Ni zamu ya vigogo CCM kufyekwa

Dar es Salaam. Fumua fumua ya uongozi au watendaji wa sekretarieti ya Chama cha Mapinduzi (CCM) na viongozi wengine inaweza kufanyika wakati wowote ndani ya chama hicho, Mwananchi imeelezwa.

Taarifa kutoka vyanzo vya kuaminika ndani ya CCM zinaeleza mchakato wa kufanya mabadiliko unaendelea ukitarajia kugusa safu za juu ya uongozi wa chama hicho tawala.

Endapo hilo litatimia basi CCM itakuwa imefanya mabadiliko katika kipindi cha miezi sita, tangu ilipofanya hivyo Agosti 23, 2025 ambapo Dk Asha-Rose Migiro aliteuliwa kuwa Katibu Mkuu wa chama hicho.

Hata hivyo, wachambuzi wa siasa za Tanzania waliozungumza na Mwananchi wamesema huenda kukawa na mabadiliko hayo, hasa wakati ambapo CCM inatakiwa ijikite katika kuitetea Serikali pamoja na maandalizi ya uchaguzi mkuu wa ndani wa chama hicho.

Duru za ndani zinasema hata kikao cha kawaida cha Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM kilichoketi jana Jumatano, Februari 25, 2026 jijini Dodoma, kilichongozwa na mwenyekiti wa chama hicho, Rais Samia Suluhu Hassan huenda ni sehemu ya mpango huo.

Taarifa zinadai sekretarieti ya CCM huenda ikamgusa Dk Migiro, aliyewahi kuwa Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN) pamoja na viongozi wengine kadhaa waandamizi.

“Kuna mabadiliko yanakuja, dalili zote zinaonyesha sekretarieti ya Dk Migiro huenda ikafumuliwa, wapo ambao hawaendani na kasi hasa kipindi hiki ambacho chama kinapaswa kusimama na Serikali kutokana na yaliyotokea Oktoba 29 mwaka jana,” kimedai chanzo hicho na kuongeza:

“Unajua mwakani kuna uchaguzi wa ndani ya chama, kwa hiyo unapaswa kuwa na timu imara kwelikweli na baadhi ya wajumbe nasikia sikia wameomba kupumzika kwani hekaheka zimekuwa kubwa na presha inaongezeko, hivyo wanaona pumzi inakata.”

Chanzo hicho kimedai baada ya Kamati Kuu, NEC itakutana wakati wowote

“Kinachosubiriwa ni Halmashauri Kuu ya Taifa, ambayo huko sasa kuna lolote linaweza kwenda kutokea, wacha tusubiri.”

Dk Migiro aliteuliwa kushika wadhifa huo Agosti 23, 2025 siku tano kabla ya CCM kuzindua kampeni zake za kutetea kiti cha urais, Agosti 28, 2025.

Dk Migiro aliyeweka rekodi ya kuwa mwanamke wa kwanza kuwa Katibu Mkuu, tangu kuanzishwa kwa chama hicho, mwaka 1977 alichukua nafasi ya Dk Emmanuel Nchimbi, aliyeteuliwa na chama hicho kuwa mgombea mwenza na sasa ni makamu wa Rais.

Katika mabadiliko ya Agosti 2025 ilishuhudiwa Kenani Kihongosi, aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Arusha akichaguliwa kuwa Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo, nafasi iliyokuwa inashikiliwa na Amos Makalla ambaye walibadilisha nafasi.

Pia, katika mabadiliko hayo Joshua Mirumbe aliteuliwa na NEC kuwa Katibu wa Uchumi na Fedha, nafasi iliyokuwa ikishikiliwa na Dk Frank Haule, aliyeteuliwa kuwa Katiba Tawala wa Mkoa wa Songwe.

Aidha, NEC pia ilimteua Halid Mwinyi kuwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM), akichukua nafasi ya Jokate Mwegelo.

Zikiwa zimepita siku 184 tangu CCM ifanye mabadiliko katika sekretarieti yake, taarifa zinadai bado unaonekana umuhimu wa kufanya mabadiliko na hivyo wakati wowote ndani ya wiki hii kikao cha Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM (NEC) kitaketi, pamoja na mambo mengine kujadili suala hilo.

Kikao hicho cha NEC kitakuwa cha kwanza tangu kumalizika kwa Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025.

Mbali na kikao cha NEC pia kuna taarifa zisizo rasmi kwamba pia unaweza kuitishwa Mkutano Mkuu maalumu utakaofanyika kwa njia ya mtandao, ambao hata hivyo ajenda yake haijafahamika.

CCM ilifanya Mkutano Mkuu Maalumu kwa njia ya mtandao Julai 26, 2025, ambapo wajumbe kutoka mikoa na wilaya mbalimbali walishiriki na kupitisha mambo kadhaa ya chama, yakiwemo mabadiliko ya katiba.

