Unguja. Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) imekiri kuwepo kwa changamoto na vihatarishi vya matumizi yasiyo salama ya mitandao hususani kwa vijana huku ikiahidi kuitafutia utatuzi.
Hayo yamebainishwa leo Alhamisi Februari 26, 2026 na Naibu Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari na Ubunifu Zanzibar, Mohammed Sijamini Mohamed wakati akijibu swali la Mwakilishi wa Chakechake, Abdulwahab Said Abuubakar (CCM) katika Baraza la Wawakilishi.
Mwakilishi huyo ametaka kufahamu mikakati ya Serikali ya kuwalinda wananchi hususani vijana dhidi ya madhara na vihatarishi vinavyotokana na matumizi ya mitandao (intaneti).
“Serikali inatekeleza sheria ya makosa ya mtandao ya mwaka 2015 kwa lengo la kudhibiti na kukabiliana na uhalifu wa mtandao, Sheria ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi ya mwaka 2022 kwa ajili ya kulinda faragha na usalama wa taarifa za wananchi,” amesema Sijamini.
Akitoa ufafanuzi wa hilo, Naibu Waziri huyo amesema Serikali inaendelea kutoa elimu na kuhamasisha jamii juu ya matumizi salama ya mitandao, kupitia wizara hiyo imefanikiwa kutoa elimu ya matumizi ili kuwawezesha kutambua vihatarishi hivyo.
Vilevile, amesema wizara hiyo imetoa uelewa na elimu ya usalama mtandaoni kwa wananchi 302 wakiwemo masheha, wataalamu wa Tehama na viongozi ili wajiandae pamoja na kukabiliana na vihatarishi vinavyotokana na matumizi hayo.
“Serikali imejenga vituo vya Tehama jamii kila wilaya kwa lengo la kutoa elimu sahihi ya matumizi ya mtandao hasa kwa vijana, ambapo hadi sasa vijana 7,937 wameshapata mafunzo kupitia vituo hivyo,” amesema.
Sijamini amesema Serikali inaendelea kuimarisha usalama wa mifumo ya kidijitali kwa kuwekeza katika miundombinu ya Tehama ikiwemo vituo vya kuhifadhi taarifa na mtandao wa mkonga wa mawasiliano, kuhakikisha mifumo ya Serikali inalindwa dhidi ya udukuzi na vitisho vya mtandao.
Pia, ameeleza Serikali inaendelea kuimarisha usalama na usimamizi wa mifumo ya serikali mtandao ambapo kupitia Mamlaka ya Serikali Mtandao Zanzibar (eGAZ) ina jukumu la kusimamia, kuratibu na kuhakikisha mifumo yote inazingatia viwango vya usalama wa taarifa.
Hata hivyo, amesema Serikali itaendelea kuboresha sera, sheria, mifumo na programu zake ili kuhakikisha matumizi ya mtandao yanakuwa salama, yenye tija na yanachangia maendeleo ya kijamii na kiuchumi bila kuhatarisha usalama, maadili na ustawi wa wananchi.