Sakata la Sowah Simba, hiki ndicho alichoiambia Mwanaspoti

PALE Simba sakata jipya kwa sasa ni juu ya mshambuliaji Jonathan Sowah ambaye inaelezwa ameondolewa kambini, huku yeye mwenyewe akivunja ukimya kwa kueleza kilichotokea.

Jana usiku Simba ilikuwa katika Uwanja wa Jamhuri, Dodoma ikicheza mechi ya Ligi Kuu Bara dhidi ya Dodoma Jiji, lakini Sowah kuanzia juzi alikuwa jijini Dar es Salaam.

Inadaiwa kwamba Simba ilimrudisha Sowah ili kukutana na uongozi wa klabu kufanya kikao ambacho kilitakiwa kufanyika juzi asubuhi, lakini kikaahirishwa kwa sababu za kiuongozi.

Baada ya kuzuka kwa taarifa hizo, Mwanaspoti lilimtafuta Sowah ambaye ameonyesha kushangazwa na madai anayoelekezewa akisema hakuna kitu cha namna hiyo.


Sowah alisema hata wakati anapewa taarifa ya kutakiwa kurudi Dar ilimkuta akiwa chumbani kwake amepumzika.

“Sijajua kwanini nimeambiwa natakiwa kurudi Dar es Salaam. Alinifuata meneja wa timu akanipa ujumbe huo. Kwa kuwa ni kiongozi wangu sikutakiwa kumhoji sana zaidi ya kutekeleza.

“Kuhusu madai ya utovu wa nidhamu, nasikia kutoka kwako lakini pia nimeona watu wanaandika tu kwenye mitandao ya kijamii. Nimesoma, ila nasubiri kwanza hicho kikao cha uongozi kujua sababu.

“Nikimalizana na uongozi ndio nitawarudia hao ambao wameandika vitu bila kujua ukweli kutoka kwangu. Mimi sio mtu wa kukubali jina langu kuchafuliwa kirahisi,” alisema Sowah.


Kabla ya kuondoka Dodoma, Sowah alisema alikuwa amejiandaa kuendelea kuitumikia Simba baada ya adhabu yake ya kusimamishwa mechi tano na Bodi ya Ligi kumalizika wikiendi iliyopita waliyoshinda mabao 2-0 dhidi ya Tanzania Prisons.

“Unajua nilikuwa nimesimamishwa. Kwa hiyo nilikuwa nimejiandaa vizuri kuanza kuichezea timu yangu, lakini naona nimeambiwa tena nirudi Dar es Salaam, imeniumiza.

“Kikao niliambiwa kingefanyika jana (juzi), lakini baadaye nikajulishwa kimesogezwa mbele mpaka watakaponiambia. Kwa hiyo nasubiri kwanza hicho kikao,” alisema Sowah.

Desemba 17, 2025, Sowah na Allasane Kante waliadhibiwa na Kamati ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi ya Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) kutokana na makosa ya utovu wa nidhamu waliyoyafanya dhidi ya Azam FC kwenye mechi ya Ligi Kuu Bara iliyochezwa Desemba 7, 2025.

Nyota hao waliotua Simba wakati wa dirisha kubwa la usajili msimu huu, wameshamaliza adhabu  baada ya kukosekana mechi tano mfululizo zikiwamo nne za Ligi Kuu Bara dhidi ya Mtibwa Sugar, Mashujaa, KMC na Tanzania Prisons. Nyingine ni ya Kombe la Shirikisho (FA) dhidi ya Greenland.


Mshambuliaji huyo alitua Simba msimu huu akitokea Singida Black Stars ambako kiwango kizuri cha ufungaji alichokionyesha msimu uliopita akicheza takribani miezi sita na kufunga mabao 13 katika mechi 14 za Ligi Kuu Bara, kiliwavutia Simba kumsajili kwa matumaini ya kuongeza makali safu ya ushambuliaji.

Akiwa Simba, msimu huu kabla ya jana timu hiyo ilipokabiliana na Dodoma Jiji, ilikuwa imecheza mechi 23 za mashindano tofauti (Ligi ya Mabingwa 10, Ligi Kuu Bara 9, Kombe la Mapinduzi 3 na Ngao ya Jamii 1), huku Sowah akicheza mechi 11 kwa dakika 477.

Mechi hizo ni Ligi Kuu Bara (4), Ligi ya Mabingwa Afrika (6) na Kombe la Mapinduzi (1) ambapo amefanikiwa kufunga mabao matatu yote kwenye Ligi Kuu Bara dhidi ya Fountain Gate, JKT Tanzania na Mbeya City.

Kuhusu Sowah kuondolewa kambini, Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally, alisema: “Kwa sasa sina majibu ya moja kwa moja, niacheni nifuatilie baada ya mechi (dhidi ya Dodoma Jiji) nitakuwa na majibu kamili.”