Uhalali Tume ya Matukio ya Oktoba 29 kuamuliwa Machi 6

Dar es Salaam. Wakati Tume ya Rais ya Kuchunguza Matukio ya Uvunjifu wa Amani wakati na baada ya  Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025 ikiongezewa siku 42 ili kukamilisha jukumu hilo, Mahakama Kuu imepanga kutoa uamuzi wa shauri la kupinga uhalali wake Machi 6, 2026.

Mahakama Kuu Masjala Ndogo Dar es Salaam imepenga tarehe hiyo, baada ya kukamilisha usikilizwaji wa hoja za pande zote leo Alhamisi, Februari 26, 2026.

Oktoba 29, siku ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2025 nchini kuliibuka vurugu zilizosababisha uharibifu wa miundombinu na mali za umma na watu binafsi pamoja na vifo na majeruhi, kufuatia maandamano ya kupinga uchaguzi huo katika majiji na miji mbalimbali nchini.

Novemba 18, 2025 Rais Samia Suluhu Hassan aliunda Tume kuchunguza matukio hayo, inayoongozwa Jaji Mkuu wa Tanzania mstaafu, Mohamed Chande na akaizindua Novemba 20, 2025 huku akiipa miezi mitatu kukamilisha jukumu hilo.

Siku hizo 90 zilikamilika Februari 20 na imeongezewa siku 42 ili kukamilisha shughuli hiyo.

Hata hivyo, wanaharakati na watetezi wa haki za binadamu, Rosemary Mwakitwange na mawakili wawili Edward Heche na Deogratius Mahinyila, wamefungua shauri la maombi ya mapitio ya mahakama dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) na wenzake, baada ya kupata ridhaa ya mahakama hiyo.

Wajibu maombi wengine ni Jaji Mkuu mstaafu, Chande ( mwenyekiti wa tume hiyo) na wajumbe, Jaji Mkuu mstaafu wa Tanzania, Profesa Ibrahim Juma, Katibu Mkuu Kiongozi mstaafu, Balozi Ombeni Sefue; Radhia Msuya, Balozi Paul Meela na Mkuu wa Jeshi la Polisi mstaafu (IGP), Said Mwema.

Wengine ni Balozi David Kapya, aliyewahi kuwa Katibu Mkuu mstaafu wa Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) na Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa mstaafu, Stergomena Tax na Chama cha Sheria Tanganyika (TLS).

Kwa mujibu wa waombaji, TLS kilichoundwa mwaka 1954 kwa Sheria ya Bunge,  majukumu yake ya msingi ni pamoja na kukuza utawala wa sheria, uadilifu na uwazi, kulinda na kusaidia umma kupata haki na huduma za kisheria katika masuala yote yanayohusu sheria.

Tume hiyo ilipaswa kumaliza na kukabidhi taarifa yake kabla au kufikia Februari 20, 2026 lakini Februari 22, 2026 Jaji Chande alitangaza tume hiyo kuongezewa muda wa siku 42 kukamilisha kazi hiyo.

Katika shauri hilo waombaji hao ambao wanawakilishwa na mawakili Mpale Mpoki na Hekima Mwasipu wanaiomba Mahakama hiyo itoe amri za kufuta na zuio la uamuzi wa Rais wa uteuzi wa wajumbe wa tume hiyo.

Wanadai kuwa tume hiyo haijakidhi vigezo vya kisheria kwa kuwa uundwaji na uteuzi wa wajumbe wake ulifanywa kwa nia ovu kinyume cha kanuni ya haki asili ya mtu kutokuwa hakimu wa kesi yake mwenyewe.

Wanafafanua hoja hiyo kuwa kwanza, mamlaka ya uteuzi ni mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi, chama tawala, kilichoshiriki na kushinda uchaguzi uliosababisha ghasia wakati na baada ya uchaguzi, na kwa hivyo kina masilahi katika uchaguzi huo na tume hiyo.

Pia wanadai mjumbe Tax ni mtuhumiwa kwani alikuwa Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa wakati ghasia za uchaguzi zilipotokea, alihusika kwa namna moja au nyingine chini ya wizara yake.

Vilevile wanadai majaji wakuu wastaafu hawawezi kuchunguza kwa haki vurugu hizo kwani baadhi ya mali zilizoharibiwa ni za mahakama waliyoiongoza, na kwamba IGP mstaafu hawezi kumchunguza kwa haki, kwa kuwa, IGP aliyepo anaweza kuwa miongoni mwa watuhumiwa.

