Mikoa yaanza kukabili Uviko-19 na mafua makali, wananchi wasuasua

Dar/Mikoani. Siku moja baada ya taarifa za ongezeko la wagonjwa wa Uviko-19 na mafua makali ya Influenza katika maeneo mbalimbali nchini, hali ya utekelezaji wa hatua za kujikinga imeanza kuchukuliwa baadhi ya maeneo, huku wananchi wakionekana kutochukua tahadhari hususan katika majiji makubwa.

Utekelezaji huo umeonekana kuanza katika ngazi za mikoa na halmashauri mbalimbali nchini.

Mkoa wa Arusha umeanza kuchukua hatua mbalimbali, ikiwemo kuandika barua kwa halmashauri zote saba (idara ya afya), ili kuhakikisha kila kituo kiko tayari, wagonjwa wenye dalili za magonjwa hayo wanapata matibabu na elimu kupitia mifumo ya serikali.

Akizungumza na Mwananchi leo, Februari 26, 2026, Ofisa Muepidemiolojia wa Mkoa wa Arusha, Dk Robert Hongo, amesema kwa siku za hivi karibuni wamewajengea uwezo watumishi wake 54 kutoka halmashauri hizo, ambao wako tayari kukabiliana na magonjwa ya mlipuko.

“Tunaendelea kufanya ufuatiliaji wa kina na kutoa elimu kwa jamii kupitia redio za jamii. Kwa sasa kuna ongezeko la watu wenye mafua na kikohozi Arusha,” amesema.

Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dk Thomas Rutachunzibwa, amesema suala hilo limeanza kushughulikiwa.

Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Dk Elizabeth Nyema, amesema tayari wameanza vikao kujadili hatua za kuchukua na kuweka wataalamu kuhakikisha wanatoa huduma kwa wagonjwa wanaobainika na ugonjwa huo.

“Tumeelekeza waliopo Kasumulu, mpakani mwa Malawi, waongeze nguvu kufanya vipimo kwa wanaoingia, bahati nzuri kuna skana pale, wafanye matibabu sahihi. Ukizingatia Mbeya kwa sasa kuna mvua na baridi,” amesema Dk Elizabeth na kuongeza kuwa wanaendelea na maandalizi ya kutoa elimu kwa wananchi.

Mganga Mkuu wa Hospitali ya Wilaya ya Rungwe, Dk Diocles Ngaiza, amesema miongoni mwa maeneo waliyoweka kipaumbele ni mikusanyiko ya watu, kwa kuwataka kujikinga hususan kunawa mikono kwa maji tiririka.

“Pia tumetoa taarifa kwa kamati za afya ngazi ya kata, baada ya Serikali kutoa tahadhari, pamoja na waganga wafawidhi wa vituo vya afya na zahanati ngazi za vijiji na kata,” amesema.

Uchunguzi uliofanywa na Mwananchi katika maeneo ya Dar es Salaam, Arusha, Mwanza, Moshi, Mbeya na Tanga umebaini kwamba licha ya msongamano mkubwa wa watu katika masoko, vituo vya mabasi, makanisa, misikiti na maeneo ya starehe, wananchi wengi hawavai barakoa wala kuzingatia umbali wa kijamii.

Vilevile, katika taasisi nyingi za umma na binafsi, hakuna vituo vya kunawa mikono vilivyowekwa kama ilivyokuwa kipindi cha awali cha mlipuko wa Uviko-19 mwanzoni mwa mwaka 2020 hadi 2023.

Kutokuchukua hatua za mapema kama kuvaa barakoa katika maeneo yenye msongamano, kunawa mikono kwa maji tiririka na sabuni, pamoja na kujitenga kwa wenye dalili, kunaweza kusababisha ongezeko la maambukizi na kuongeza mzigo kwa mfumo wa afya.

Mtaalamu wa afya ya umma, Dk Ali Mzige, amesema licha ya mikusanyiko, kaya kwa kaya zinapaswa kuanza kuzingatia kanuni za usafi na kuhakikisha wanachukua hatua za kujikinga.

