Serikali yafafanua meli iliyokamatwa na dawa za kulevya

Dar es Salaam. Serikali ya Tanzania imeeleza hatua zilizochukuliwa kufuatia kukamatwa kwa meli yenye bendera ya Tanzania nchini El Salvador, iliyodaiwa kubeba tani 6.6 za dawa za kulevya aina ya kokeini.

Kwa mujibu wa Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa, baada ya kusambaa kwa taarifa za kukamatwa kwa meli hiyo Februari 17 mwaka huu, siku iliyofuata Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar iliifutia meli hiyo usajili wake.

Msigwa ameeleza hayo leo Alhamisi, Februari 26, 2026, wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mafanikio ya sekta za usafiri na uchukuzi pamoja na hatua mbalimbali zinazochukuliwa na Serikali kuboresha miundombinu.

Katika mkutano huo, waandishi walitaka kujua ni hatua gani Serikali imechukua kuhusu meli hiyo. Akijibu swali hilo, Msigwa alianza kwa kusema:

“Tumepokea taarifa hiyo, na baada ya kupitia takwimu zetu, tumebaini kuwa ni meli iliyokuwa imesajiliwa Zanzibar.

 “Wenzetu wameisajili hii meli kupitiwa wakala, ambapo ni utaratibu kama nchi kupitia Shirika la Meli Duniani. Kiutaratibu ukiwa katika lile shirika una uwezo wa kuwa na mawakala mbalimbali watakaosaidia kusajili meli katika maeneo mbalimbali,” amesema.

Msigwa amefafanua kuwa usajili wa meli hauimaanishi kuwa chombo hicho kinatoka au kinamilikiwa na raia wa nchi husika, kwani meli zinaweza kusajiliwa katika nchi moja na kutumika katika nchi nyingine.

Amesema ndiyo maana katika tukio la meli iliyokamatwa El Salvador, hakuna Mtanzania aliyeshikiliwa.

Kuhusu hatua nyingine zilizochukuliwa, Msigwa amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar iliwatafuta wamiliki wa meli hiyo ili kupata taarifa za kina. Hata hivyo, wamiliki hao hawakutoa ushirikiano wa kutosha kwa mamlaka husika.

“Pili ile kampuni ya meli imepigwa faini ya zaidi ya Sh51.08 milioni kwa mujibu wa IMO. Pia, inaendelea kufanya mawasiliano na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki ili kuondokana na utambuzi wowote wa meli hii kimataifa.

“Zaidi ya hapo wanaendelea kufanya tathimini ya mawakala wote walioingia nao mkataba ya kusajili meli ili wale wababaishaji waondolewe kwenye mfumo wa usajili. Hizo ndio hatua ambazo Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imezichukua haraka,” ameeleza Msigwa.