Wanaongeza kuwa Amiri Jeshi Mkuu, mamlaka ya uteuzi wa tume hiyo (Rais) katika tarehe tofautitofauti alitoa maagizo kwa Polisi na Jeshi kujiandaa kwa ghasia za wakati na baada ya uchaguzi.

Katika hoja nyingine wanadai kuwa uundaji wa tume hiyo umekiuka masharti ya Sheria ya Tume ya Uchunguzi, Sura 32 Marejeo 2023, kifungu cha 16.

Wanadai  kuwa hakuna ufafanuzi wa madhumuni yake yaliyo wazi kama kifungu hicho kinaielekeza mamlaka ya uteuzi  bali  yanategemea hisia tu, kinyume na misingi ya Katiba, utawala bora na utaratibu sahihi wa haki.

Pia wanadai maneno yaliyotumika ‘Uchunguzi wa matukio ya uvunjifu wa amani’ yanapunguza na kudharau vifo, watu waliopotea, miili iliyopotea, majeraha na athari kubwa kwa umma kwa jumla.

Wanafafanua kuwa tume hiyo siyo huru kwani haikujumuisha wajumbe kutoka vyama huru vya kitaaluma kama TLS, Chama cha Madaktari, mashirika ya kijamii, ya kidini kama Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata), Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) au wadau wengine huru wasio na mgongano wa masilahi, kuepuka upendeleo kwa mamlaka ya uteuzi.

Wanadai wajumbe wote ni watumishi wa umma waliostaafu, waliokuwa na nafasi za kuteuliwa na Rais, waliokula kiapo cha siri kwa Rais, ambacho hakijafutwa wakati wa kustaafu au hadi tarehe ya uteuzi kama wajumbe wa tume inayopingwa.

Hivyo, wanadai wajumbe hao hawawezi kuchunguza mamlaka ya uteuzi wao.

Shauri hilo la maombi ya mapitio ya Mahakama namba 32537 la mwaka 2026 linalohoji uhalali wa tume hiyo limesikilizwa na Jaji Awamu Mbagwa leo Februari 26, 2026.

Wakati wa usikilizwaji huo wakili Mwasipu kwa niaba ya waombaji amewasilisha hoja akifafanua kwa undani sababu za madai yao katika hati ya maombi na kiapo cha waombaji.

Wakili wa Serikali, Erigh Rumisha akisaidiana na Daniel Nyakiha kwa niaba ya wajibu maombi wote amepinga madai na hoja za waombaji kuwa hazina mashiko, pamoja na mambo mengine akidai uteuzi wa wajumbe hao umekidhi matakwa ya kisheria.

Hata hivyo, wakili Ferdinand Makore kwa niaba ya mjibu maombi wa 10, TLS ameunga mkono madai na hoja za wadai.

Pamoja na mambo mengine Wakili Makore amedai kuwa tume hiyo ni batili kwa kuwa haikutangazwa kwenye Gazeti la Serikali na wala wajumbe wa tume hiyo hawakula viapo kabla ya kuanza kazi yao, kinyume na matakwa ya sheria.

Wakili Makore amedai kuwa kwa mujibu wa kifungu cha 20 cha Sheria ya Tume ya Uchunguzi ili wajumbe wa tume wawe halali wanapaswa watangazwe katika Gazeti la Serikali.

Amefafanua kuwa Amri C. 27 ya Kanuni za Kudumu za Utumishi wa Umma za Mwaka 2009 inataka machapisho na matangazo yote ya Serikali kuchapishwa na kutangazwa siku ya Ijumaa ya wiki husika.

Hata hivyo amedai kuwa nakala ya gazeti lililowasilishwa na wajibu maombi kama kielelezo kuwa tume hiyo ilitangazwa si halali kwa kuwa limechapishwa Novemba 20, 2025 siku ya Alhamisi, hivyo kuifanya tume hiyo kutokuwa halali.

Pia wakili Makore amedai kuwa kwa mujibu wa kifungu cha 7 cha sheria hiyo ili wajumbe wa tume wawe halali wanapaswa kula viapo kwanza kabla ya kuanza majukumu yao.

Hata hivyo, amedai wajibu maombi katika majibu yao na viapo vyao kinzani hakuna mahali wanapoeleza kama walikula viapo wala kuambatanisha na fomu ya viapo.

Jaji Mbagwa baada ya kusikiliza hoja za pande zote ndipo akapanga kutoa uamuzi Machi 6, 2026.