaja  kiongozi huyo wa kiroho kuwa mtu aliyelitumikia kanisa na  Taifa kwa uadilifu na unyenyekevu.