Na Pamela Mollel,Longido
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mwigulu Nchemba, amepongeza maendeleo ya ujenzi wa Mradi wa Majisafi wa Sinya–Namanga, akieleza kuwa utekelezaji wake ni hatua muhimu katika kumaliza tatizo la maji lililodumu kwa miaka mingi katika maeneo hayo.
Dkt. Nchemba alikagua mradi huo Februari 23, 2026 katika eneo la Sinya, wilayani Longido mkoani Arusha na kujionea maendeleo ya kazi yanayoendelea. Alisema kukamilika kwa mradi huo kutaleta mabadiliko makubwa kwa wakazi wa Sinya na Namanga, hasa katika kuboresha huduma za kijamii na shughuli za kiuchumi.
Mradi huo unatarajiwa kuzalisha lita milioni 4.1 za maji safi kwa siku, kiwango kitakachoongeza upatikanaji wa maji kwa matumizi ya majumbani, taasisi za kijamii pamoja na mifugo. Eneo hilo limekuwa likikabiliwa na changamoto ya uhaba wa maji kutokana na kuongezeka kwa mahitaji, huku chanzo cha Mto Simba kikishindwa kukidhi mahitaji yaliyopo.
Utekelezaji wa mradi unasimamiwa na mkandarasi Zongii Contractors Co. LTD kwa gharama ya shilingi bilioni 13.5, fedha zinazotolewa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Kwa mujibu wa taarifa ya utekelezaji, hadi Januari 2026 mradi ulikuwa umefikia asilimia 24.7 ya utekelezaji, huku hatua mbalimbali za awali zikiendelea kukamilishwa.
Akizungumza na wananchi, Waziri Mkuu anasema serikali imejipanga kuhakikisha miradi ya maji inatekelezwa kwa wakati na kwa viwango vinavyokidhi ubora unaotakiwa, ili kuondoa adha ya wananchi kutembea umbali mrefu kutafuta maji. Aliongeza kuwa upatikanaji wa maji wa uhakika utachochea maendeleo ya kijamii na kiuchumi katika ukanda huo wa mpakani.