Global Publishers
February 26, 2026
0 Comments
Jaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, George Masaju, amewataka Majaji na Mahakimu nchini kutekeleza majukumu yao ipasavyo na kwa kujituma bila kusubiri maelekezo kutoka kwa Viongozi.
Masaju ametoa maagizo hayo leo Februari 25, 2026 wakati akifungua Kikao cha Mwaka cha Majaji Wafawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania kinachofanyika kwenye ukumbi wa Mikutano wa Makao Makuu ya Mahakama jijini Dodoma.
“Mimi siku zote naimba wimbo juu ya kujituma (Proactivity) na hili sio sharti langu kama nimelibuni, ni sharti la Katiba lipo kwenye Ibara ya 25 ya Katiba na kujituma huku kunatokana na kuwajibika,” amesema Jaji Mkuu.
Masaju amesema Ibara ya 25 ya Katiba inazungumza juu ya uwajibikaji wa watumishi wote wa Serikali na kila mtu, katika hotuba yangu nilipoongea na Wasajili tarehe 22 Desemba, 2025 nilizungumza kwamba hatuwezi kuishi kwa maelekezo, sisi ni binadamu tuna akili kuliko Wanyama, tunatambua wajibu wetu na tunapaswa kujua kwamba ili kama binadamu tuweze kuendelea kimwili, kiroho na kiakili tunapaswa tufanye nini,” amesema Mhe. Masaju.
Sambamba na hilo, Jaji Mkuu amewataka Maafisa Mahakama hao kujituma wanapotimiza majukumu yao kwa kuwa pia ni takwa la kikatiba kwa mujibu wa Ibara ya 25 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Masaju ameongeza kwa kuwataka Majaji hao kuwajibika kama Viongozi kwa kuimarisha uwazi na uwajibikaji kwa kuwa Mahakama inapaswa kukimbiliwa na wananchi.
Na MARY GWERA, Mahakama-Dodoma