Usafiri mwendokasi mguu sawa Gongo la Mboto

Dar es Salaam. Awamu ya tatu ya usafiri usafiri wa mabasi yaendayo haraka iko mbioni kuanza kati ya Gongo la Mboto na katikati ya Jiji la Dar es Salaam, imefahamika.

Hatua hiyo ni baada ya Serikali kutangaza kuwa mabasi 49 yapo tayari na wakati wowote yataingia barabarani kutoa huduma huku mengine takribani 99 yakiwa bandarini yakisubiri taratibu za kutoka.

Hayo yamebainishwa leo Alhamisi Februari 26, 2026 na Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa wakati akizungumza na wanahabari kuhusu sekta ya usafiri na usafirishaji mkutano uliofanyika Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere.

Alipoulizwa ni lini mabasi hayo yataingia barabarani, Msigwa amesema ni ngumu kusema siku fulani yataanza kufanya kazi kwa sababu kuna maandalizi ya mwisho yanafanyika na wakati wowote huduma zitaanza kutolewa.

“Yapo mambo ya timu na mifumo yanakamilishwa. Nisingependa kusema ni lini rasmi yataanza kazi, lakini yako tayari na muda wowote yataanza kutoa huduma,” amesema Msigwa.

Msigwa amebainisha mabasi mengine 99 tayari yamewasili nchini na yako bandarini yakikamilisha taratibu za kupokewa kabla ya kuunganishwa na mengine kutoa huduma kati ya Gongo la Mboto hadi Posta.

Hatua hiyo inatajwa kuwa itapunguza kwa kiasi kikubwa adha ya usafiri inayowakabili wakazi wa Gongo la Mboto na viunga vyake, ambao kwa muda mrefu wamekuwa wakiusubiria.

Mmoja wa wakazi wa maeneo ya Gongo la Mboto, Amina Juma amesema kuanza kwa huduma ya mabasi awamu ya tatu kutaleta matumaini makubwa wakazi wa Gongo la Mboto na maeneo jirani ya Jiji la Dar es Salaam.

 “Ujio wa mabasi ya mwendokasi  ni hatua muhimu sana katika kuboresha usafiri wa kila siku kwa wakazi wa Gongo la Mboto na kwa wananchi wote kwa ujmla,”

 “Tumekuwa tukikumbana na changamoto za usafiri, ikiwemo foleni ndefu, gharama kubwa za nauli, pamoja na kuchelewa kufika kazini au kwenye shughuli za kimaendeleo,” ameeleza Amina.

Naye mkazi Majumba Sita, Thomson Mwakalinga, amesema usafiri huo utaleta unafuu mkubwa kwa wafanyakazi wanaosafiri kila siku kwenda katikati ya jiji.

“Kwa sasa natumia zaidi ya saa mbili kufika Posta, lakini sasa safari itapungua kwa kiasi kikubwa,” ameeleza.

Pia, katika mkutano huo Msigwa ameeleza hatua mbalimbali zinazochukuliwa na Serikali katika kuboresha usalama, miundombinu ya viwanja vya ndege na ujenzi wa majengo ya abiria ili kuchochea sekta ya usafiri wa anga nchini.

“Tunafanya uwekezaji huu ili kuvutia kampuni kubwa za kimataifa zije kufanya kazi.Tayari kuna kampuni saba zinazotoa huduma katika viwanja vyetu,” amesema Msigwa.

Katika hatua nyingine Msigwa amesema moja ya jitihada zinazofanywa na Serikali kuboresha usafiri wa anga kwa soko la ndani ni kununua ndege nyingine nne aina ya Bombadier ndani ya mwaka huu.

“Leo nipo hapa kuwaambia ndani ya mwaka huu Serikali itanunua ndege mpya nne aina ya Bombadier ili kuimarisha mtandao wetu wa ndege wa ATCL (Shirika la Ndege la Tanzania),” amesema Msigwa.