SIMBA imevuka Bahari ya Hindi kuifuata Yanga kwa ajili ya pambano la kwanza la Dabi ya Kariakoo katika Ligi Kuu kwa msimu huu, lakini kuna jambo lililowavuruga mabosi wa klabu hiyo, hususan kocha mkuu Steve Barker, kuhusiana na kipa Yakoub Suleiman.
Si mnakumbuka kipa huyo aliyetua msimu huu kutoka JKT Tanzania, alikuwa majeruhi tangu akiwa katika Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2025 na inaelezwa alishapona na kuanza kujifua na wenzake? Basi unaambiwa jamaa ghafla juzi kati amejitonesha na kushtua mabosi.
Inadaiwa, Yakoub Suleiman ataendelea kufanya mazoezi ya kutafuta ufiti kwa takribani wiki tatu zaidi, chini ya kocha wa viungo Sibusiso Meshack Makhula, baada ya hapo wataangalia maendeleo yake kama atakuwa tayari kwa mechi.
Hivi karibuni wakati Simba ikifanya mazoezi ya kujiandaa na mechi dhidi ya Dodoma Jiji iliyotoka nayo suluhu kwenye Uwanja wa Jamhuri, Dodoma Februari 25, Yakoub aliumia enka, jambo lililoelezwa lilitokana na mwili wake kukosa ufiti.
“Enka aliyoumia juzi imetokana na kutokuwa fiti kimwili, alikuwa anafanya mazoezi ya kurudi nyuma ndipo akateguka, tulisafiri naye kwa sababu kocha anahitaji kumuona kwa ukaribu maendeleo yake, lakini anatambua kabisa anatakiwa kukaa nje kwa takribani wiki tatu,” kilisema chanzo hicho na kuongeza;
“Baada ya kuumia akiwa na timu ya taifa, Taifa Stars kule Morocco katika michuano ya AFCON wakati wanajiandaa na mechi dhidi ya Nigeria, alitakiwa kuwa nje ya uwanja kwa miezi miwili ambayo ilikuwa ya matibabu ila kwa sasa ni kutafuta ufiti wa mwili wake.”
Chanzo hicho kilisema Yakoub aliye na clean sheets mbili katika Ligi Kuu, msimu uliyopita alimaliza na nane akiwa JKT Tanzania na huduma yake inahitajika ili kusaidiana na kipa wa kigeni Djibrilla Kassali aliyetua kuchukua nafasi ya Moussa Camara aliyeumia mapema kabla ya Yakoub.
“Kitendo cha kuumia makipa wote wawili kwa pamoja Moussa Camara aliyemaliza msimu uliopita akiwa kinara wa clean sheets (19) na Yakoub, ilikuwa ni pigo, ndio maana Camara aliondolewa katika mfumo wa usajili ili kumpisha Kassali,” kiliongeza chanzo hicho kilichosisitiza kwa sasa Yakoub atasubiri nje kwa wiki tatu kabla ya kuanza kutumika, tofauti na mipango ya awali baada ya kuonekana amepona.
Kutokana na hilo, kipa na kocha wa zamani wa timu hiyo Idd Pazi amesema: “Kwa sasa makocha na viongozi wanapaswa kuendelea kumwamini kipa mzawa Hussein Abel ni mzuri ndiyo maana walimsajili, wakimpa mechi tatu mfululizo zitamjengea ujasiri.”
Kipa mwingine wa zamani wa Yanga, Benjamin Haule amesema: “Hakuna mchezaji mbaya. Wakati mwingine ni kuaminiwa tu. Kipindi ambacho Yakoub anarejea taratibu, apewe nafasi Abel ambaye ataongeza ushindani wa namba.”