Vatican. Kiongozi wa kanisa Katoliki duniani, Papa Leo XIV, anatarajia kufanya ziara nchini Algeria, Cameroon, Angola, na Equatorial Guinea katikati ya Aprili taarifa iliyotolewa na Vatican Februari 25, 2026.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo kituo cha kwanza katika ziara yake ya siku 10 kitakuwa miji ya Algiers na Annaba kuanzia Aprili 13 hadi 15, 2026. Ziara hii itakuwa ya kwanza ya kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani nchini Algeria, nchi ambayo Uislamu ndio dini ya serikali.
Desemba mwaka uliopita, Papa Leo alitangaza nia yake ya kufanya ziara nchini Algeria kuzuru maeneo ambayo Mtakatifu Augustine aliishi, lakini pia kuendelea na mazungumzo na kujenga mahusiano kati ya ulimwengu wa Kikristo na Kiislamu.
Ziara hiyo inalenga kufanya mazungumzo kati ya dini mbalimbali. Kisha Papa atasafiri hadi Yaoundé, Bamenda, na Douala nchini Cameroon kuanzia Aprili 15 hadi 18. kuanzia Aprili 18 hadi 21, atazuru Luanda, Muxima, na Saurimo nchini Angola.
Nchi zote mbili zinakabiliwa na migogoro mikubwa ya kisiasa na maandamano makubwa ya kiraia. Ziara ya Papa Leo inalenga kutoa fursa ya wito wa amani dhidi ya mandhari ya kidini inayobadilika haraka, kulingana na taarifa kwa vyombo vya habari vya Vatican.
Papa Leo atahitimisha ziara yake barani Afrika Malabo, Mongomo, na Bata nchini Equatorial Guinea kuanzia Aprili 21 hadi 23, 2026.