Rithe: Tutaadhimisha mwezi wa wanawake kwa kuwakumbuka waliopoteza maisha Oktoba 29, 2025

Dar es Salaam. Ngome ya Wanawake ya Chama cha ACT-Wazalendo imetangaza kuadhimisha Siku ya Wanawake Duniani, pamoja na mwezi mzima wa Machi, kwa kuwakumbuka waliopoteza maisha wakati wa vurugu zilizotokea katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025.

Vurugu hizo zilisababisha vifo vya watu kadhaa, majeruhi na uharibifu wa mali za umma na binafsi. Aidha, zilisababisha kusimamishwa kwa shughuli mbalimbali za kijamii na kiuchumi.

Akizungumza na waandishi wa habari leo, Februari 26, 2025, jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa Ngome hiyo, Janeth Rithe amesema maadhimisho ya mwaka huu yatakuwa ya kipekee, yakijumuisha maombolezo, ibada na matendo ya huruma kwa waathirika.

Rithe amesema watatumia kipindi hicho kufanya maombi ya kuliombea Taifa, kuwaombea waliopoteza maisha pamoja na wale waliojeruhiwa katika matukio ya Oktoba 29, 2025.

Pia, watafanya ziara ya kuwatembelea wazee na kuwafariji yatima ambao baadhi yao walipoteza wazazi wakati wa vurugu zilizotokea wakati wa uchaguzi Oktoba 29, 2025.

“Tumeamua kuwatembelea wazee ili kuwafariji na kuwakumbusha kuwa wao ni tunu na ushauri wao ni muhimu katika kuhakikisha nchi inakuwa na amani,” amesema.

Ameeleza kuwa wanatarajia kufanya usafi katika vituo mbalimbali nchini na kufanya zoezi la kuchangia damu kama ishara ya kuonyesha upendo na shukrani kwa madaktari waliohangaika usiku na mchana kuokoa maisha ya majeruhi wa Oktoba 29, 2025.

“Pia, tunatarajia kuzuru makaburi ya baadhi ya watu waliopoteza maisha Oktoba 29, 2025 na kwenda kuziona familia zao na kuzifariji, kufanya mikutano na hitima kwa upande wa bara na Zanzibar kwa ajili ya kuwaombea wapigania haki wote waliotangulia mbele za haki.

“Tuna mpango wa kuzindua mnara maalumu kama sehemu ya kuwaenzi wote waliopoteza maisha Oktoba 29, 2025 na tutaupamba kwa mashada ya maua,” amesema.

Maadhimisho ya Siku ya Mwanamke Duniani hufanyika kila Machi 8 duniani kote, yakilenga kuenzi mchango wa wanawake katika nyanja mbalimbali za kijamii, kiuchumi na kisiasa.