Kundemba, Vuga ngoma droo Masauni & Seif Cup

TIMU za Kundemba na Vuga zimeanza kwa suluhu katika mechi ya uzinduzi wa michuano maalumu ya Masauni & Seif Cup iliyoanza juzi kwenye Uwanja wa Mnazi Mmoja, mjini Unguja, ikishirikisha jumla ya timu 20, huku Serikali ikiahidi kuwekeza zaidi michezoni.

Klabu nyingine zinazoshiriki michuano hiyo kwa msimu huu ni; KISC FC, Ujamaa, Urusi, Misyuu, Aston Villa, Malindi, Mlandege, Mladu, Villa Coast, Muungano, Medson, Black Fighter, Kwahani, Kilimani, Mafunzo, Real Zanzibar, Rio na Galilaya.

Katika ufunguzi wa michuano hiyo juzi, Naibu Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo wa SMZ, Ali Abdulgulam Hussein aliyekuwa mgeni rasmi, alisema serikali itaendelea kuwekeza katika miundombinu ya michezo ikiwa pamoja na ujenzi wa viwanja na kuangalia fursa mbalimbali ili kuendeleza vipaji kwa vijana.

Waziri Hussein alisema serikali ipo katika mchakato wa ukarabati wa Uwanja wa Matumbaku ili michezo mbalimbali iweze kufanyika kwenye uwanja huo kama ilivyokuwa viwanja vingine.

“Nichukue nafasi hii kuwapongeza viongozi wa Jimbo la Kikwajuni kuifanya ligi hii kuwa ya Wilaya ambapo sasa inahusisha timu kutoka maeneo tofauti ikiwa ni sehemu ya kuwasaidia vijana.

Kwa upande wa Mbunge wa Jimbo la Kikwajuni, aliye pia Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais, Injinia Hamad Yussuf Masauni alisema jimbo hilo limekuwa mnufaika mkubwa wa uwekezaji wa miundombinu ya kimichezo ambaye serikali imeweka hasa katika viwanja.

Masauni alisema Kikwajuni ina historia kubwa katika michezo kwa kutoa wanamichezo wengi ambao kwa sasa wanacheza ligi mbalimbali Tanzania ndio maana ligi hiyo imekuwa ikifanyika mfululizo ndani ya miaka 15.

Aliongeza tayari kuna ujenzi wa uwanja wa kisasa utakaojumuisha michezo mbalimbali kama vile mpira wa pete, kikapu na soka ambapo hadi Januari mwakani utakuwa umeanza kutumika, huku Mbunge wa Kundi la Vijana Kanda ya Pemba, Zainab Abdallah alisisitiza kuna kila sababu ya kumpongeza Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk Hussein Ali Mwinyi kwa uwekezaji katika sekta ya michezo.

Zainab alisema uwekezaji huo umewafanya vijana waone hii ni sehemu ya ajira na Kikwajuni imeendelea kuwa mfano wa kuigwa kutokana na ushirikiano wa viongozi ambao wamewafanya vijana kuwa pamoja kila mwaka nyakati kama hizi.