“Kunapokuwa na ukame, vumbi, upepo mkali na hakuna tahadhari, ni rahisi kuambukizwa, mtu anaweza kuambukizwa kwa kushikana mikono na mtu mwingine, kutoka kwenye maji, matunda, vyakula visivyochafika, au mtu anapokohoa bila kufunika mdomo.

“Usafi unaanzia majumbani. Wanapokaa wengi mahala pamoja, ni rahisi kuambukizana kama magereza, kambini, shuleni na hospitali. Uvaaji barakoa na kunawa mikono kutasaidia kupunguza uambukizi,” amesisitiza Dk Mzige.

Alipotafutwa Mkurugenzi wa Huduma za Afya, Ustawi wa Jamii na Lishe, Ofisi ya Rais-Tamisemi, Dk Rashid Mfaume, amesema: “Maelekezo yalishatolewa na Mganga Mkuu wa Serikali. Jukumu hili sasa lipo chini ya waganga wakuu wa mikoa na wilaya kushughulikia hili.”

Katika Jiji la Dar es Salaam, ambako kuna idadi kubwa ya watu na shughuli nyingi za kiuchumi, hali ni ya kawaida kana kwamba hakuna tishio lolote la kiafya.

Mabasi yaendayo haraka (BRT) na daladala hujaa kupita kiasi bila tahadhari, huku baadhi ya abiria wakionekana kuwa na dalili za mafua lakini wakiendelea na shughuli zao bila kujitenga.

“Kwa bahati mbaya, nilisikia juu juu tu jana uwepo wa corona, lakini naendelea kubeba abiria kama kawaida. Sijaona yeyote aliyevaa barakoa wala kushika kitakasa mikono, naona labda ni maneno tu. Ingawaje wiki hii napakiza sana watu wanakohoa na kupiga chafya,” amesema Amosi Abel, mwendesha bodaboda Tabata, jijini Dar es Salaam.

Kwa upande wa daladala, madereva wamesema bado hawajachukua hatua zozote kwa kuwa hawajafuatiliwa, huku wengine wakisema hawajatangaziwa.

Katikati ya Jiji la Dodoma na maeneo ya jirani hali iko kama siku zote, hakuna maeneo yanayoonesha kuna tahadhari ya namna nyingine yenye kuonesha kama kuna tatizo.

“Hatuna taarifa kama kuna ugonjwa, nimeleta hapa mwanangu alijifungua hivi karibuni, lakini anasumbuliwa sana na mafua, hawajatuambia kama tunawe mikono na hata mgonjwa mwenyewe hajaniambia tangu nilipotoka kijijini,” amesema Ihewa Mwaluko.

Hali kama hiyo imeripotiwa pia katika miji kadhaa inayopokea watalii na wageni kutoka mataifa mbalimbali.

Mwananchi limepita katika maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Kilimanjaro na kushuhudia shughuli zikiendelea kama kawaida bila kuzingatia tahadhari za kujikinga kama kunawa mikono au kutumia vitakasa mikono.

Aidha, katika baadhi ya masoko na vituo vya mabasi, hakuna mabango au matangazo ya kuhamasisha tahadhari dhidi ya magonjwa hayo ya mlipuko.

Katika majiji ya Mwanza na Tanga, wakazi wamesema hawajapata kampeni zozote mpya za uhamasishaji kuhusu tahadhari za Uviko-19 au mafua makali.

“Maisha yanaendelea kama kawaida. Hatusikii matangazo wala kuona mabango ya tahadhari,” amesema mkazi mmoja wa Mwanza.

Wito umetolewa kwa mamlaka za afya katika ngazi za mikoa na halmashauri kurejesha kampeni za uelimishaji na kuhakikisha hatua za kinga zinazingatiwa, hasa katika majiji yenye mikusanyiko mikubwa ya watu. Bila hatua hizo, hatari ya kuibuka kwa wimbi jipya la maambukizi inaendelea kuwepo kimyakimya.

Imeandaliwa na Herieth Makwetta (Dar), Janeth Mushi (Arusha), Janeth Joseph (Moshi), Habel Chidawali (Dodoma), Hawa Mathias na Sadam Sadiki (Mbeya).