Vyanzo vingine vinaeleza vikao hivyo vya CCM vitapokea taarifa kuhusu kikao cha Kamati Maalumu ya CCM Zanzibar kilichoketi Februari 19, 2026 chini ya Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara na Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi, ambapo wajumbe walijadili maendeleo ya mazungumzo ya kupata maridhiano kati ya CCM na ACT – Wazalendo kuhusu Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK) Zanzibar.

Akizungumzia taarifa hizo, Mchambuzi wa siasa, Dk Richard Mbunda amesema haishangazi kwa kuwa hivi sasa ni wakati ambao CCM inatakiwa iwe ‘active’, ikiwemo kuitetea Serikali iliyopo madarakani.

“Chama kinatakiwa kiwe mstari wa mbele, mbinu na mikakati kabambe iliyowekwa kuitetea Serikali. Ukiangalia hivi karibuni Kihongosi ameingia kwenye mgogoro na manguli wa CCM, akiwemo Jaji Joseph Warioba na Joseph Butiku.

“Hawa watu (Butiku na Warioba) kimsingi CCM na Serikali wanatakiwa kuwatumia ili kutuliza mambo, sasa anapotoka kiongozi wa chama na kuwasema vibaya ni kama vile anamwagia petroli kwenye moto,” ameeleza Dk Mbunda.

Kwa mujibu wa Dk Mbunda, Dk Migiro ni mtu aliyepoa, akisema ni kiongozi anayefaa kuendesha chama wakati wa utulivu, kwa sababu si mpambanaji wa kukipigania chama.

“Kimsingi chama kweli kimepoa, nadhani kipindi CCM inatakiwa iwe na njia tofauti kabisa kijamii na kujenga uhalali kwa wananchi ili kuibeba Serikali.

“Naweza kuelewa kwa nini huenda kukawa na mabadiliko au panga pangua inayoweza kuja,” amesema Dk Mbunda.

Kwa upande wake, Kiama Mwaimu amesema kukiwa na mabadiliko hayo, sababu zinaweza kuwa mbili kuu, mosi baadhi ya viongozi wa sasa wa sekretarieti wameshindwa kuendana na kasi.

“Mfano Dk Migiro ambaye anaonekana zaidi kama mtendaji wa kitalaamu ambaye si mwanasiasa, na huenda kwa sababu hana uzoefu huo,” amedai Mwaimu.

Mwaimu amesema kwa hali ya mambo inavyoendelea hivi sasa, CCM inahitaji katibu mkuu mwenye karba kama za Abdulrahman Kinana, na mwenye uwezo na utulivu wa kuchambua mambo katika mtizamno wa kisiasa.

“Kinana anajua kuifanya nyeupe, ikaonekana kuwa nyeupe au kuwa nyeusi, huyu ana ufahamu, uzoefu na mbinu za kucheza michezo ya kisiasa. Hivyo CCM wanahitaji katibu mkuu wa aina hii maana siasa ni kitu kingine,” ameeleza Mwaimu.

Mchambuzi mwingine wa siasa, Ali Makame amesema tangu kumalizika kwa uchaguzi mkuu wa Oktoba 29, 2025, sekretarieti ya CCM haijawa na nguvu ambayo wananchi wanaitegemea.

Makame amesema kuna hoja nyingi za nchi zinazozungumzwa, lakini hazipati majibu yanayoridhisha kutoka ndani ya CCM.

“Inavyoonekana ndani ya CCM wakati wa kupitisha wagombea ubunge na udiwani kulikuwa na malalamiko hasa kwa waliokatwa. Ukiangalia nguvu za waliopo sasa na ukiunganisha CCM na uchaguzi wa mwaka 2027, lazima kuweka sekretarieti nzuri, endapo watafanya hivyo,”

“Lazima wapate safu nzuri ya kuingia nayo kwenye uchaguzi wa ndani wa mwaka 2027. CCM ni chama kikubwa, kuna mambo mengine siri wanazihifadhi, lakini unapoona wanafanya mabadiliko hayo wanarekebisha mapungufu yaliyopo,” amesema Makame.

Mbali na hilo, Makame amesema kuna siku 100 za Rais Samia zimekamilika hivi karibuni, kuna baadhi ya ahadi alizitoa ikiwemo ya upatikanaji wa Katiba Mpya haijatekelezwa katika siku hizo.

Makame amesema huenda kukawa na hayo mabadiliko ili kupata sekretarieti itakayosimamia mchakato huo, lakini pia ni sehemu maandalizi ya kujipanga na uchaguzi wa ndani wa CCM wa 2027 na ule uchaguzi mkuu wa mwaka 2030.

“Wataukabili vipi mchakato huo kama sekretarieti ipo legelege? Lazima kuwepo na sekretarieti imara. Uchaguzi wa mwaka 2030 utakuwa mzito ndani ya CCM, maana kutakuwa na wagombea wapya Tanzania Bara na Zanzibar,” amesema.