KWIMBA WAISHUKURU TAASISI YA DORIS MOLLEL KUJENGA JENGO LA KISASA LA KIMATAIFA KUHUDUMIA WATOTO NJITI


Na Mwandishi Wetu,Kwimba

WANANCHI wa Wilaya ya Kwimba mkoani Mwanza wameishukuru Taasisi ya Doris Mollel (Doris Mollel Foundation) kwa kuleta mabadiliko makubwa katika Wilaya hiyo baada ya kufadhili na kusimamia ujenzi wa jengo la kisasa la Kimataifa la kuwahudumia Watoto wanaozaliwa kabla ya wakati (njiti).

Jengo hilo limejengwa katika Hospitali ya Wilaya ya Kwimba, ambapo linalosogeza huduma hizo muhimu karibu na wananchi kwa mara ya kwanza.

Akizungumza kuhusu ujenzi wa jengo hilo Mkuu wa Wilaya ya Kwimba Ng’wilabuzu Ludigija amesema ameridhishwa na utekelezaji wa mradi huo unaofadhiliwa na Taasisi ya Doris Mollel , akieleza jengo hilo litakuwa na mchango mkubwa katika kuokoa maisha ya Watoto.

Kwa upande wake mkazi wa Kwimba, Joyce Emmanuel James, ameishukuru Doris Mollel Foundation kwa kujenga jengo hilo, akieleza changamoto walizokuwa wanapitia kabla ya uwepo wa huduma hizo karibu.

Awali Mwakilishi wa Shirika la Afya Duniani (WHO) nchini Tanzania, Dkt. Alex Ntale Gasasira, ametambua uwekezaji huo na kusisitiza umuhimu wa uwepo wa huduma hizo karibu na jamii, akieleza mfumo huo unaendana na miongozo ya WHO inayosisitiza umuhimu wa Mama na Mtoto kuwa pamoja wakati wa matibabu.

Jengo hilo la kimataifa linalotarajiwa kuzinduliwa Februari 28, 2026 ,limefadhiliwa na kujengwa na Taasisi ya Doris Mollel (DMF) kwa lengo la kuboresha huduma za Watoto wachanga na kuleta matumaini mapya kwa familia za Wilaya ya Kwimba na maeneo ya jirani.Ujenzi wa jengo hilo umegharimu Sh.bilioni hilo 2.125 kwa kushirikiana na Taasisi ya Keep A Child Alive na Jhpiego.