Miezi minne migumu anayopitia Mzize Yanga

TAKRIBANI miezi minne imepita tangu Clement Mzize afanyiwe upasuaji wa goti, lakini hii ya sasa inaweza kuwa taarifa mbaya kwa mashabiki wa Yanga, baada ya mshambuliaji wao huyo kukumbana na majanga mengine.

Mzize imeripotiwa kujitonesha jeraha la goti na inaelezwa kuwa yupo nchini Afrika Kusini tayari kwa upasuaji mwingine.

Mzize amewatia hofu tena viongozi wa timu hiyo baada ya kutonesha jeraha lake akiwa mazoezini wakijiandaa kucheza mechi ya mwisho hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya JS Kabylie, iliyochezwa Februari 15, 2026.

Mshambuliaji huyo amejitonesha jeraha lake la goti ambalo awali ilielezwa amepona na kuruhusiwa kurudi kwenye majukumu yake.

Chanzo cha kuaminika kutoka ndani ya Yanga, kimeliambia Mwanaspoti kuwa baada ya kufanyiwa vipimo kwa mchezaji huyo, imebainika ametonesha vibaya, hivyo anatakiwa kupasuliwa tena na tayari kasafiri kwenda Afrika Kusini kwa ajili ya hilo.

“Mzize hayupo pamoja na timu, kasafiri kwa ajili ya upasuaji mwingine, nafikiri ni muda sasa tangu majibu yake yatoke na kubainika kuwa na shida nyingine kubwa katika jeraha lake, nimesikia kapelekwa Afrika Kusini,” amesema mtoa taarifa huyo ambaye hakutaka jina lake litajwe.

Wakati huohuo, Mwanaspoti lilifanya jitihada za kumtafuta Daktari wa Yanga, Moses Etutu, kuzungumzia maendeleo ya Mzize ambapo amesema mshambuliaji huyo alirudi uwanjani baada ya matibabu ya goti kwenda vizuri, lakini akiwa katika harakati za kujiandaa na mchezo dhidi ya JS Kabylie alijitonesha, hivyo tayari wamemfanyia vipimo na kumuandalia program maalum ya matibabu.

“Mzize baada ya upasuaji wa goti ambao ulienda vizuri alirejea uwanjani na kuendelea na majukumu akipata dakika chache za kucheza mechi ya ugenini dhidi ya AS FAR Rabat na baada ya hapo akiwa kwenye maandalizi ya mechi ya pili alipata shida kidogo, tatizo tayari limefanyiwa vipimo na anatarajia kuanza program ya matibabu karibuni,” alisema na kuongeza;

“Kwa sasa yupo kwenye uangalizi maalum kwa ajili ya kuona matibabu yake yanakwenda kwa uharaka ili aweze kurejea uwanjani kuendelea na majukumu yake kama kawaida.”

Awali Mzize alirejea kwenye kikosi cha Yanga baada ya kukaa nje ya uwanja kwa zaidi ya wiki nane, akipambana na majeraha ya goti yaliyomlazimu kufanyiwa upasuaji.

Jeraha hilo lilitokea Septemba 27, 2025, kwenye mechi ya awali ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Wiliete Benguela ya Angola, Yanga ikiibuka na ushindi wa mabao 3-0, lakini ushindi huo uliambatana na janga hilo.

Hali ya Mzize ilizidi kuwa mbaya zaidi baada ya kujiunga na majukumu ya timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars, ambako alijitonesha jeraha hilo. Tukio hilo lilimlazimu Novemba 2025 kufanyiwa upasuaji na kuanza safari ndefu ya kurejea kwenye ubora wake wa awali.