Dar es Salaam. Wakati dunia ikiendelea kuishi na maambukizi ya Uviko-19, wataalamu wa afya wameanza kufuatilia kwa karibu lahaja mpya (aina ya virusi) inayojulikana kama NB.1.8.1, ambayo ni tanzu ya familia ya Omicron ambayo ilisumbua mwaka 2025.
Ingawa tafiti za awali zinaonyesha kuwa haisababishi ugonjwa mkali zaidi kuliko lahaja zilizopita, Shirika la Afya Duniani (WHO) na Kituo cha Kukinga na Kudhibiti Magonjwa (CDC) zimeeleza kuwa na uwezo mkubwa wa kuambukiza na hivyo kuzua wasiwasi katika jamii.
Lahaja hiyo ilianza kuonekana mwishoni mwa mwaka 2025 na mwanzoni mwa 2026, imeonekana kuwa na dalili zinazofanana kwa kiasi kikubwa na mafua makali (influenza), huku kukiwa na kurejea kwa dalili ya kupoteza ladha au harufu ambayo hapo awali ilikuwa imepungua.
Nchini Tanzania tayari jana Jumatano, Februari 25, 2026, Serikali kupitia Wizara ya Afya imetoa tahadhari kwa wananchi kufuatia ongezeko la wagonjwa wa mafua makali na Uviko-19, huku ikiwasihi kuchukua hatua za kinga ili kudhibiti maambukizi.
Kwa mujibu wa taarifa mbalimbali za kitaalamu, NB.1.8.1 imegunduliwa katika maeneo kadhaa duniani na ina sifa ya kusambaa kwa haraka, hasa katika maeneo yenye mikusanyiko kama shule, ofisi, vyombo vya usafiri wa umma na ndani ya familia.
Wataalamu wanasema kasi hiyo ya maambukizi inatokana na mabadiliko madogo ya kijenetiki yanayoviwezesha virusi kuenea kwa urahisi zaidi kutoka mtu mmoja kwenda kwa mwingine.
Dalili za lahaja hii zinafanana kwa kiasi kikubwa na zile za lahaja za awali za Omicron, kwa mujibu wa takwimu zilizokusanywa na WHO.
Miongoni mwa dalili zinazoripotiwa mara kwa mara ni koo kuwasha au kuuma kwa makali, mafua au msongamano wa pua, kikohozi kikavu, uchovu, maumivu ya kichwa, homa ya kiwango cha chini, baridi na maumivu ya misuli.
Kupoteza ladha au harufu, dalili iliyokuwa maarufu mwanzoni mwa janga, sasa huripotiwa kwa nadra zaidi.
Hata hivyo, baadhi ya wagonjwa wanaweza kupata dalili zisizo za kawaida kama upungufu wa pumzi, maumivu ya kifua, kichefuchefu au kuharisha. Kwa watu wengi, dalili huanza taratibu na hupungua ndani ya siku chache.
Lakini kwa wazee, wajawazito, watu wenye magonjwa sugu kama kisukari, shinikizo la damu au magonjwa ya mapafu, pamoja na wenye kinga dhaifu, wapo katika hatari ya kupata madhara makubwa.
Changamoto kubwa kwa sasa ni kutofautisha kati ya Uviko-19, mafua ya kawaida na mzio. Mafua mara nyingi huanza ghafla yakifuatana na homa kali na maumivu makali ya mwili, wakati dalili za Uviko-19 zinaweza kuanza polepole na kuhusisha zaidi koo kuuma na uchovu wa muda mrefu.
Mzio kwa kawaida husababisha kupiga chafya na kuwashwa macho bila homa au maumivu ya mwili. Wataalamu wanasisitiza kuwa upimaji bado ni njia sahihi ya kuthibitisha maambukizi.
Wananchi wanashauriwa kupima iwapo wana dalili za mafua au wamekuwa karibu na mtu aliyethibitika kuwa na maambukizi.
Vipimo vya haraka vinavyotumika nyumbani vinaendelea kuwa na uwezo wa kugundua lahaja hii, ingawa inapendekezwa kurudia kipimo baada ya saa 24 hadi 48 kama dalili zinaendelea huku majibu ya awali yakiwa hasi.
Kwa wagonjwa wenye dalili za kawaida, matibabu hulenga kupunguza makali ya dalili kwa kupumzika, kunywa maji mengi na kutumia dawa za kushusha homa au maumivu. Watu walio katika makundi hatarishi wanaweza kupewa dawa maalumu za kupunguza makali ya ugonjwa iwapo watagundulika mapema.
Wataalamu wa afya wanaendelea kusisitiza umuhimu wa chanjo na nyongeza zake, kunawa mikono mara kwa mara, kuvaa barakoa katika maeneo yenye msongamano na kubaki nyumbani unapohisi dalili. Licha ya kupungua kwa hofu ikilinganishwa na miaka ya mwanzo ya janga, tahadhari bado inahitajika ili kulinda makundi yaliyo hatarini.
Kadiri lahaja mpya zinavyoendelea kujitokeza, uelewa wa dalili na kuchukua hatua mapema kunabaki kuwa silaha muhimu katika kupunguza maambukizi na madhara katika jamii.
Akizungumza na Mwananchi jana, Februari 25, 2026 Daktari bingwa wa magonjwa ya ndani na mfumo wa upumuaji, Elisha Osati alisema magonjwa ya mafua makali na Uviko-19 hutokea zaidi kipindi hiki cha mvua na msimu wa joto unavyoanza.
“Wakati hali ya hewa inabadilika na wadudu nao wanabadilika wanatengeneza aina mbalimbali za protini zinazowasaidia kuishi, katika mabadiliko hayo wanaweza kuleta madhara kwa watu,” alisema Dk Osati akisisitiza umuhimu wa kujikinga ili kutoambukiza wengine.