Kafulila – ”Kardinali Pengo Aliamini Umoja wa Kitaifa Bila Kujali Upepo wa Kisiasa”

Bakari Mahundu
February 26, 2026
0 Comments

Mkurugenzi wa Kituo cha Ubia kati ya Serikali na Sekta Binafsi (PPP Centre), David Kafulila, amesema aliyekuwa Kiongozi wa Kanisa Katoliki nchini, Kardinali Polycarp Pengo, atakumbukwa kama kiongozi wa dini aliyeamini na kusimamia umoja wa kitaifa bila kujali upepo wa kisiasa wa wakati husika.

Kafulila amesema Kardinali Pengo alisimamia kile alichoamini kuwa ni sahihi kwa maslahi ya Taifa, hata pale ambapo misimamo yake ingeweza kupokewa tofauti katika muktadha wa kisiasa. Ameeleza kuwa Pengo hakuwa kiongozi wa kupima upepo, bali alisimama imara kwa misingi aliyoiamini inaleta mshikamano na manufaa mapana ya Taifa.

Akizungumzia mazingira ya sasa ya zama za habari (information age), Kafulila amesema kasi na nguvu ya mitandao ya kijamii imewafanya baadhi ya viongozi kutoa maoni kwa tahadhari kubwa kutokana na shinikizo la maoni ya umma. Hata hivyo, amesema Kadinari Pengo aliweza kuyamudu mawimbi hayo kwa kusisitiza alichoamini kuwa ni sahihi, bila kuyumba.

Kafulila amesisitiza kuwa dunia ya leo inakabiliwa na changamoto mpya zinazochochewa na mabadiliko ya mazingira ya habari, hivyo Taifa linapaswa kumuenzi Kardinali Pengo kwa kuendeleza misingi ya kusimamia yale yanayoweza kuunganisha Watanzania, hasa katika nyakati zenye mitihani mikubwa ya kisiasa na kijamii.