JKT TZ yaendelea rekodi mbovu

KIPIGO cha mabao 5-0, ilichokipata JKT Tanzania juzi kwenye Uwanja wa KMC Complex, Mwenge, jijini, Dar es Salaam, katika mechi ya Ligi Kuu dhidi ya mabingwa watetezi Yanga, kimeifanya timu hiyo ya maafande kuandika rekodi mbili mbovu.

Mabao hayo ya Yanga, yalifungwa na Mohamed Hussein ‘Tshabalala’ dakika ya 7, Laurindo Dilson Maria ‘Depu’ dakika ya 60, Mudathir Yahya dakika ya 63, Prince Dube dakika ya 85, huku Shekhan Khamis akipelekea maumivu kwa kupiga la tano katika dakika ya 89.

Matokeo hayo, yameifanya JKT kuandika rekodi mbili, ambapo ya kwanza ni kufungwa idadi kubwa ya mabao kama ilivyotokea msimu wa 2023-2024, ilipochapwa 5-0, Agosti 29, 2023, huku ya pili ni kufikisha miaka sita bila ya kuifunga Yanga bao.

Katika msimu huo wa 2023-2024, Yanga ilishinda pia mabao 5-0, yaliyofungwa na Stephane Aziz KI dakika ya 45+5, Kennedy Musonda dakika ya 54, Kouassi Yao dakika ya 64, huku Maxi Mpia Nzengeli, akifunga mawili kuanzia dakika ya 79 na 88.

Mara ya mwisho kwa JKT kuifunga Yanga bao la Ligi Kuu, ilikuwa ni sare ya 1-1, katika mechi iliyopigwa kwenye Uwanja wa Jamhuri jijini, Dodoma Juni 17, 2020, ila kuanzia hapo hadi leo hii kikosi hicho cha maafande kimeshindwa kufunga bao.

Katika mechi hiyo, JKT ilipata bao kupitia kwa Michael Aidan dakika ya 36, kisha, Patrick Sibomana akaisawazishia Yanga katika dakika ya 76, huku wachezaji wawili, Lamine Moro wa Yanga na Mwinyi Kazimoto wa JKT Tanzania wakionyeshwa kadi nyekundu.

Tangu Juni 17, 2020, JKT imekutana na Yanga katika mechi saba za Ligi Kuu Bara bila ya kufunga bao lolote, ambapo kati ya hizo imechapwa tano na kutoka sare mbili, huku kikosi hicho cha maafande kikiruhusu nyavu zake kutikiswa mara 15.